Wauguzi Dar wataka siku zaidi za mapumziko

Wakunga wakiwa kwenye matembezi ya hisani.

Muktasari:

Wauguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameieleza Serikali changamoto zinazowakabili na kutoa mapendekezo namna ya kuboresha, ili kuinua tasnia hiyo na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kuwahudumia Watanzania.

Dar es Salaam. Wauguzi na wakunga wa mkoa wa Dar es Salaam, wamelalamikia kufanya kazi zaidi ya saa nane kwa siku, pamoja na kutumia siku 28 mpaka 30 wakiwa kazini bila mapumziko.

Wauguzi hao wamesema licha ya kupata mapumziko ya likizo ya siku 28 kwa mwaka, bado wameendelea kufanya kazi kwa saa 12 kila siku.

Hiyo ni miongoni mwa changamoto tano zinazowakabili kiutendaji walizoziwasilisha kwa Serikali,  ikiwemo upungufu wa wauguzi katika vituo vya kutolea huduma, kutopata malipo ya mazingira ya kazi hatarishi na stahiki mbalimbali za kazi na  kutowepo vifungu vya kuwalipa wauguzi wafawidhi.

Pia wamesema asilimia 15 ya stahiki za watumishi inawaumiza wauguzi,  kwani ndiyo wanaofanya kazi siku sita badala ya tano kwa wiki.

Hayo wamebainisha leo Mei 6, 2024 kwenye maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani kwa ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam, huku sherehe hizo kitaifa zikitarajiwa kufanyika Mei 12 mwaka huu mkoani Tanga.

Akisoma risala ya wauguzi hao, mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, muuguzi kutoka Manispaa ya Ubungo, Tainoi Moringe amesema upungufu wa watumishi unasababisha kupunguza ubora wa huduma.

"Mapendekezo yetu Serikali iajiri wauguzi kwa kuzingatia mahitaji, kuendelea kuacha pengo hili inasababisha kupunguza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wengi kuzidi uwezo wa mtoa huduma," amesema Moringe.

Kuhusu asilimia 15 ya stahiki za watumishi, Moringe amesema ilivyo sasa kiwango hicho kinawaumiza wauguzi kwa sababu wanafanya kazi siku sita badala ya tano.

"Wengi wetu wanafanya kazi saa 12 kwa siku na kwa mwezi wanafanya kazi siku 28 hadi 30, wanapumzika siku mbili kwa mwezi lakini saa za ziada wanalipwa siku moja Sh40,000 tu hii inaathiri afya zetu na familia kwa ujumla," amesema na kuongeza kuwa hupata siku 28 za likizo kwa mwaka.

Akijibu baadhi ya changamoto ikiwemo kuajiri wauguzi, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Tanzania, Ziada Sellah amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo huku akisema bado Serikali inafanyia kazi upungufu huo katika kuajiri.

"Mwaka jana pekee Serikali iliajiri wauguzi 4,500 ni idadi kubwa ambayo haijapata kutokea. Niwasihi endeleeni kuwa wavumilivu, wakati Serikali ikiendelea kushughulika na utatuzi wa changamoto na fanyeni kazi kwa kuzingatia maadili ya uuguzi na utumishi wa umma," amesema.

Sellah amesema kada hiyo ni muhimu kwani inakaa na wagonjwa saa 24 na wanatoa huduma kwa asilimia 80 ya wataalamu wote wa afya na asilimia 20 zinazobaki, zinafanywa na kada nyingine.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi Mtambule amesema kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, Serikali inafanyia kazi changamoto zote zilizotolewa

"Niwasihi acheni kufanya mambo ya kuitia doa tasnia hii, tusimame kama watu tuliokula kiapo kuokoa maisha ya Watanzania acheni kupokea rushwa," amesema.

Maadhimisho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu: ‘Wauguzi sauti inayoongoza wekeza katika uuguzi, heshimu haki linda afya,' yalianza na matembezi ya hisani.