Waziri awaonya wanaovamia maeneo

What you need to know:

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amewatahadharisha wananchi wanaovamia  maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya matumizi na kwamba serikali haitawajibika kuwalipa fidia.Tanga. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amewatahadharisha wananchi wanaovamia  maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya matumizi na kwamba serikali haitawajibika kuwalipa fidia.

Dk Mabula ameyasema hayo mjini Tanga baada ya kikao cha kamati ya mawaziri wanane wa kisekta wakiongozwa na Mabura pamoja na viongozi wa Mkoa wa Tanga.

Amesema ziara hiyo ni ya kwenda mkoa kwa mkoa kushughulikia migogoro ya ardhi katika vijiji 975 ambavyo baraza la mawaziri limeridhia kufanyiwa marekebisho.

Pia vingine kuondoshwa na vingine vifanyiwe mpango wa matumizi bora ya ardhi kutokana na maamuzi yatakayotoka

Mabula amesema ndani ya mkoa huo kuna vijiji 18 kati ya  975 ambapo kati ya vijiji hivyo vijiji 14 kuna marekebisho kadhaa yatafanyika.

Amesema timu hiyo itapita kwenye maeneo hayo kufanya tathimini na watapeleka ushauri kwa serikali kuhusu hatua za kuchukua  pamoja na tathimini ya mkoa.

“Nitoe rai kwa wananchi watakaokuwa wametengewa maeneo na  kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi,  hatutarajii kuona mnaingia maeneo ya hifadhi yaliyozuiwa. Mnaingia kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, taasisi mbalimbali ambazo wamekuwa wakivamia maana hayo ndio yametufikisha hapa tulipo,”amesema Mabula.

Awali akizungumza wakati wa kikao hicho mkuu wa Mkoa wa Tanga,  Adam Malima amesema mkoa huo wameshaanza kupambana na migogoro ya ardhi kutokana na ushirikiano mzuri baina yao na mamishna wa ardhi.

“Lakini hayo ndio umekuja na kamati kuyaondoa na hayo ni mambo makubwa yaliyofanywa na kamati na ni mafanikio..Tanga na kuna maeneo ya muheza ya mashamba ya  Mkonge yaliyokuwa rasmi ya serikali watu wamevamia na katika kuvamia wenye umiliki hawakukemea jambo hilo miaka sita au tano iliyopita  sasa wanakuja kufata matumizi yake ya maeneo yao”amebainisha

Naye, kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi,  Dk Allan Kijazi amesema  kamati hiyo imepita maeneo mbalimbali na kuweza kutoa mrejesho wa maamuzi ya baraza la mawaziri kuhusu migogoro iliyopo kwenye maeneo mbalimbali nchini.