Wapandishwa kizimbani kujibu mashtaka 11 likiwemo utakatishaji Sh658 milioni

Muktasari:

Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 11 likiwemo la utakatishaji wa fedha zaidi ya Sh658 milioni.



Dar es Salaam. Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 11 likiwemo la utakatishaji wa fedha zaidi ya Sh658 milioni.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga amewataja washtakiwa hao ni mfanyabiashara Ridhiwani Shaban na Moses Nassoro.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili, Mwanga amedai kati ya Agosti 28 hadi Septemba 9, 2022, katika maeneo tofauti nchini washtakiwa hao walikula njama na kutenda kosa la kujipatia Sh658.8 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Mwanga amedai washtakiwa hao walijipatia fedha hizo kutoka kwa Reymond Mavika kwa madai kwamba wataziwekeza katika biashara ya mazao ya kilimo badala yake walitakatisha fedha hizo Kwa kujinunulia vitu mbalimbali.


"Washtakiwa hao walitakatisha fedha hizo kwa kujinunulia vitu mbalimbali huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kujipatia fedha kwa udànganyifu," amedai Mwanga.

Inadaiwa Shabani alizitumia kwa kununua gari aina ya Toyota IST, Music System, gari aina ya Toyota Rush, seti ya Luninga aina ya Goodvision, genereta, taa za disko, trekta na Sh21.4 milioni aliziweka katika akaunti yake ya CRDB.

Mwanga alidai kuwa mshtakiwa Nassoro alizitumia kwa kununua gari aina ya Toyota Harrier, Town Hiace, spea za gari na Sh96 milioni alikutwa amezihifadhi nyumbani kwake Mang'ula, Kilombelo huku akijua ni kosa.

Upelelezi bado haujakamilka na washtakiwa hao walikana makosa yanayowakabili.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkuu, Rhoda  Ngimilanga aliahirisha shauri hilo hadi Juni 21, 2023.