Watanzania watakiwa kudumisha upendo, amani

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Askofu Lazarus Msimbe (katikati) akiteta jambo na Askofu mstaafu wa kanisa hilo, Telesphor Mkude (kulia) wakati wa tamasha la dini hiyo iliyokutanisha waumini kutoka tarafa za kikanisa nane (Dekania) mjini Morogoro, kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa idara ya Litrujia Baraza la Maskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Ifakara, Salutaris Libena. Picha na Juma Mtanda.

Muktasari:

Tamasha la dini kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro limehusisha waumini wa dini hiyo kutoka dekania nane zinazounda jimbo hilo.

Morogoro. Watanzania wametakiwa kuendelea kudumisha upendo, amani na mshikamano ili kuepuka kutokea kwa viashiria vya uvunjifu wa amani na vurugu nchini.

 Akizungumza katika tamasha la dini ya kikristo mkoani Morogoro, Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Mhashamu Telesphory Mkude amesema machafuko yanayotokea nje ya Tanzania yanaweza kutokea nchini hivyo wananchi na viongozi wana wajibu wa kuendelea kutunza, kudumisha matendo ya upendo, umoja na mshikamano kwani hiyo ndio moja ya silaha ya utulivu.

Askafu Mkude amesema nchi iliyokosa utulivu, umoja, mshikamano haiwezi kuwa na amani kwa sababu viongozi, wananchi wameshindwa kuwa wamoja jambo ambalo ni rahisi kutokea machafu.

“Penye upendo, pana amani, penye amani pana mshikamano hivyo Watanzania kiujumla wao tunahitaji kuendelea kupendana bila kuja dini, kabila na rangi za ngozi zetu sisi sote wa baba mmoja na tunahitaji amani zaidi kwani kinachotokea nje ya Tanzania kinaweza kutokea hapa nyumbani.”amesema Askofu huyo.


Makamu Mwenyekiti wa idara ya Litrujia Baraza la Maskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Ifakara, Salutaris Libena amesema jamii hasa waumini wa dini ya kikristo wamekuwa hawatekelezi vizuri ibada na kufuata matendo ya kimaadili.

“Tunakumbushana baadhi ya waumini hawatekelezi vizuri tendo la kupiga goti kwa sababu ya mavazi waliyovaa kuwabana awe mwanamke au mwanamke kwani hatuonyeshi unyenyevu wetu mbele ya bwana na hapo tunakatisha masharti ya ibada.”amesema Askofu Libena.

Katika tamasha hilo limewakutanisha waumini na kwaya za tarafa nane za kikanisa (Dekania) kwa kutumbuiza kwa kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu.

Muumini wa dini hiyo kutoka Bagamoyo, Lucia Mshambu (18) amesema baadhi ya waumini wanapoenda kanisani wamekuwa haonyeshi kama wamejindaa kwa ajili ya ibada.

“Muumini aliyejiandaa kwenda kanisani atakuwa amejindaa kiroho, kiimani na mavazi yanayoendana na eneo takatifu la kanisa kwa ajili ya kuabudu ili kupata utakatifu kutoka baba yetu aliye mbinguni lakini uvaaji wa nguo za kubana au fupi maana yake ukivaa utashindwa kutekeleza tendo la unyenyekevu la kupiga goti.”amesema Lucia.