Wanne wahukumiwa kunyongwa hadi kufa Shinyanga
Muktasari:
- Watu Wanne waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, wamehukumiwa Kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kuua mume na mke kwa kukusudia.
Shinyanga. Watu wanne waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kuua wanandoa kwa kukusudia.
Watu hao ni Salawa Ndelema, Mayala Charles, Shija Ngelanija na Emanuel Manoni.
Hukumu hiyo imetolewa Septembe 21, 2023 katika Mahakama hiyo mbele ya Jaji Seif Mwinshehe Kulita ambapo amesema baada ya kusikiliza mashahidi saba wa upande wa Jamhuri ushahidi huo pasipo shaka watu hao walifanya mauaji hayo kwa kukusudia.
Tukio hilo la mauaji lilitokea katika Kijiji cha Masengwa Halmashauri ya Shinyanga mwaka 2019 baada ya kaka wa marehemu kukodi washtakiwa namba 2 hadi 4 kwa kuwalipa Sh1.2 milioni ili kuwauwa kaka yake pamoja na mkewe.
Katika shitaka hilo namba 14 la mwaka 2022 washtakiwa wakiongozwa na Salawa Ndeleama aliyewalipa Sh1.2 milioni kwenda kuumua kaka yake, Mayala Ndelema na Mkewe, Nyamizi Mserengeti; fedha hizo zilitumika kununua panga pamoja na shoka vifaa vilivyotumika kuondoa uhai wao kisha kuachwa eneo la tukio.
Jaji Kulita amesema katika ushahidi wa shahidi wa 5 ulionesha kuwa walikwenda eneo la tukio na kufanya uchunguzi, ambapo mshitakiwa wa nne alikiri kushiriki kwa kulipwa ujira wa Sh400,000 ambazo zilikuwa zimefichwa chini ya ardhi.
Aidha katika ushahidi wa shahidi wa 3, 4, 6 na 7 umeonesha na kutoacha shaka kuwa washtikiwa hao walifanya kosa hilo kwa kukusudia baada ya kupewa pesa ili kwenda kutekeleza mauaji hayo nyumbani kwa marehemu.
Katika maelezo yake, Jaji Kulita amesema washtakiwa hao walipewa nafasi ya kujitetea ambapo kila mmoja alieza jinsi tukio hilo lilivyomkuta ambapo maelezo yao hayakuwa na mashiko mbele ya Mahakama hiyo.
“Ushahidi umeweka wazi kuwa mshitakiwa no 1 Salawa Ndelema ambaye ni mdogo wa Marehemu Mayala Ndelema aliwakodisha watuhumiwa namba 2, 3 na 4 kwa sababu alikuwa na mgogoro wa ardhi na kaka yake huyo huku akimtuhumu shemeji yake marehemu, Nyamizi Mserengeti kuwa ni mchawi na amekuwa akimloga”
Jaji kulita baada ya kupitia Ushahidi wa mashahidi saba kutoka upande wa Jamhuri ambao haukucha shaka, watuhumiwa wamekutwa na hatia ya kuua kwa kukusudia na kuwapa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Kesi hiyo upande wa Jamhuri ilikuwa na mawakili watatu wakiongozwa na Shani Wampumbulya, Upendo Mwakimonga na Magoti Nyamunyaga huku upande wa utetezi ukiwa na mawakili wanne wakiongozwa na Wakili Geofrey Tuli.