Waziri Kombo kumwakilisha Rais Samia uapisho Rais wa Djibouti
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo akijadili jambo na Waziri wa Bajeti wa Djibouti, Isman Ibrahim Robleh.
Muktasari:
- Guelleh mwenye umri wa miaka 78, anatarajiwa kuapishwa leo akiweka kumbukumbu ya kutawala taifa hilo dogo la Pembe ya Afrika lenye watu wapatao milioni moja kwa zaidi ya miongo
Djibouti. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo anatarajiwa kumuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sherehe za uapisho wa Rais Mteule wa Djibouti Ismaïl Omar Guelleh.
Waziri Kombo tayari amewasili nchini humo Mei 8,2026 na kupokelewa na Waziri wa Bajeti wa nchi hiyo Isman Ibrahim Robleh.
Mwakilishi huyo wa Rais Samia anatarajiwa kushiriki katika sherehe hizo zinazotarajiwa kufanyika jijini hapa leo Mei 09, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Djibouti .
Rais Guelleh amechaguliwa tena kuongoza nchi hiyo Aprili mwaka huu kwa muhula wa sita baada ya matokeo rasmi kuonyesha kuwa ameshinda kwa asilimia 97.81 ya kura ya uchaguzi wa jana Ijumaa.
Guelleh mwenye umri wa miaka 78, ametawala taifa hilo dogo la Pembe ya Afrika lenye watu wapatao milioni 1 kwa zaidi ya miongo miwili.
Mwaka jana, wabunge wa nchi hiyo walifutilia mbali sheria ya ukomo wa umri wa rais. Maofisa wa uchaguzi wamesema kura hiyo ilikuwa ya amani.
Katika uchaguzi huo wa Aprili, Rais huyo akikabiliana na mpinzani mmoja, Mohamed Farah Samatar, mwanachama wa zamani wa chama tawala, katika uchaguzi ambao wachambuzi wanasema ulitoa ushindani mdogo halali.