Wasomi vyuo vikuu waungana kufungua kampuni ya kuchomelea
Muktasari:
- Wasomi wa vyuo vikuu waungana na kufungua kampuni ya uchomeleaji baada ya kupata mafunzo kwenye Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (Veta).
Dodoma. Wakati wahitimu wengi wa vyuo vikuu nchini wanalia kuhusu ukosefu wa ajira, mambo ni tofauti kwa vijana wawili wa kike ambao wamejiajiri kupitia fani ya uchomeleaji na kusahau suala la kuajiriwa.
Vijana hao Paulina Chuma na mwenzake Hilda Mwajombe ni wahitimu wa digrii ya elimu ya biashara na utawala kutoka vyuo vya CBE na St Augustino (SAUT) cha Mwanza ambao ili kujikwamua kiuchumi waliamua kusoma Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Tanzania (Veta) na kupata ujuzi wa kuchomelea.
Wakizungumza na gazeti hili kuhusu safari yao ya mafanikio vijana hao wamesema baada ya kumaliza elimu yao ya chuo kikuu walirudi mitaani na kusubiri kuajiriwa kama wanavyofanya wahitimu wengi wanaomaliza vyuo vikuu.
Paulina anasema baada ya kumaliza digrii yake kwenye masuala ya biashara na utawala kutoka CBE alitumia elimu aliyoipata kuanzisha biashara ndogo zilizokuwa zinamwingizia kipato ambacho hakikuwa kikubwa.
Anasema kwenye harakati za maisha alikutana na mwenzake Hilda ambaye naye alikuwa amemaliza masomo yake ya utawala na biashara Chuo Kikuu cha St. Agustine (SAUT) cha Mwanza ambapo kwa pamoja walijiunga na kuanza biashara ndogo ndogo.
Anasema wakati wanaendelea na biashara zao pembeni na ofisi yao kulikuwa na kijana aliyefahamika kwa jina la Rojas Mgunda aliyekuwa nafanya kazi ya kuchomelea vitu mbalimbali na hivyo waliamua kuingia naye maelewano ya kumtangazia biashara yake kwa njia ya mitandao ya kijamii.
Paulina anasema walikuwa wanatuma picha za vitu mbalimbali alivyokuwa anavitengeneza yule fundi na kama mtu anahitaji vitu hivyo basi wanaongea na fundi akishauza anawapa pesa kidogo ya udalali.
Anasema walifanya biashara hiyo kwa muda mrefu lakini walikuwa hawapati fedha nyingi kwa sababu wao walikuwa wanakula fedha ya udalali ambayo siyo nyingi japo iliwasaidia kuendesha maisha yao.
Anasema baada ya muda kupita walipata taarifa za mafunzo yanayotolewa na Veta ambayo yaliwavutia zaidi kwenda kusomea kozi ya uchomeleaji.
Anasema walishauriana na rafiki yake Hilda kwenda kusomea kozi ya uchomeleaji ambayo ilikuwa ni moja ya mafunzo yanayotolewa bure na Veta.
Anasema walisoma kozi hiyo kwa muda wa miezi minne na walipohitimu kozi hiyo walikwenda kujiunga na Rojas ambapo walianzisha kampuni inayoitwa PAHIRO Interprices ambayo inafanyakazi mpaka leo.
Hilda anasema sasa hivi maisha yao siyo kama yalivyokuwa huko nyuma kwani sasa hivi wana uhakika wakiamka asubuhi wanakwenda kazini na siyo kukaa tu nyumbani.
Anasema wateja wao wanawaamini kwani wakikuta mafundi ni wanawake wanajua kazi yao itakuwa nzuri na wataipata kwa wakati hali inayowapa wateja wengi.
Anasema pamoja na kusoma mpaka chuo kikuu lakini mafunzo aliyoyapata Veta ndiyo yaliyomfanya ajiajiri na kuajiri watu wengine wanne ambao huwa wanawasaidia kazi kama wanapata kazi kubwa.
“Lakini kwenye kazi ndogondogo huwa tunafanya wenyewe kwa sababu pesa yake huwa ni kidogo tofauti na kazi kubwa ambayo mteja huwa anaihitaji kwa haraka hivyo tumeajiri vijana wengine wanne ambao huwa wanatusaidia kazi,” anasema Hilda.
