Washtakiwa ugaidi wasimulia mazito jela

Waliokuwa washitakiwa wa kesi ya ugaidi wakikumbatiana na  ndugu na jamaa zao baada ya kuachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mtwara jana. Picha na Mwanamkasi Jumbe

Muktasari:

  • Wameishi katika Gereza la Lilungu, Manispaa ya Mtwara kwa miaka zaidi ya minne na nusu, bila ya kuwapo kwa ruhusa ya kutembelewa wala kuonana na ndugu zao.

  

Mtwara. Wameishi katika Gereza la Lilungu, Manispaa ya Mtwara kwa miaka zaidi ya minne na nusu, bila ya kuwapo kwa ruhusa ya kutembelewa wala kuonana na ndugu zao.

Hicho ni kilio kimojawapo cha Omar Salum Bumbo (54), Wazir Suleiman Mkalianganda (36) na Ramadhani Moshi Kakoso (44) waliofikwa na masaibu ya kupelekwa mahabusu gereani mkoani hapa, baada ya kamatwa na kushitakiwa kwa tuhuma za kujiunga na kikundi cha Hizbu Tahir kinachodaiwa kushawishi watu kuanzisha dola ya Kiislamu nchini Tanzania.

Hadi wanaachiwa juzi kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), upelelezi wa kesi dhidi yao ulikuwa haujakamilika.

Bumbo, fundi ujenzi na mkazi wa Tandika, jijini Dar es Salaam, Makaliaganda, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mtwara, na Kakoso, mfanyabiashara na mwalimu wa madrasa, mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam, wamelieleza Mwananchi magumu waliyopitia baada ya kukamatwa.

Akizungumzia maisha ya gerezani mara baada ya kutoka mahakamani jioni ya Februari 23, 2022, Kakoso alisema kwa kipindi chote walichokuwa gerezani hawakuruhusiwa kutembelewa na ndugu

Alisema uongozi wa gereza ulikataa kata kata kutoa kibali hicho, licha ya wao kufanya kila jitihada waruhusiwe kuonana na wapendwa wao.

Alisema waliishi kwa dhiki na tabu lakini walivumilia mpaka siku walipopata nusura ya kuachiwa huru.

Gerezani ni sehemu yenye dhiki kubwa kwa binadamu. Ni sehemu ngumu sana. Tumepoteza biashara zetu, shughuli zimepotea na tumetengana na familia lakini tunaamini Mwenyezi Mungu atatupa mbadala,” alisema Kakoso.

Kwa upande wake, Bumbo, alisema kuwa siku alipokamatwa alianza kupigiwa simu ya kazi ya ujenzi na alipokwenda alikamatwa na kupelekwa Mtwara kisha kushtakiwa kwa ugaidi.

Mtoto wake, Omar Bumbo ameshukuru wadau wote waliosimamia suala hilo hadi baba yake mzazi na wenzie kuachiwa huru.

“Natoa shukrani sana kwa vyombo vya habari, ndugu jamaa na marafiki walisimamia kwa njia moja au nyingine kutoka kwa babangu,” alisema Omar.

Naye Mkaliaganda alisema kuwa siku ya tukio alikuwa akitokea msikitini ndipo wakatokea watu wakamuita kwa jina lake na kujitambulisha kuwa ni wapelelezi na kwamba walikuwa na mazungumzo naye.

Alisema baada ya hapo walimpeleka kituo cha polisi bila kupewa nafasi ya kuwataarifu ndugu zake.

“Tangu Jumamosi ya Oktoba 21, 2017 mpaka Februari 22, 2022 ndipo nilipowaona ndugu zangu baadhi waliofika mahakamani,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi, shemeji wa mmoja wa washtakiwa hao, mkazi wa Majengo mkoani hapa, Said Hassan Bwatamu alisema kuwa familia zimefurahi sana na zinaishukuru Serikali kwa kuwaachia ndugu zao.

“Tunashukuru sana Serikali hasa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kwa kuwaachia ndugu zetu.Hatuna la zaidi ya furaha,” alisema ndugu huyo.

Khalid Salum Nkrumah, mkazi wa Magomeni, ndugu wa karibu wa mmoja wa washtakiwa hao alisema kukamatwa kwa ndugu zao, kulileta masikitiko na majonzi makubwa lakini wamefurahi sasa kuwaona wakiwa huru.

Alisema baishara na shughuli walizokuwa wakifanya washitakiwa hao zimekufa na kuwarudisha nyuma kimaisha.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Kakoso, Tiba Moshi alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msukumo kwa mamlaka zenye kusimamia haki.

Rais Samia amewahi kuelekeza vyombo vya utoaji haki kuharakisha upelelezi wa kesi ambazo zina muda mrefu ili zisikilizwe au washtakiwa, ambao ushahidi umekosekana waachiwe huru ili wafaidi uhuru wao.

Tiba alisema kauli hiyo ya Rais Samia imethibitika kwa ndugu yao Ramadhani Kakoso pamoja na wenziwe kuachiwa huru.

Washtakiwa hao walikamatwa mwaka 2017 katika maeneo tofauti ya mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara kisha kushitakiwa kwa makosa ya ugaidi.

Walidaiwa kujiunga na kikundi kisichosajiliwa cha Hizbu Tahir kinachodaiwa kushawishi watu kujiunga na kuanzisha dola ya Kiislamu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.