Watatu wafariki, 15 wajeruhiwa vurugu za mgogoro wa ardhi Kibaha
Muktasari:
- Mapigano hayo mbali na kusababisha baadhi ya kaya kukosa makazi, yamesababisha pia vifo na majeruhi
Kibaha. Ni hali ya taharuki, simanzi na sintofahamu kwa wakazi wa Lupaso, Kata ya Vikawe, wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani baada ya kuibuka mapigano kati ya wakazi na watu waliotajwa kuwa mabaunsa, alfajiri ya kuamkia leo Mei 6, 2026.
Mapigano hayo mbali na kusababisha baadhi ya kaya kukosa makazi, yamesababisha pia vifo vitatu na majeruhi 15 wote wakiwa ni wanaume.
Mwananchi iliyofika eneo la tukio saa chache baada ya vurugu hizo imeshuhudia askari wa kutuliza ghasia wenye silaha za moto na wengine wakiwa na mabomu ya machozi wakiimarisha ulinzi.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Vurugu hizo zinatajwa kusababishwa na mgogoro wa ardhi kwenye eneo la Lupaso, ambalo wananchi waliuziwa kati ya mwaka 2008 hadi 2019 na waliodai ni ya kwao, kabla ya kujitokeza mmiliki halali hivi karibuni.
Hata hivyo, wananchi hao walidai maridhiano kati yao na mmiliki, yalifanyika kwenye uwanja wa Vikawe, Kibaha Aprili mosi, 2026 na kufikia muafaka kwamba eneo hilo lipimwe na waliouziwa awali na kujenga wamlipe mmiliki halali wa eneo, ikiafikiwa kila mita ya mraba iuzwe Sh3,000.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Wananchi wanadai mkutano huo wa maridhiano uliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Niki wa Pili na mmiliki ambaye wanadai hakuwa hakifahamu ukubwa wa eneo lake baada ya kupimwa, aligoma kulipwa na kutaka wananchi waliokuwa wamejenga makazi kuondoka.
Hata hivyo, mkuu wa wilaya ambaye wananchi wanaeleza alikuwepo eneo la tukio leo baada ya vurugu, alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia hilo, aliomba apigiwe baadaye yupo kwenye kikao na alipopigiwa simu yake haikupokewa.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alipoulizwa, alikiri kutokea kwa vurugu katika eneo hilo ambalo chanzo chake ni mgogoro wa ardhi.
"Vyombo vya ulinzi vinaendelea kufanyia uchunguzi tukio hilo," amesema Kunenge kwa kifupi wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani alipopigiwa simu kuzungumzia hilo alitaka apigiwe baadaye na kusema yupo kwenye kikao, alipotafutwa tena simu yake haikupokewa.
Mwananchi ilifika Hospitali ya Mkoa ya Tumbi na kushuhudia majeruhi wa tukio hilo wakiendelea kupatiwa matibabu.
Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura hospitalinj hapo, Sialely Moshi amesema wamepokea maiti tatu na majeruhi 15 wa tukio hilo wote wakiwa ni wanaume. Amesema kati ya majeruhi 15 waliopokewa watano wanaendelea vizuri.
Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Hali ilivyokuwa
Mwananchi ilishuhudia baadhi ya kaya zikiwa zimejaa taharuki, hazina makazi na watoto wakishindwa kwenda shule, huku vyombo vikiwa vimetapakaa nje na nyumba nyingi kubomolewa.
Michirizi ya damu ilionekana katika baadhi ya maeneo kutokana na mapigano hayo ambayo wananchi wanaeleza yalihusisha silaha kama nyundo, visu na mapanga baina yao na watu waliojiita mabaunsa waliodai kupewa mamlaka ya kuvunja nyumba hizo na mtu waliyemtaja ndiye mwenye eneo hilo.
Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
"Nilisikia kelele nje, wakati nachungulia dirishani kujua nini, nikasikia mlango wangu umepigwa teke na kundi la watu kama saba kuingia ndani," amesema Saumu Kijangwa.
