Waziri amsweka ndani aliyesema hajali hata akifukuzwa kazi

Wednesday July 06 2022
aliyefukuzwapiic

Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel (kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa wizara hiyo, Mhandisi Paul Koroso (kulia).

By Mwandishi Wetu

Ukerewe. Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel ameagiza kuondolewa madarakani kwa Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa wizara hiyo, Paul Koroso kutokana na mgogoro ulioibuka katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh2.9 bilioni.

Dk Mollel pia ameagiza Koroso aswekwe mahabusu akidai amemtolea majibu na lugha ya kijeuri kuwa “hajali lolote hata akifukuzwa kazi”.

Dk Mollel ametoa maagizo hayo Julai 5 akiwa mjini Nansio Ukerewe alipofika kutatua mgogoro uliobuka kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi hospitali ya Rufaa ya mkoa katika kisiwa hicho ndani ya Ziwa Victoria.

"Kutokana na changamoto zilizojitokeza kwenye mradi huu, Koroso utakoma kuwa mkuu wa Idara ya Ujenzi Wizara ya Afya. Katibu mkuu atamteua mkuu mpya wa idara ambaye atakuja kusimamia mradi wa Ukerewe," alitangaza Dk Mollel.

Pamoja na viongozi na wataalamu wa Wizara, mkoa na wilaya, kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi wa CCM, halmashauri na mkandarasi Suma JKT.

Miongozi mwa malalamiko yaliyotolewa na viongozi wa Wilaya ya Ukerewe dhidi ya Koroso ni kutowashirikisha viongozi wa wilaya na halmashauri katika utekelezaji wa mradi huo.

Advertisement

"Ofisi ya DC, halmashauri na CCM Wilaya ya Ukerewe hawakushikishwa katika utekelezaji wa mradi huu," Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Kanali Denis Mwila alimweleza Dk Mollel.

Muda mfupi kabla ya amri ya kuswekwa mahabusu, Koroso alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa Serikali ingeokoa kati ya Sh180 milioni hadi Sh260 milioni iwapo ungetekeleza mradi huo kwa mtindo wa Force account (kutumia nguvu za wananchi) badala ya ukandarasi.

Kiwango kilichotajwa na Koroso kilitofautiana na kiwango cha Sh600 milioni kilichotajwa na mhandisi wa mkoa wa Mwanza, Chagu Nghoma.

Kutokana na tofauti hiyo, Dk Mollel akamtaka Koroso kutoa ufafanuzi, ndipo akasisitiza kuwa hesabu zake ndizo sahihi kwa mujibu wa kanuni na msingi wa kitaaluma na kwamba yuko tayari kuchukullwa hatua yoyote.

"Mheshimiwa Naibu Waziri, kiwango nilichotaja kimezingatia kanuni, vigezo na hesabu za kitaaluma; nitaendelea kusisitiza hilo hata kama ukinifukuza kazi sitajali," alisema Koroso.

Kutokana na kauli hiyo, Koroso aliyeketi jirani na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi Wilaya ya Ukerewe akajikuta anawekwa chini ya ulinzi na kupelekwa mahabusu.

Advertisement