Wasomi: Tozo mpya ya benki ni batili, ifutwe

Wasomi: Tozo mpya ya benki ni batili, ifutwe

Muktasari:

  • Wasomi wa masuala ya kodi, wamesema kuwa Sheria ya Tozo ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2022, haikufanyiwa tathmini ya athari zake kwenye uchumi kuanzia kwa watu wa chini, hivyo inakwenda kinyume na misingi inayokubalika duniani na haipaswi kutumika.

Dar es Salaam. Wasomi wa masuala ya kodi, wamesema kuwa Sheria ya Tozo ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2022, haikufanyiwa tathmini ya athari zake kwenye uchumi kuanzia kwa watu wa chini, hivyo inakwenda kinyume na misingi inayokubalika duniani na haipaswi kutumika.

Tozo hizo ambazo wanasema zinakata zaidi ya mara mbili kwenye chanzo kimoja, ni utaratibu usiotakiwa kwenye mchakato wa kuanzisha chanzo cha mapato ya Serikali.

Kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi, kilichopo kwenye tozo hizi, ni makato yanayofanywa katika kila hatua ya mtu kutaka kuitumia fedha yake, jambo ambalo halishauriwi kwenye kodi.

“Chukulia kwa mfanyakazi aliyelipwa mshahara wake benki. Akisema aiingize kwenye akaunti yake ya M-pesa au Tigopesa, atakatwa na atakapotaka kuitoa ili aitumie atakatwa tena. Hiki ni kipato kimoja ambacho kimekatwa (kodi ya mshahara) PAYE…huwezi kukata kodi tatu kwenye chanzo kimoja,” alisema Dk Balozi Morwa, mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CUCoM).

Naye mhadhiri mwandamizi wa masuala ya kodi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Deogratius Mahangila, alisema kilichopo kwenye tozo za miamala ya kielektroniki kimevuka kiwango kinachokubalika.

“Hii hata sio double taxation (kutoza kodi mara mbili) bali ni multiplicity of levies (utitiri wa tozo) uliowekwa baada ya Serikali kuona kuna miamala mingi inafanyika kidijitali. Ikiendelea, itapunguza hamasa ya kutumia huduma za fedha. Inatakiwa iangaliwe upya, napendekeza ipunguzwe,” alishauri Dk Mahangila.

Mhadhiri huyo alisema badala ya kiasi cha juu kuwa Sh4,000 kipunguzwe mpaka Sh500 kwani itawapa watu unafuu katika kipindi hiki kigumu ambacho mafuta yamepanda bei na bidhaa nyingine kama vyakula na hata nauli.

“Wote tunafahamu kuwa kodi ni muhimu kuiwezesha Serikali kutoa huduma za kijamii, lakini haitakiwi kumuumiza mwananchi. Kwa hali ilivyo sasa hivi, kila mtu anakuwa makini na kila shilingi anayoitumia. Tozo zisifutwe kabisa ila zipunguzwe mpaka kiasi kinachovumilika, Sh500 hivi sio mbaya,” alisema.


Tathmini ya madhara

Dk Morwa ambaye ni mshauri wa kimataifa wa masuala ya kodi, alisema kuna vitu viwili vinajidhihirisha kwenye tozo hiyo, ambayo Serikali haikuwa makini wakati inaipitisha.

“Research and development (utafiti na maendeleo) ni muhimu kwenye kila kitu ila hapa inaonekana haikuzingatiwa matokeo yake ndio haya malalamiko ya wananchi. Kingine walichosahau kufanya ni levy incidence analysis (tathmini ya waathirika wa tozo) ndio maana unaona mtu mmoja analipishwa zaidi ya mara moja kutokana na kipato kilekile,” alisema Dk Morwa.

Kwenye tozo hizi ambazo zinahusisha miamala inayofanywa kwenye akaunti za simu za mkononi au zile za benki, alisema zinawagusa watu wengi ambao walitakiwa kushirikishwa kujua namna gani wataathirika kabla ya kuipitisha na kuanza kutumika.

Aliwataja baadhi ya wadau muhimu kwenye mnyororo wa miamala ya kielektroniki kuwa ni benki zenyewe na kampuni za kadi za benki (mastercard au visacard), wamiliki wa minara ya simu, mawakala wa huduma za fedha zinazotolewa na kampuni za simu pamoja na wale wa benki na kampuni za simu zenyewe bila kuwasahau wateja ambao ndio wananchi.

“Ukifuatilia taarifa za mmoja wao, utagundua idadi ya miamala inayofanyika ndio inayompa kipato na faida ya biashara anayoifanya. Idadi ya miamala iliyokuwa inafanyika ilimpa kipato kila mdau muhimu hapo ndio maana biashara ilishamiri. Miamala ikipungua, athari zake zitawagusa wote hao,” alikumbusha Dk Morwa.


Ni tozo au kodi?

Licha ya kodi kukatwa zaidi ya mara mbili kwenye chanzo kimoja, Dk Morwa alisema bado haijaeleweka tofauti ya kati ya kodi na tozo na kinachoonekana ni kama Serikali inajificha kwenye neno tozo, ili isionekane inakiuka kanuni za kodi zinazokubalika duniani.

