Waziri Kairuki awajia juu walimu adhabu mashuleni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Angellah Kairuki.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Angellah Kairuki amesema mwanafunzi apewe adhabu ya vikobo kwa kuzingatia maelekezo ya Waraka namba 24 wa Mwaka 2002 na kanuni zake.
Waziri Kairuki ametoa kauli hiyo leo Januari 25, 2023 wakati wa Kikao kazi cha mapitio na tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu mwaka 2022 Mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri Kairuki anatoa ufafanuzi huo ikiwa ni siku moja baada ya mjadala wa video iliyosambaa mitandaoni ikionyesha mwalimu akichapa wanafunzi chini ya unyayo wa miguu.
“Ukitoa adhabu kinyume na waraka huo ni kosa la jinai na adhabu zake zipo, tayari tumeshaanza kuchukua hatua, lakini pia ni kinyume cha haki za binadamu,” amesema Waziri Kairuki.
Kwa mujibu wa waraka huo, adhabu ya viboko itatolewa kwa mwanafunzi aliyeonyesha utovu wa nidhamu uliokithiri, kosa la jinai au kosa linaloshisha heshima ya shule.
Vigezo vya adhabu hiyo vinazingatia ukubwa wa kosa, jinsi yake, afya ya mwanafunzi, umri wake na adhabu haitazidi idadi ya viboko vinne.
Mwanafunzi wa kike atapewa adhabu ya viboko mikononi na mwalimu wa kike na mwanafunzi wa kiume kwenye makalio na mwalimu wa kiume.
Mwanafunzi wa kike atapewa adhabu na mwalimu wa kiume endapo shule hiyo haina mwalimu wa kike.
Aidha, waraka huo unamtambua mkuu wa shule pekee katika utoaji wa adhabu hiyo lakini anaweza kukasimisha jukumu hilo kwa mwalimu mwingine.
Kabla ya adhabu, mtoa adhabu (mwalimu mkuu au aliyekasimishwa) atajaza taarifa ya adhabu katika kitabu maalumu, jina la muadhibiwa, idadi ya viboko huku akitakiwa kusaini.