Watoto wanne washambuliwa na fisi wakiwa wamelala

Muktasari:

  • Waliojeruhiwa ni Jishanga Izengo (18), Kanizio Joseph, mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Mwalata, Lazaro Emmanuel anayesoma darasa la tano katika shule ya msingi Mwalata pamoja na Malambi Mayala.

Shinyanga. Vijana wanne wa familia moja katika kijiji cha Mwalata kilichopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamenusurika kuuawa na fisi aliyewavamia na kuwamejeruhi sehemu mbalimbali za miili yao wakati wakilinda mifugo nyumbani kwao.

Vijana hao waliokolewa na mama yao mzazi, Mbuke Jishanga ambaye hata hivyo alimshambulia fisi huyo hadi kumuua.

Hayo yamethibitishwa leo Januari 31, 2023 na mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Kishapu mkoni Shinyanga Mohamed Mkumbwa wakati akitoa taarifa kwa mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa na mjumbe wa baraza kuu la Umoja wa Wanawake Taifa (UWT), Hellen Bugohe.

Mjumbe huyo alikuwa akitoa zawadi kwa wagonjwa na wazazi waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo alipokuwa kwenye maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM.
Dk Mkumbwa amesema majeruhi hao walioshambuliwa na fisi waliwapokea majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia jana Jumatatu Januari 30, 2023 wakiwa na hali mbaya na baada ya kuwapa huduma sasa wanaendelea vizuri.

“Majira ya alfajiri saa 10 tuliwapokea majeruhi wanne wakiwa na hali mbaya, kuna aliyejeruhiwa kwa kung’atwa chini ya pua mwingine kichwani mwingine mapajani na mwingine sehemu ya kichwani kuelekea shingoni na sasa tunamshukuru Mungu wanaendelea vizuri,” amesema Dk Mkumbwa.

Amewataja waliojeruhiwa kuwa ni Jishanga Izengo (18), Kanizio Joseph, mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Mwalata, Lazaro Emmanuel anayesoma darasa la tano katika shule ya msingi Mwalata pamoja na Malambi Mayala.

Mama wa watoto hayo, Mbuke akisimulia tukio hilo lilivyotokea, amesema majira ya saa 7 usiku alimsikia kijana wake Jishanga akipiga kelele nae alitoka nje akakuta vijana hao wameshambuliwa na fisi, alirudi ndani na kuchukua panga na kuanza kupambana na huyo fisi huku akipiga kelele majirani zake wakaja kumsaidia.

“Nilisikia kelele watu wanalia nikiwa nimelala ule usiku nikawa nimetoka nilipotoka nikakutana na kijana wangu mkubwa, akaniambia kuna kitu kimetuuma hatujui ni kitu gani baada ya kumuona na mwingine anahangaika naye nikarudi ndani kuchukua panga na kuanza kumshambulia huyo fisi,” ameeleza Mbuke.

“Kwa kweli nisingetoka nje huyu fisi angeniulia kabisa watoto wangu, sisi kwetu huwa tuna desturi ya watoto wa kiume kulinda mifugo ikiwemo mbuzi na ng’ombe, hivyo wakati wamelala ndipo akaja fisi kuanza kuwashambulia,”

“Nikaona nichukue panga nianze kupambana nae, nikamkata eneo la kichwa akaenda kujibamiza ukutani mwa nyumba akapanga mipango ya kunirudia na mimi nikaweka panga vizuri akaja, nikamkata tena akalala na watu wakaja wakakuta tayari nimeshamkatakata,” amesema Mbuke.

Kwa upande wake, mjumbe wa UWT, Hellen Bugohe amesema wamefika hosipitalini hapo na kuwajulia hali vijana hao, kweli wamejeruhiwa vibaya lakini mwanamke jasiri Mbuke Jishanga aliwaokoa vijana hao baada ya kufika na kuanza kumshambulia huyo fisi.

“Nimpongeze sana huyu mama kwani ni mwanamke jasiri. Wanawake tunaweza, tukisema tunaweza kweli tunaweza, tunatakiwa tumpongeze sana mwanamke mwenzetu amefanya kazi kubwa sana na sasa ni wazima hospitali yetu inatoa huduma za haraka,” amesema