Wawekezaji kutumia mfumo wa dirisha moja taasisi zote zinazotoa huduma TIC
Muktasari:
Serikali katika kuhakikisha inaboresha huduma ya uwekezaji hasa kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) imeanza kuandaa mfumo wa pamoja ambao utawezesha taasisi zinazotoa huduma kwa wawekezaji iweze kusomana (Interface).
Morogoro. Serikali katika kuhakikisha inaboresha huduma ya uwekezaji hasa kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) imeanza kuandaa mfumo wa pamoja ambao utawezesha taasisi zinazotoa huduma kwa wawekezaji iweze kusomana (Interface).
Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Mifumo ya Taarifa kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Maftaa Bunini alisema hayo Juni 7, 2022 Mkoani Morogoro baada ya kuwakutanisha watendaji wakuu wa taasisi 12 zinazohusika na kutoa vibali mbalimbali kwa wawekezaji nchini.
Bunini alisema Mfumo wa Tanzania Electronic Investment Window (single window) utawawezesha wawekezaji kuweza kupata huduma za uwekezaji kupitia dirisha moja na kupitia mfumo huo watapata huduma mbalimbali ikiwemo cheti cha vivutio vya uwekezaji, usajili wa kampuni na namba ya mlipa kodi na nyingine.
Alisema mfumo huo kwa sasa wataalamu wanaukamilisha na matarajio ni kuanza Juni 15, 2022 kwa majaribio na kwa matumizi ya ndani utakuwa umekamilika na serikali itaweza kuuzindua rasmi wakati wowote.
Meneja mradi wa Mfumo wa Single Window Robert Mtendamema alisema taasisi hizo zinatengeneza dirisha moja ambalo litamwenzesha mwekezaji akiingia kwenye mfumo aweze kupata vibali mbalimbali vya uwekezaji kwa haraka na utawasaidia kupata vibali vyote kwa pamoja na kuacha kufuata kila kimoja kwenye taasisi yake na manufaa yake mwekezaji hatakuwa na urasimu wa kwenda na kuchukua muda mrefu.
Kamishna wa Uhamiaji nchini Dk Anna Makakala alisema mfumo huo utasaidia na kuwapa fursa wageni, watalii na wawekezaji popote walipo kuingia kwenye dirisha moja kupata huduma za taasisi zote ambazo anatakiwa.