Kwa kawaida, alisema kodi hutozwa kitaifa lakini tozo huwa chini ya mamlaka fulani hasa halmashauri na huwekwa kwenye huduma mahsusi kama vile uzoaji taka au ulinzi ili kuziboresha.

“Halmashauri ikiweka tozo ya kuzoa taka, huwa inaeleweka ni gharama za kulipia magari pamoja na wafanyakazi wanaotoa huduma hiyo. Ikitokea huduma imesitishwa, tozo nayo haiendelei ila hapa kwenye miamala hapaeleweki tozo imekujaje,” alisema.

Kutokana na makato haya kutoeleweka vizuri, alisema ndio maana si Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wala wizara yoyote iliyojitokeza kuelimisha na kuhamasisha wananchi wailipe kama inavyofanywa kwenye maeneo mengine ili kutunisha mfuko wa Serikali.

“Hii tozo inawaumiza pia wafanyabiashara wanaopitisha mauzo yao benki na ambao hulipa kodi ya faida kutokana na huduma wanazotoa. Akiitoa fedha aiweke kwenye simu yake atakatwa, akisema amtumie mtu, atakatwa tena na huyo atakayepokea akiitoa atakatwa. Kwa muda mrefu tumekuwa tukihamasisha uchumi wa kidijiti, lakini juhudi hizo zinakwenda kukutana na vikwazo. Kuna makato mengi yanayopunguza hamasa ya kutumia huduma za fedha kidijitali,” alisema na kuongeza:

“Watu wataanza kulala na fedha ndani na ikitokea wamevamiwa na wezi watajichukulia sheria mkononi. Hii sheria ikiendelea kutekelezwa, uhalifu unaweza kurejea kwa kasi huko siku za mbele.”

Kutokana na malalamiko yaliyopo mtaani, mshauri huyo wa kodi alisema ni muhimu kwa Serikali kujitokeza na kuwaelimisha wananchi kuhusu tofauti kati ya tozo na kodi ili waelewe kwa nini makato haya yanafanywa kwenye fedha zao ambazo zimekatwa kodi nyingine muhimu kutokana na chanzo chake.

“Ni muhimu sana, TRA wasikae kimya. Huu ni wakati wao kujitokeza na kuufafanulia umma ili kujenga uzalendo wa watu kulipa kodi kwa hiari yao wenyewe,” alishauri Dk Morwa.

Kuhusu kuwaelimisha wananchi, Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema: “Kwa kuwa hizo tozo zimetolewa na wizara, naomba uwatafute wao wakupe ufafanuzi unaouhitaji.”

Wakati wananchi wakiumizwa na ukubwa hata wingi za kodi na tozo, bado wanaona usimamizi wa Serikali kwenye mapato ya umma ni kama haupo na huwa inaamua kuongeza au kupunguza viwango vya makato bila kuwashirikisha.

“Maswali magumu kuhusu kodi na tozo hayaulizwi kabla ya kupitishwa. Na wananchi nasi tunalalamika nje ya mifumo rasmi. Tukipata nafasi ya kuongea na viongozi tunaishia kusifia na kupongeza kwa ujenzi zahanati au barabara wakati hayo ni majukumu yao kusimamia matumizi ya fedha za umma na wakati mwingine utekelezaji wake umetuingiza hasara,” alisema Zena Abeid, mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Mbeya.

Kwa maana ya tozo hii ya miamala, Zena alisema hata makundi yasiyotakiwa kulipa kodi kisheria kwa sasa hayana ujanja.

“Chukulia mfano wa mwanafunzi anayepewa mkopo na bodi (Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu) kuanzia sasa atakatwa tozo ya Serikali hiyohiyo iliyomkopesha kabla hajaanza kuitumia. Kumbuka atakapomaliza chuo atatakiwa kuulipa ukiwa na riba yake. Yaani unakatwa kodi wakati mkopo uliopewa haujauzalisha ukapata faida yoyote sanasana wanakupunguzia kiasi unachoweza kutumia. Sasa hivi hata fedha za sadaka zitatozwa hii tozo, kumbuka wao huwa hawalipi kodi kama ilivyo kwa wanafunzi,” alisema Zena.


Kuchagua kodi za kulipa

Katika elimu ya kodi, wataalamu wanasema inashauriwa kwa mlipaji kuchagua aina ya kodi anazotaka kulipa kwa uhuru ili kulijenga Taifa lake kulingana na kipato alichonacho au ‘tax planning’ kama wanavyoiita wenyewe, inayotoa nafasi ya kufanya tax avoidance (kukwepa baadhi ya kodi kwa kufuata sheria).

“Mfano mzuri ni kwenye mshahara, kila kiwango kina kodi yake. Kama mwajiri wako akikuongezea mshahara utakaokuweka kwenye kundi kubwa la kodi, unaweza kuzungumza naye akupunguzie. Kwa wafanyabiashara kuna VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ambayo hulipwa na wenye mauzo yanayoanzia kiasi fulani, kama hutaki kuilipa huikuzi biashara yako tu,” alisema Elizabeth John, mwanasheria wa kujitegemea jijini Dodoma.