Anasema chuo cha ufundi stadi Veta ndiyo mkombozi kwa vijana na wanawake nchini kwani mafunzo yake yanamwandaa mtu kujiajiri mwenyewe au kuajiriwa kwani mafunzo yanayotolewa na chuo hicho ni ujuzi tosha.
Anasema kama hapo awali angeambiwa achague kwenda Veta kujifunza ufundi stadi asingekubali kwani fikra zake zilikuwa zinamwambia kuwa akimaliza tu chuo kikuu angepata ajira serikalini lakini kwa sasa kipaumbele chake ni mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Veta.
Kwa sasa vijana hao wameungana na kuanzisha kampuni yao ya uchomeleaji inayojulikana kwa jina la PAHIRO Interprices ambayo ipo eneo la Kisasa Sheli Jijini Dodoma wanatengeneza vitu mbalimbali kwa njia ya uchomeleaji.
Paulina anasema wateja wao wakubwa ni wanachi wa kawaida ambao hufika ofisini kwao kwa ajili ya kutengenezewa samani mbalimbali za majumbani kwao.
Aidha anasema kuna baadhi ya taasisi kama mashule na za watu binafsi pia huwa wanafika kupata huduma zao ambazo wanazitoa kwa viwango vya juu.
Vijana hao wanasema kupitia Veta wamejifunza kwa vitendo kuchomelea vitu mbalimbali ambavpo wanatumia ujuzi huo kujiingizia kipato kwa sasa.
Anasema hivi sasa wana uwezo wa kuetengeneza majiko mbalimbali ya kutumika kwenye mashule na taasisi mbalimbali, kutengeneza masufuria makubwa ambayo yanatumika kupikia chakula cha watu wengi, wanatengeneza majiko banifu ambayo yanatumia mkaa kidogo na samani za ndani.
Wito kwa wasomi na wanawake
Vijana hao wanatoa wito kwa vijana na wanawake ambao hawana shughuli zozote za kufanya mitaani kujiunga na chuo cha Veta kwa ajili ya kupata ujuzi.
Anasema pamoja kusoma mpaka kupata digrii ya masuala ya biashara lakini elimu hiyo haijawasaidia kuajiriwa wala kujiajiri hivyo wamewashauri vijana kujiunga na Veta kwa sababu ndiyo mkombozi kupitia mafunzo ya ufundi.
Paulina anasema huu siyo wakati wa kukaa nyumbani kwa kukosa cha kufanya wakati Veta inatoa mafunzo bure ya kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa
Changamoto
Vijana hao wanasema hivi sasa wanakabiliana na changamoto ya mtaji kwani wameanza kazi zao kwa kutumia pesa kidogo walikuwa wanazipata kwenye biashara zao za awali.
Wanasema mtaji huo ni kidogo hautoshelezi mahitaji kwani kuna wakati wanapata kazi kubwa lakini wanashindwa kuifanya kutokana na kukosa mtaji.
Wamewaomba watu wenye uwezo wa kuwasaidia hasa taasisi za kifedha ikiwemo mabenki kuwawezesha mitaji ili wafanye kazi kubwa na zenye ubora kwa ajili ya uchumi wa Taifa.
Veta
Mkuu wa Chuo cha Veta nchini, Anthony Kasore anasema vijana hao wamepata mafunzo kupitia programu ya kukuza ajira na ujuzi kwa maendeleo Afrika (E4D) ambapo vijana 4,000 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo.
Anasema program hiyo inatoa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa ufundi stadi kwenye fani za uchomeleaji wa majumbani na viwandani pamoja na ufunzi bomba wa majumbani na viwandani.
Anasema ufundi huo utawasaidia vijana waliomaliza kozi hizo kupata ajira kwenye miradi mbalimbali inayoendelea hapa nchini ikiwamo ya ujenzi wa bomba ya mafuta, ujenzi wa reli ya mwendo kazi (SGR) na ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP).
Anasema mafunzo hayo yanatolewa kwenye vyuo vya Veta vilivyoko mikoa minne ya Manyara, Dodoma Lindi na Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Veta Dodoma, Stanslaus Ntibara alisema programu hiyo imewanufaisha vijana 2,200 mkoani hapa na idadi hiyo inaweza kuongezeka.
Anasema wengi wa vijana waliohitimu katika kozi hizo wameajiriwa kwenye makampuni mbalimbali waliyokwenda kufanya mazoezi kwa vitendo na wengine wamejiajiri.