Watuhumiwa 40 panya road wafikishwa mahakamani

Muktasari:

  • Watuhumiwa 40 wa makosa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha na kuvunja nyumba usiku ‘panya road’ wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Dar es Salaam. Watuhumiwa 40 wa makosa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha na kuvunja nyumba usiku ‘panya road’ wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Mtuhumiwa Lubea Manzi maarufu Master pamoja na wenzake 39 wamefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi Oktoba 6, 2022 na kusomewa mashtaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuvunja nyumba usiku na kujeruhi watu maeneno mbalimbali ya Wilaya ya Ilala.

Mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali, Michael Momboko, amesema kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo Septemba 19-21, 2022 maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam ambapo walivunja nyumba usiku na walipora mali.

Amesema walijeruhi wananchi kwa kutumia silaha za jadi (mapanga, nondo, visu) na kukimbia.

Watuhumiwa hao kwa pamoja walikana mashtaka hayo na kurudishwa rumande kutokana na mashataka wanayowakabiliwa nayo kutokuwa na dhamana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 19, 2022.

Kesi hiyo inasikilizwa na Mahakimu watatu, Hakimu Mkazi Glory Nkwera, Fadhili Luvinga na Rehema Liana