Wasiojulikana waiba ng'ombe 14 shuleni Mbozi

Muktasari:

  • Ng'ombe hizo 14 zimeibwa zikiwa kwenye zizi usiku wa kuamkia leo Junatano Julai 19, 2023.

Songwe. Taharuki imeibuka baada ya ng'ombe 14 wa Shule ya Sekondari Hollywood, nje kidogo ya Mji Mdogo wa Mlowo wilayani Mbozi mkoani Songwe, kupotea usiku, katika mazingira yanayodhaniwa ni ya wizi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Julai 19, 2023; Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya, amesema kuwa taarifa hizo amezipata.

"Taarifa hizo nimezipata lakini ng'ombe zilikuwa chini ya mlinzi ambaye hajapatikana. Nimemuagiza OCD kuangalia taarifa ajira ya mlinzi aliyekuwepo, ili kama alikuwa na wadhamini wasaidie kumpata mlinzi huyo,” amesema Kamanda Mallya.

Kwa upande wake Debora Kameka, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shule hiyo, amesema wanaodhanikuwa kuwa ndiyo wezi wa mifugo hiyo, walivunja geti la nyuma na kuondoka na ng’ombe hao.

"Asubuhi wakati najiandaa kwenda kazini, nilipigiwa simu na kaka yangu akaniambia naomba uje haraka shuleni ng'ombe wote zizini wamechukuliwa. Nikafika hapa moja kwa moja nikapita hadi kwenye zizi nikakuta ngombe zimechukuliwa amebaki ng'ombe mmoja tu," ameeleza mkurugenzi huyo.

Amesema kuwa ng'ombe zilizoibwa zina thamani ya zaidi ya Sh6 milioni.

"Wameibwa ng’ombe wakubwa 12, lakini pia wadogo wawili ambao thamani yake kwa ujumla ni zaidi ya Sh6 milioni. Kwenye zizi amebaki ng'ombe moja, ambaye inawezekana aliwasumbua ndio maana wakamuacha," amesema mkurugenzi huyo.

Amesema kuwa shule hiyo inafuga ng'ombe kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi wakati wa sherehe zikiwemo za mahafali.

"Ng'ombe hao wanatusaidia kwenye sherehe. Tukiwa na mahafali tunachinja mmoja. Tulianza kufuga ng'ombe wawili mwaka 2007 kwa sasa walikuwa 15," ameeleza.

Akizungumzia hali ya ulinzi shuleni hapo, mkurugenzi huyo amesema shule ina walinzi wanne ambao wanafanya kazi kwa kupokezana ambapo ili kuboresha ulinzi geti moja la mbele ndilo linatumika huku la nyuma likiwa linafungwa muda wote.

"Tuna walinzi wanne ila mlinzi mmoja ambaye alikuwa lindo usiku huo hajaonekana hata kwenye simu hapatikani," amesema Debora na kuongeza

"Walinzi wengine pamoja na mchunga ng'ombe wanahojiwa na polisi ambao wamefika hapa ahuleni" ameeleza