Watumishi wanaokwamisha kuwahudumia wananchi kwa kisingizio 'mtandao uko chini' waonywa
Muktasari:
- Siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya watumishi kudai kushindwa kutoa huduma kwa maelezo kuwa mifumo ina changamoto hivyo kusababisha wananchi kukosa huduma husika kwa wakati.
Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewaonya watumishi wa serikali wanoshindwa kutoa huduma bora na stahiki kwa wananchi kwa kisingizio cha mfumo mbovu kuacha mara moja na badala yake mifumo ya hiyo ya kidijitali itumike kuboresha huduma hizo.
Akizungumza mjini Musoma leo Ijumaa Julai 25, 2025 wakati akikabidhi kompyuta kwa idara ya afya, Kanali Mtambi amesema siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya watumishi kushindwa kutoa huduma wakidai mifumo ina changamoto jambo ambalo siyo kweli.
"Kuna homa imeibuka huko, kila saa wanadai mfumo mbovu mara mfumo haufunguki hivyo wanaacha kutoa huduma bora na inayotakiwa kwa wananchi, nitoe onyo wale wenye huu ugonjwa wakae tayari kuanzia sasa tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu," amesema.
Amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwaajili ya kuboresha huduma za kijamii hivyo hatakuwa tayari kuona mtumishi yeyote anakwamisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi kwa visingizio ambavyo havina ukweli.
Kanali Mtambi amesema awali Mkoa wa Mara ulikuwa ukiongoza nchini kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika huduma mbambali za serikali lakini kwasasa mkoa huo umeshuka na kuwa wa nane kwa matumizi hayo kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo ya visingizio vya mifumo mibovu.
Kutokana na hali hiyo ameagiza taasisi zote za serikali kutumia mifumo hiyo kama ambavyo imeelekeza huku akiagiza kuwa ifikapo Agosti 31 mwaka huu vituo vyote vya kutolea huduma za afya viwe vimeunganishwa kwenye mifumo na kuanza kutoa huduma kupitia mifumo hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kushoto) akimkabidhi kompyuta Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini Dk Joseph Fwoma. Picha na Beldina Nyakeke
"Utoaji wa huduma bora za afya kwa kiwango kikubwa unategemea matumizi ya Tehama kwani kila kitu kinakuwa kimerahisishwa, hata kwenye suala zima la matibabu mfumo unawezesha pia kwenye suala la ukusanyaji wa mapato sambamba na udhibiti wa matumizi ya mapato hayo," amesema
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya amesema serikali imetoa jumla ya kompyuta 142 kwaajili ya zahanati mbalimbali zilizopo katika halmashauri tisa za Mkoa wa Mara.
Kusaya amesema lengo la kutoa kompyuta hizo ni kutaka kuboresha zaidi utoaji wa huduma za afya katika sekta ya afya mkoani Mara.
"Tunataka kuhama kutoka kwenye matumizi ya karatasi lakini pia sote tunafahamu mchango wa mifumo ya kidijitali katika kuboresha huduma hivyo kama ambavyo serikali imekuwa ikidhamiria kuboresha huduma kwa maslahi ya wananchi, hivi vitendea kazi vinalenga kuwa na huduma bora kwa wananchi," amesema.
Baadhi ya watumishi wamesema matumizi ya mifumo yanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwepo upungufu wa vifaa, elimu, pamoja na mtandao na nishati ya umeme hasa kwa maeneo ya vijijini.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini, Dk Joseph Fwoma amesema mifumo ya kidijitali ina manufaa mengi katika sekta ya afya hivyo kuomba serikali kuwekeza zaidi katika elimu kwa wasimamizi wa mifumo hiyo.
"Kuna haja ya kutoa elimu ya mara kwa mara kwasababu wengi waliopo kule hii mifumo imewakuta wakiwa kazini hivyo kuna haja ya kutenga bajeti ya kutisha ili kuwapa elimu wahusika na hii itaketa ufanisi kwenye utekelezaji wa jambo hili," amesema.
Amesema tathmini inaonyesha kuwa mifumo hiyo ikitumika vema upatikanaji wa huduma pia utaboreshwa zaidi sambamba na ongezeko la mapato na uwajibikaji kwa ujumla.