Watoto 157 wazaliwa mkesha wa Pasaka
Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Tanga, Shabani Sonyo akimkabidhi Mariamu Athumani mtoto wake ambaye alijifungua usiku wa mkesha wa Pasaka. Watoto 10 walizaliwa hospitalini hapo. Picha na Rajabu Athumani
Muktasari:
Kati ya watoto hao, 92 walizaliwa Dar es Salaam, 34 mikoa ya Manyara na Arusha, 17 Hospitali ya Rufaa ya Geita, 10 hospitali ya Handeni, Tanga na wanne Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi.
Dar/Mikoani. Watoto 157 wakiwamo watatu waliozaliwa kwa pamoja, wamezaliwa katika Hospitali mbalimbali nchini kwenye mkesha wa Sikukuu ya Pasaka.
Kati ya watoto hao, 92 walizaliwa Dar es Salaam, 34 mikoa ya Manyara na Arusha, 17 Hospitali ya Rufaa ya Geita, 10 hospitali ya Handeni, Tanga na wanne Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi.
Mganga Mfawidhi wa Mkoa wa Manyara, Dk Catherine Magali alisema watoto saba walizaliwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa huo huku na mama mmoja alijifungua watoto watatu kati yao, wawili wa kike na wote wakiwa ni wenye afya njema.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali Mkoa ya Mount Meru, Jacline Urio alisema watoto saba walizaliwa kati yao wasichana wawili na wavulana watano.
Kati ya watoto 92 waliozaliwa katika Hospitali za Muhimbili, Temeke, Mwananyamala na Amana, 52 ni wa kike na wa kiume ni 40. Muuguzi mwandamizi wa Muhimbili, Mariam Mlawa alisema, watoto saba walizaliwa kati yao wa kike wanne na wa kiume watatu.Alisema idadi ya watoto waliozaliwa Muhimbili ni ndogo kuliko hospitali nyingine kwa kuwa inapokea wagonjwa wanaohitaji tiba za kibingwa.
Katika hospitali ya Temeke, muuguzi kiongozi, Asha Kitumbuizi alisema watoto 43 walizaliwa, kike 23 na wa kiume 20. Huko Mwananyamala, ofisa muuguzi kiongozi, Loyce Kayanda alisema watoto 15 kati yao tisa wa kike na sita wa kiume walizaliwa na Amana, watoto 27 (wa kike 16 na kumina moja wa kiume walizaliwa.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Geita, mganga mkuu wa mkoa huo, Japhet Simeo alisema watoto 17 walizaliwa, wanane wa kike na tisa wa kiume na ofisa habari wa KCMC, Gabriel Chisseo alisema watoto wanne ,wawili wa kiume na wawili wa kike walizaliwa.
Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Shabani Sonyo alisema kuanzia saa sita na dakika moja mpaka asubuhi, watoto 10 walizaliwa.
Alisema kati ya watoto hao, wapo pacha ambao mmoja ni wa kiume na mwingine wa kike.
Akizungumzia watoto hao pacha Sonyo alisema, “Bado wapo katika uangalizi maalumu kutoka na hali zao kutotengemaa vizuri hivyo kushindwa kukabidhiwa kwa mama yao.”
Mmoja wa wazazi hao ambaye alijifungua mtoto wa kiume, Saumu Issa alisema anawashukuru wahudumu wa hospitali ya Wilaya Handeni kwani walimpokea vizuri hadi kujifungua.
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge (Dar), Joseph Lyimo (Manyara), Filbert Rweyemamu (Arusha), Rajabu Athumani (Handeni), Rehema Matowo (Geita) na Janeth Joseph (Moshi).