Wawili wafariki baada ya kugonga treni
Muktasari:
- Dereva wa bodaboda akiwa na abiria wake wamepoteza maisha baada ya pikipiki yao kugonga treni.
Morogoro. Wanaume watu wakazi wa Lukobe wamefariki dunia papo hapo baada ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria kugonga behewa la treni katika kivuko cha reli eneo la mpaka wa kijiji cha Kingolwira na Misongeni Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 23, 2023 eneo la tukio mjini hapa, Mkazi wa mtaa wa Misongeni, Tatimu Mohamed amesema ajali hiyo imetokea katika kivuko cha reli katika vijiji hivyo kwa dereva pikipiki akiwa na abiria wake kupoteza maisha baada ya kugonga treni ya mizigo na kufariki dunia.
Tamim amesema eneo iliyotokea ajali ni eneo hatarishi ambapo hapo awali, ukifanyika ujenzi wa reli ya kisasa katika kivuko hicho kulikuwa na ulinzi uliosaidia watumiaji kuzuiliwa pale treni ikipita lakini kwa sasa eneo hilo hakuna ulinzi wowote jambo linalopelekea madereva wa vyombo vya moto kupoteza umakini wakati wa kuvuka.
“Wakati ule ujenzi wa reli ya kisasa, eneo hili lilikuwa na ulinzi, ambao ulisaidia kuzuia pikipiki na magari wakati treni inapita, kitu ambacho ni tofauti na sasa. Hakuna dereva anayekuwa makini na leo imesababisha ajali na watu wawili kufariki dunia,” amesema Tamim.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Tanki la Maji Kingolwira, Salama Ally amesema watu wawili wanaume wamefariki dunia baada ya pikipiki yao kugonga behewa la treni.
“Tunawaomba wenzetu hawa bodaboda wanapofika eneo hili wawe wanapunguza mwendo kwa sababu ya kulinda usalama, wapunguze mwendo; endapo angekuwa na mwendo mdogo, wangeweza kusimama,” ametahadharisha.
Kwa upande wa mkazi wa mtaa huo Salum Juma, amesema tukio hilo limewahudhunisha kwa dereva wa bodaboda kugonga treni na kusababisha chake na abiria wake.
Mkuu wa Stesheni ya Reli mkoa wa Morogoro, Salvatory Kimaro amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo saa 2:10 asubuhi ya leo kwa treni ya mizigo 862 iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea mikoa ya bara kugongwa na pikipiki iliyokuwa na watu wawili na kusababisha watu hao kupoteza maisha.
Kimaro amesema kisheria kivuko cha reli na barabara watumiaji wa vyombo vya moto wanalazimika kusimama kwanza kabla ya kuvuka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema tukio hilo limetokea leo asubuhi na kusababisha vifo vya watu wawili.
“Tukio hilo limetokea leo asubuhi na kusababisha vifo vya wanaume wawili waliokuwa wakisafiri kwa kutumia pikipiki kugonga treni na miili hiyo imehifadhiwa chumba cha maiti Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro,” amethibitisha Kamanda huyo na kuongeza;
“Tukio hilo limetokea kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro, Mussa Jackson (35) na Edson Kalugadi (35) kupoteza maisha kwa chombo chao kugonga treni katika kivuko cha kinachotenganisha Kijiji cha Kingolwira na Misongeni na hivyo kupoteza maisha, lakini kwa taarifa zaidi wasiliana na Kamanda wa Kikosi cha Reli.”