Watatu wafariki dunia magari yakigongana na kuwaka moto
Moja ya lori lililopata ajali baada ya kugongana uso kwa uso na kuwaka moto eneo la Ipagala jijini Dodoma.
Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea saa 12 asubuhi ikihusisha gari aina ya Howo lililokuwa na mzigo wa saruji na jingine kama hilo lililokuwa limebeba mchanga.
Dodoma. Watu watatu wamekufa papo hapo baada ya magari ya mizigo kugongana uso kwa uso na kuwaka moto eneo la Ipagala jijini Dodoma.
Ajali hiyo imetokea saa 12 asubuhi ikihusisha magari ymawili aina ya Howo ambapo mojawapo lililokuwa na mzigo wa saruji na jingine lilikuwa na mchanga.
Gari hilo la saruji lilikuwa linatokea Dar es Salaam na kuelekea Shinyanga, ambapo inaelezwa kuwa lilikuwa na dereva peke yake, na gari la mchanga lilikuwa likitokea eneo la Nala jijini Dodoma likielekea Nane Nane ndani ya Jiji la Dodoma.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera amesema chanzo cha ajali hiyo inadaiwa ni uzembe wa dereva wa gari lililokuwa na saruji, ambaye inaelezwa huenda alisinzia na kuacha njia.
“Ajali hii imetokea leo saa 12 asubuhi. Chanzo cha awali kinaonyesha dereva wa gari lililokuwa limebeba mzigo wa saruji aliacha njia na kwenda upande mwingine na huenda alikuwa amesinzia,” amesema Kamanda Hyera.
Moja ya lori lililopata ajali baada ya kugongana uso kwa uso na kuwaka moto eneo la Ipagala jijini Dodoma.
Amewataja waliopoteza maisha kuwa wametambulika kwa jina moja kila mmoja, ambao ni Lukas (dereva wa gari la mchanga) na wasaidizi wake Elisha na Kevin, ambao walibanwa huku gari lao likiendelea kuwaka moto.
Kamanda amesema ni wakati kwa madereva wa magari yanayokwenda masafa marefu kupata muda wa kupumzika, kwani wakiendesha kwa muda mrefu mara nyingi wanapata usingizi au mwili unachoka na hivyo akili haziwi kwenye usukani.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabil Shekimweri amesema kuwa dalili za ajali hiyo moja kwa moja zinaonyesha kuwa madereva hao walikuwa kwenye mwendo wa kasi wakati katika eneo hilo kuna taa za kuongoza magari.
“Eneo hili kama mnavyoliona, zipo taa za kuongoza magari. Kwa akili ya kawaida, hata kama kungekuwa na ajali, isingekuwa kwa ukubwa huu maana kila mtu alipaswa kuchukua tahadhari, ikiwemo mwendo mdogo. Sasa inashangaza hali hii ilivyotokea,” amesema Shekimweri.
Mmoja wa mashuhuda katika ajali hiyo, Patrick Daniel, mkazi wa Mtaa wa Meriwa amesema kwa namna yoyote huenda dereva wa roli la mchanga ndiye chanzo kwani alikuwa kwenye mwendo wa kasi lakini alikuwa anapiga sana honi.
“Yule jamaa sijui kama alitaka kuziwahi taa au labda gari ilikuwa na shida, maana alitoka upande wa mjini akipiga honi kwa nguvu tena kwa haraka, halafu ni eneo la taa. Hivi huyu mwingine angefanyaje?” amesema Daniel.
Kwa upande wake, Thomas Yaile amesema wakati ajali inatokea aliishuhudia na kwamba gari la mchanga lilikuwa kwenye mwendo kasi lakini lilikuwa likipiga kelele, ndipo kikasikika kishindo kisha akaona moto unawaka.
Yaile anasema alifika mapema eneo la tukio na kwamba waliona mtu mmoja akitoka kwenye roli lililobeba saruji na kukimbia, lakini moto ulitanda zaidi upande wa gari lingine na hakuna aliyetoka hadi zimamoto walipofika na kufanikiwa kuuzima moto huo ndipo wakatolewa wanaume watatu waliokuwa wameungua na haikuwezekana kuwatambua.