Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wapigakura kuboresha taarifa zao Daftari la Wapiga Kura

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacob Mwambegele

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya  Uchaguzi, Jaji Jacob Mwambegele amesema mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura wenye maboresho makubwa utaanza rasmi Julai Mosi, 2024 mkoani Kigoma, kisha kwenda mikoa ya Katavi na Tabora kwa hatua za awali.

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema mfumo wa uandikishaji wa Daftari la Wapigakura 2024  umeboreshwa ili kutoa fursa kwa mtu aliyepo katika daftari hilo kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia simu au kompyuta.

Imefafanua kuwa baada ya mpiga kura huyo, kukamilisha taratibu zake atalazimika kutembelea kituo anachokusudia kujiandikisha ili kupatiwa kadi yake ya mpigakura.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Juni 7, 2024  na Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacob Mwambegele katika mkutano na vyama vya siasa kuhusu uboreshaji wa Daftari la Wapigakura, mchakato utakaoanza Julai mosi mkoani Kigoma, kisha kwenda Katavi na Tabora kwa awamu ya kwanza.

"Tume inakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ikiwa ni pamoja na kurahisisha mchakato huu wa uboreshaji wa daftari, hii ni kwa mara kwanza mtu aliyepo kwenye daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake," amesema Jaji Mwambegele.

Mbali na hilo, Jaji Mwambegele amesema uboreshaji wa daftari kwa mwaka 2024 utatumia teknolojia ya BvR Kit (biometric voters' registration kits) zilizoboreshwa na kuwekwa programu endeshi za kisasa zaidi.

Amesema uboreshaji wa mwaka 2015 na 2019 ulitumia BVR ambazo hutumika katika kutambua mtu na kumtofautisha na mwingine, lakini kwa mwaka 2024 kutakuwa na utofauti ambapo BVR kits zilizoboreshwa zitatumika.

Amesema BVR kits zitakazotumika zimepunguzwa uzito ili kuleta urahisi wa kubebeka sambamba na kurahisisha shughuli ya uboreshaji wa daftari kuwa jepesi hasa katika maeneo ya vijijini ambapo watendaji hulazimika kubeba vifaa kwa umbali mrefu zaidi.

Akizungumzia mfumo huo, Kailima amesema utawezesha wapigakura walioandikishwa kuanzisha mchakato wa uboreshaji wa taarifa zao kwa njia ya mtandao.

Amesema mfumo huo, Online voters registration system  'OVRS', utaruhusu mtu kutumia simu ya kiganjani au kompyuta, kubadilisha taarifa, kuhama mkoa, wilaya au jimbo au kubatilisha kuhama.

"OVRS umefanyiwa usanifu na kuboreshwa ili kukidhi aina ya BVR kit za kisasa zinazotumia programu endeshi ya androidi. Hii ni tofauti na BVR kit za awali zilizotumia programu endeshi ya windows na zilikuwa na uzito wa kilogramu 35 lakini sasa zimepunguzwa uzito hadi kilogramu 18," amesema Kailima.

Pia, amesema INEC imeshanunua BVR kit 6,000 zinazotumia vishkwambi kuchukua taarifa za wapigakura, ikiwemo picha, alama za vidole na saini.

Kwa mujibu wa Kailima, jumla ya vituo 40,126 vitatumika kwa ajili uandikisha wapigakura katika uboreshaji wa daftari mwaka 2024. Kati ya hivyo, vituo 39, 709 vipo Tanzania Bara na 417 Zanzibar. Amesema hilo ni ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na 37, 814 vilivyotumika 2019/20.

"Wapigakura wapya 5, 586,433 wanatarajiwa kuandikishwa, sawa na asilimia 18.7 ya wapigakura  29,754,699 waliopo katika daftari la wapigakura baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20. Wapigakura 4, 369, 531 wataboreshewa taarifa zao," amesema Kailima.

Katika hatua nyingine, Kailima amesema tume hiyo imeweka utaratibu wa kuwaandikisha wafungwa na wanafunzi waliohukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita na mahabusu ili kuwa wapigakura.

Amesema katika kufanikisha hilo, Tanzania Bara kutakuwa na vituo vya kuandikisha 130 vilivyopo kwenye magereza na Zanzibar vitakuwa 10 katika vyuo vya mafunzo.