Amesema kundi hilo lilimtolea kisu na kumwambia atoke nje, wanabomoa nyumba asije kufia ndani.
"Niliwatoa wanangu watatu na kuwaficha kichakani jirani na kwangu, wakati huo wale watu wanapekua ndani na wengine wakivunja nyumba, lilikuwa ni kundi kubwa la watu kama 300.
"Walijigawa kwa makundi wengine wakivamia huku na wengine kule, wamechukua vile walivyoona vinastahili ikiwamo akiba yangu niliyokuwa naichimbia chini ndani mwangu, nikidunduliza ili mchakato wa kumlipa mmiliki halali wa eneo ukianza nilipe," amesema.
Akizungumzia chanzo cha mgogoro huo wa ardhi, amesema aliuziwa hapo mwaka 2017 na kujenga na kuhamia, lakini mwaka huu ndipo wakasikia eneo lina mmiliki halali.
Amedai wananchi baada ya sekeseke hilo, hawakubisha walikubali wamedhulumiwa, hivyo kwa kuwa walikuwa wengi na tayari wamejenga walikwenda kwenye maridhiano na mmiliki halali, maridhiano yaliyoongozwa na mkuu wa wilaya na kukubaliana eneo lipimwe na kila mita ya mraba, mmiliki apewe Sh3,000.
Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
"Tuliambiwa malipo yakianza tumlipe asilimia 30, hivyo tulikuwa tumeanza kujichanga na kukubali kwamba waliotuuzia mwanzo walituibia, lakini ghafla huyu mmiliki akasema hataki maridhiano, tuhame tukiwa hatujui nini kinaendelea ndipo usiku tukavamiwa na kuanza kubomolewa nyumba," amesema.
Mkazi mwingine, Upendo Mlale amesema mida ya saa 10 alfajiri, walivamiwa na kundi la watu wakiwa wamevaa kombati, wakiwa na visu na mapanga na kuanza kuwapiga na kuwatoa nje ya nyumba zao.
"Tumeshangazwa na tukio hili kwa kuwa tayari tulishafanya maridhiano, lakini ghafla tu tumevamiwa na kuanza kupigwa na wizi wa mali zetu kutokea, mbali na kubomoa nyumba zetu wameiba vitu na pesa ambazo tulishaanza kuhifadhi ili control number zikitoka tuanze kumlipa mwenye eneo baada ya kupimiwa," amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Shaban Ally Shaban ameiambia Mwananchi kwamba majira ya saa 10 alfajiri alipigiwa simu na kuambiwa kuna watu wasiojulikana wamevamia eneo hilo wanavunja nyumba.
Amesema alimpigia simu mkuu wa upelelezi na polisi kata, sanjari na polisi jamii ili kwenda kutoa msaada.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Amesema wakati wanafika eneo la tukio walikutana na watu kama 300 waliokuwa na Toyota Coaster sita na mapanga na nyundo.
"Wakati huo wananchi pia walikuwa wanapiga filimbi kuitana ikawa ni vurugu kubwa, wananchi wamejeruhiwa kwa mapanga na nyumba zao kuvunjwa," amesema.
Amesema katika tukio hilo, hakuna mwananchi aliyepoteza maisha isipokuwa wale mabaunsa na majeruhu.
Akizungumzia mgogoro wa ardhi, amesema anachokifahamu eneo hilo wananchi na mmiliki halali walishafanya maridhiano na walishaleta wapima wakapima ili wananchi waliouziwa kwa kutapeliwa awali na kujenga wamlipe mmiliki halali.
"Kila kitu kilikwenda vizuri na huyo mmiliki alikubali kulipwa mbele ya mkuu wa wilaya, lakini Mei 2, 2026 alikwenda kwa mkuu wa wilaya na kusema ametengua maridhiano," amesema.
Amesema mkuu wa wilaya aliwaita na alichokiamua ni kumtaka mwenye eneo (jina linahifadhiwa) kwenda mahakamani, lakini siku tatu baadaye kabla ya kwenda mahakamani ndipo kundi hilo la watu limevamia na kuvunja nyumba na kusababisha vurugu hizo.