Watano wafariki dunia, 12 majeruhi mafuriko Hanang
Muktasari:
- Mafuriko mabaya yametokea Hanang, Mkoa wa Manyara, Tanzania, yakisababisha vifo vya watu watano na majeruhi 12, huku wengine wakiwa hawajulikani walipo. Mkuu wa Mkoa, Queen Sendiga, amethibitisha hali hiyo na kutoa wito wa msaada.
Hanang. Watu watano wamefariki dunia na 12 wamejeruhiwa huku baadhi wakiwa hawajulikani walipo wilayani Hanang' mkoani Manyara, baada ya mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia leo Jumapili Desemba 3, 2023 kusababisha mafuriko.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amethibitishia Mwananchi Digital kutokea kwa vifo na adha hiyo na kuwa tayari timu ya uokozi imekwishafika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada.
Sendiga amesema hadi sasa (saa 4 asubuhi) vifo vya watu watano vimethibitishwa, watu 12 wamejeruhiwa, baadhi ya nyumba zimezingirwa na maji na baadhi ya watu hawajulikani walipo.
"Asubuhi hii nilikuwa kwenye ziara wilayani Kiteto ila nimeikatisha na naelekea kwenye tukio wilayani Hanang na Mganga Mkuu wa Mkoa Dk Damas Kayera yupo eneo la tukio kwa ajili ya kutoa huduma," amesema Sendiga.
Amesema timu za uokoaji zikiongozwa na Jeshi la Zimamoto na uokoaji zimeshafika eneo la Mji Mdogo wa Katesh wilayani humo kwa ajili ya uokoaji na majeruhi wapo Hospitali ya Wilaya ya Hanang ya Tumaini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Rose Kamili amesema athari zilizozopo eneo la Gendabi, zinafanana na za volcano iliyotokea miaka iliyopita.
"Maporomoko ni makubwa, mawe, miamba, miti mikubwa na tope yamezoa nyumba nyingi, tumeshindwa kufika kwani hali si shwari, hapaendeki," amesema Kamili.
“Pia hata maeneo ya Katesh, Gedan’gonyi nyumba nyingine zimefukiwa na tope, miti na mawe,” amesema Kamili.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja amesema uokozi unaendelea na ameitaka jamii uendelee kuchukua tahadhari na kuwasaidia waliopatwa na matatizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, George Katabazi amesema yupo njiani kuelekea eneo la tukio.
Mkazi wa eneo la Jorodom wilayani Hanang, Hamis Juma amesema katika eneo lake kuna msiba tayari uliosababishwa na mafuriko kwani mama mmoja amefariki dunia baada ya nyumba kusombwa na maji na watoto wake hawaonekani.
“Watu wamefariki na wengine wamepanda juu ya mapaa ya nyumba na mabasi yanayopita njia ya Arusha kwenda Singida yameshindwa kuendelea na safari,” amesema Hamis.
Mmoja kati ya wasafiri kwenye barabara ya Arusha- Singida, Amina Ally amesema wamesitisha safari kwa muda, kutokana na athari za mvua hiyo ya jana.