Badala ya kulalamika sana, Elizabeth alisema wananchi wanahitaji kuelimishwa namna ya kuchagua kodi za kulipa kwani sio lazima kuilipa kila iliyopo na akapendekeza namna ya kupunguza kiasi cha kulipa hata kwenye hii tozo ya miamala.

“Ukitoa kiasi chochote zaidi ya Sh400,000 makato yake ni Sh1,637. Kama unajua utahitaji Sh900,000 kwa wiki au mwezi, zitoe zote mara moja badala ya mara mbili au tatu. Kwa kufanya hivyo utakuwa umepunguza makato ya tozo. Hili linakubalika ukilitumia hata kwenye maeneo mengine ya mapato yako,” alishauri mwelimishaji huyo wa usimamizi wa fedha binafsi.

Kwa kutambua uwezekano wa kukwepa baadhi ya kodi na tozo zilizopo, Mwalimu Hezekia Njovu wa mkoani Iringa alisema waajiri nao wanapaswa kutoa elimu kuhusu njia za kuwalipa wafanyakazi wao mishahara yao pamoja na stahiki nyingine.

“Nitakwenda nizungumze na mhasibu. Naamini ni haki kukubaliana na mwajiri wangu jinsi atakavyonilipa mshahara wa kila mwezi. Sidhani kama nahitaji tena aniingizie kwenye akaunti. Nitapenda nilipwe fedha taslimu kukwepa hizi tozo. Nikilipa PAYE inatosha kuchangia ujenzi wa Taifa langu,” alisema Njovu.


Vyanzo mbadala vya mapato

Kwa kuzingatia rasilimali zilizopo nchini kuanzia madini, ardhi, bahari hata fursa za biashara za ndani na kimataifa, wananchi wanaamini Serikali inapaswa kubuni vyanzo vipya vya mapato tofauti na ilivyo sasa.

Dk Morwa alisema kodi ya majengo ni kati ya maeneo yanayoweza kuipa Serikali fedha nyingi, lakini juhudi kidogo sana zimewekwa huko licha ya fursa nyingi ilizonazo kutoa mapato mengi.

“Kuna danadana nyingi huku sababu wamiliki wa nyumba nyingi nzuri zinazopaswa kulipa kodi kubwa ni vigogo. Badala ya kuibua vyanzo vipya vya mapato wanawabebesha wananchi tozo ambazo ni mzigo kwao,” alisema.


Vita vya benki, kampuni za simu

Ilipoanzishwa tozo ya miamala ya simu Julai 15 mwaka jana, kampuni za simu ziliungana na wananchi kuilalamikia huku benki kadhaa zikiwataka wananchi kutumia huduma zao kwamba ni nafuu zisizo na makato mengi.

“Kwa jicho la kibiashara, benki zilifanikiwa kuzipiga zengwe kampuni za simu ndio maana nyingi zilitoa matangazo ya unafuu wa huduma zao. Walisahau kuwa zamu yao itafika. Sasa mambo yamegeuka na hapa benki zitaumia sana kwenye hizi tozo mpya,” alisema Alfred Jacob, wakala wa huduma za simu jijini Dar es Salaam.

Jacob alisema vita vya mafahari hawa ndivyo vinavyowaumiza wananchi wakati huu ambao fedha imekuwa bidhaa adimu sana.

“Benki na kampuni za simu zinashirikishwa kwenye upitishaji wa hizi sheria. Sasa Serikali inaonekana hupokea maoni ya kundi mojamoja na kila upande unajitahidi kujilinda ili kupeleka mzigo kwa mwenzake matokeo yake ni kilio mtaani,” alisema wakala huyo anayehofia biashara miamala kupungua nguvu.

Licha ya pande hizo mbili kuonekana zinachomeana utambi, Hellen Kavishe, mhamasishaji wa ujasiriamali alisema Serikali imefanikiwa kupandisha kiasi cha tozo inachokusanya.

“Mwaka jana, Serikali ilipunguza ukomo wa tozo kutoka Sh10,000 mpaka Sh7,000 na kwenye Bunge la bajeti mwaka huu ikasema inashusha kutoka Sh7,000 mpaka Sh4,000 lakini ukitizama kwa umakini haijapunguza ila imeongeza kutoka Sh7,000 mpaka Sh8,000,” alisema Hellen.

Alifafanua kuhusu ongezeko hilo kwamba, ukomo ulipokuwa Sh4,000 kwenye miamala ya simu, kutoa pesa kutoka akaunti ya benki kwenda akaunti ya simu hakukuwa na makato ambayo sasa hivi yamewekwa.

“Hata ukisema uende ATM (mashine ya kutolea fedha) ni yaleyale. Yaani Serikali imekaba maeneo yote. Lazima tulipe vinginevyo hela yako isionekane katika mfumo rasmi,” alisema.