Waonya kukithiri michezo ya kubahatisha nchini

Muktasari:

  • Inaelezwa kuwa baadhi ya vijana wanaacha kufanya shughuli za kuwaingia kipato na badala yake wanatumia muda mwingi kucheza kamari kwa matarajio ya kupata fedha ndani ya muda mfupi.

Dar es Salaam. Wakati kampuni za michezo ya kubahatisha na kamari zikiendelea kukithiri na kuongeza watu wanaoangukia kwenye uraibu wa michezo hiyo, watalaam wa ustawi wa jamii wametoa angalizo  wakisema hiyo sio dalili njema kwa jamii.

Inaelezwa kuwa baadhi ya vijana wanaacha kufanya shughuli za kuwaingia kipato na badala yake wanatumia muda mwingi kucheza kamari kwa matarajio ya kupata fedha ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, wengi wao wanaishia kwenye lindi la umaskini unaoenda kuathiri hadi familia na jamii kwa ujumla na kuendelea mnyororo wa umaskini.

Hayo yameleezwa jana Novemba 11 jijini hapa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wataalam wa Ustawi wa Jamii  (Taswo), Dunstan Haule wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutao wa mwaka wa chama hicho utakaofanyika Novemba 14 hadi 16 mkoani Mbeya.

Haule amebainisha kuwa kwa sasa si vijana pekee, bali hadi watu wazima wanajihusisha na michezo hiyo ambayo hatima yake ni kuwaongezea msongo wa mawazo.

“Siku hizi hadi watu wazima, wapo wengine wastaafu kabisa wanacheza kamari. Vijana kinachowasukuma huko ni uvivu wa kufanya kazi lakini wanatamani maisha mazuri hivyo wanaona kamari ndiyo njia ya mkato ya kuwa milionea.

“Kinachotokea badala ya kupata fedha yeye ndiye anatumia fedha na muda mwingi kucheza kamari inayomfanywa ashindwe kufanya shughuli nyingine. Tunakutana na kesi za waliooa wanashindwa kuhudumia familia kwa sababu ya kamari hii ni changamoto kubwa kwenye jamii yetu,” amesema Haule.

Hii si mara ya kwanza kwa suala la kamari kupigiwa kelele, Agosti mwaka huu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lugano Kusiluka amesema wanafunzi  wengi wa vyuo vikuu wanamaliza fedha kwenye kamari na kujikuta wanaingia kwenye umaskini.

Akizungumza kuhusu mkutano huo, Makamu mwenyekiti wa Taswo, Salma Fundi amesema mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo umaskini katika jamii, usawa wa kijinsia, watoto, vijana, wazee, wenyeulemavu na unyanyasaji wa kijinsia.

Amesema mkutano huo utabebwa na kauli mbiu, ‘Tuheshimu tofauti zetu kupitia hatua za pamoja za kijamii’ na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson.

“Kauli mbiu yetu inasisitia umuhimu wa kuheshimu tofauti za kiitikadi, kidini, kikabila na kijinsia katika jamii.
"Wanataaluma wa ustawi wa jamii tunaamini kwamba ni muhimu kuheshimu tofauti za watu na kwamba tunaweza kufanya hivyo kwa kuchukua hatua za pamoja za kijamii.

"Tunaishi katika jamii ambayo ina tofauti nyingi, ila tofauti hizi zinaweza kuwa chanzo cha nguvu na maelewano. Jamii bora ni ile inayoheshimu tofauti za watu na ambayo inaunda fursa kwa kila mtu kufikiwa ustawi,” amesema Salma.