Wataja afya ya udongo kuongeza uzalishaji chakula
Rais Samia Suluhu Hassan, akikabidhi cheti kwa mshindi wa GoGettaz, Hasina Andriatsitohaina wa Madagascar, baada ya mdahalo wa vijana na kilimo jijini Dar es Salaam. Wengine ni Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Yara International, Svein Tore Holsether na kulia ni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Muktasari:
- Baadhi ya wanajopo katika Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) wamependekeza njia za kulifanya Bara la Afrika kuwa mzalishaji wa chakula mkubwa duniani, kuwa ni pamoja na kujali afya ya udongo katika kilimo.
Dar es Salaam. Baadhi ya wadau wa kilimo wa kimataifa wameshauri Bara la Afrika kujali afya ya udongo ili kukuza uzalishaji wa mazao na kuhakikisha usalama wa chakula.
Wakizungumza leo Septemba 7 katika mjadala wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula la afrika (AGRF) jijini hapa, baadhi ya wanajopo walipendekeza njia za kulifanya Bara la Afrika kuwa mzalishaji wa chakula mkubwa duniani wakipendeekeza ushirikishwaji wa wanawake, vijana na ukuzaji wa tekenolojia.
Akizungumzia suala hilo, Rais na Mtendaji Mkuu wa Yara International, Svein Tore Holsether amesema Bara la Afrika linapaswa kujenga mfumo endelevu wa chakula kwa kuhakikisha afya ya udongo.
“Mimea ni kama binadamu, inahitaji afya hivyo unatakiwa kupata virutubisho. Udongo unatakiwa kulindwa ili ukabiliane na joto, mafuriko na ukame hivyo unatakiwa uandaliwe. Kuna uhusiano kati ya afya na mafanikio,” alisema.
Amesema usalama wa chakula siyo lishe pekee, bali pia ni Afrika kuwa huru na chakul chake a kukifanya kilimo cha kibiashara.
“Afrika inaweza kulisha dunia yote,” amesema.
Kwa upande wake Melinda Bohanan kutoka Idara ya Haki za Binadamu na Maendeleo katika Wizara ya Mabo ya Nje ya Uingereza, amesema Kwa miaka mitatu iliyopita, Bara la Afrika limekabiliwa na majanga yakiwemo ya ujio wa nzige kati ya mwaka 2019, Uviko 19 na vita vya Ukraine na Russia.
“Pamoja na migogoro ya na mabadiliko ya tabia nchi yaliyokuba dunia nzima bei za vyakula na mbolea zimekwenda juu,” amesema.
Huku akirejea kauli mbiu ya AGRF, amesema Afrika inapaswa kuwekeza katika kilimo, kuhakikisha upatikanaji wa mbolea na kualika sekta binafsi kuwekeza.
Kuhusu kutekeleza alisisitiza nchi za Afrika kuwa na umoja wa malengo, uboreshaji wa miundombinu, utafiti na matumizi ya takwimu.
“Ili kuleta mabadiliko katika kilimo cha Afrika, wadau wote wanatakiwa kufanya kazi kwa pamoja, vijana, wanawake Serikali, wafanyabiashara,” amesema.
Naye Rodger Voorhies kutoka Bill and Melinda Gates Foundation na Mjumbe wa Bodi ya AGRA amesema suala siyo tu kurejesha kilimo kama kauli mbiu inavyoeeza, bali pia kilimo kinatakiwa kikue.
“Tunataka kilimo kikue na ukuaji huo uendane na hali ya sasa ya mabadiliko ya tabia nchi. Tunatakiwa kuja na mfumo mpya wa chakula edelevu kupitia wakulima wadogo.
“Katika maisha yangu yote, nimewahi kusikia idadi kubwa ya watu masikini duniani, kwanza ilikuwa China na Asia Kusini, lakini nasimama hapa leo nikiweka lengo kwa Melinda Gate Foundation kwamba umasikini utaanza kuondoka Kusini mwa Afrika,” amesema.
Katika hilo alisisitiza ushirikishwaji wa wanawake na matuizi ya tenolojia za kilimo ikiwa pamoja na matumizi ya mbegu bora.