Waziri Mchengerwa azindua bodi mbili za wakurugenzi Tanapa, TTB

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa akizindua bodi hizo jijini Arusha
Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amezindua bodi mbili za wakurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), alizoziteua hivi karibuni na kuzitaka bodi hizo kuhakikisha zinapadisha kiwango cha watalii kuingia nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo leo Jumanne Agosti 22 jijini Arusha, Waziri Mchengerwa amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua tena, Jenerali mstaafu George Waitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Tanapa pamoja na Balozi Dk Ramadhan Dau kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TTB.
Amesema uteuzi huo umezingatia weledi, uzoefu, uchapakazi na uzalendo katika kutumikia taifa na kuzitaka bodi hizo kusimamia masilahi mapana ya nchi katika kukuza uchumi wa taifa, upatikanaji wa fedha za kigeni na uzalishaji ajira.
Amezitaka bodi hizo kukidhi malengo ya Taifa ya mwaka 2020/25 ya kuhakikisha idadi ya watalii milioni 5 na mapato ya taifa ya dola za Marekani bilioni 6 yanafikiwa.
"Nina imani Taasisi ya Tanapa inayosimamia vivutio vyetu ya utalii ikiwemo Hifadhi ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro pamoja na Bodi ya Utalii yenye dhamana ya kutangaza vivutio hivyo ndani na nje ya nchi, zitachochea kwa kiasi kikubwa kufikia malengo hayo," amesema.
Amezitaka Bodi ya Utalii Tanzania kujipanga kikamilifu ili kuongeza idadi ya watalii ukizingatia kwamba idadi ya watalii 6,000 wa sasa ni ndogo ukizingatia ukubwa wa nchi, wingi wa hifadhi pamoja na vivutio vilivyopo haviendani na idadi hiyo ya watalii.
Aidha amezitaka bodi hizo za utalii kufanya kazi usiku na mchana kujiboresha na kuondokana na utendaji wa mazoea ili kwenda na kasi ambayo Rais Samia anaihitaji ya kutangaza vivutio na kuongeza idadi ya watalii nchini.
"Huko nyuma kupitia mitandao ya kijamii wadau wetu wa utalii wamekuwa wakilalamika kwamba viongozi wa bodi ya utalii wamekuwa wakisafiri kwa ajili ya kufanya shopping nje ya nchi wakati mwingine tulipata aibu nchini Korea Kusini walitengeneza maboksi kutangaza utalii wa Tanzania hii ni aibu kubwa," amesema.
Aidha akitolea mfano suala la uwekezaji wa vyumba vya kulala wageni hapa nchini ,amesema kuna vyumba takribani 120,000 kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na nchi ya Kenya ambayo inavyumba zaidi ya Sh1.5 milioni.
"Tuna kwenda kufanya mapitio ya sheria itakayowapa mamlaka ya kuhakikisha mnaishauri serikali kwenye eneo la uwekezaji na kujua ni namna gani tunakwenda kuongeza idadi ya watalii, kuongeza vyumba vya kulala watalii na eneo la ukarimu," amesema.
Ameongeza mpango mwingine wa TTB ni kuhakikisha inateka soko la watalii wanaotoka China kwani hivi sasa ni watalii 34,000 tu wanaokuja nchini wakati watalii wanaotoka China kwenda mataifa mbalimbali duniani wanakaribia milioni 200 kwa mwaka, hivyo ni lazima walau watalii milioni 3 kutoka China waje hapa nchini.
Amefafanua takwimu zinaonesha kwamba bado hatujalifikia soko la watalii wengi duniani hasa kutoka bara la Asia.
Akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa bodi hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tanapa, Jenerali mstaafu George Waitara amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumwamini na kumteua katika kipindi kingine cha tatu kuongoza bodi hiyo.
"Natambua Rais Samia ametuamini na sisi kazi yetu ni kuchapa kazi hatutamwangusha na imani hii tutailinda tunachohitaji kwako ni ushirikiano tu," amesema.
Walitara ametoa onyo kwa majangili walioanza kujitokeza ambao aliwaita ni wadogo kwani kazi kubwa ya kutokomeza ujangili nchini imefanyika hasa baada ya kuzinduliwa kwa jeshi Usu.