Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Mkuu apiga marufuku ukamataji bidhaa za wafanyabiashara

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi jimboni kwake Iramba mkoani Singida leo Jumamosi Juni 13, 2026.

Muktasari:

  • Msimamo huo umeleta matumaini ya wafanyabiashara wadogo, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia ukamataji wa bidhaa na mali zao unaowaathiri kiuchumi.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wadogo nchini wamepata ahueni baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kupigilia msumari onyo kwa watendaji na maofisa wa udhibiti wanaokamata bidhaa za wananchi kwa madai ya ukaguzi, akisema vitendo hivyo vinaharibu mitaji ya watu na kuwatumbukiza kwenye umaskini.

Agizo kama hilo alilitoa Desemba 8, 2025, akiwa mkoani Dodoma alipowataka viongozi wa majiji na halmashauri nchini kuhakikisha wafanyabiashara hawanyang’anywi bidhaa zao.

Leo Juni 13, 2026, akiwa jimboni kwake Iramba mkoani Singida, Waziri Mkuu amerejea agizo hilo akisema Serikali haiwezi kuruhusu wananchi wanaojitafutia riziki kwa jasho lao kuendelea kunyanyaswa kwa kupokonywa bidhaa ambazo ndizo msingi wa maisha yao ya kila siku.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliolenga kuwashukuru wananchi wa jimbo la Iramba mkoani Singida, Dk Mwigulu ameeleza kutoridhishwa na vitendo vya maofisa kuchukua mafuta ya kula kutoka kwa wafanyabiashara wadogo kwa madai ya kukagua ujazo wake, licha ya kuwepo kwa maelekezo ya awali yaliyokataza ukamataji wa mali za wananchi.

"Nimesema msikamate hata bakuli la maharagwe. Kwa nini mmeenda kuchukua mafuta ya wafanyabiashara? Dumu moja la mafuta ndio mtaji wake, nyie mnachukuaje?"

Ametoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi mmoja aliyedai kuwa bidhaa zao zilichukuliwa na maofisa wa ukaguzi na kuwafanya kushindwa kuendelea na biashara zao kwa siku kadhaa.

Mfanyabiashara huyo, amemweleza Waziri Mkuu kuwa wamekuwa wakikimbizwa na kunyimwa fursa ya kufanya biashara kwa takribani siku tano kutokana na bidhaa zao kuchukuliwa.

"Tumekuwa tukikaa nyumbani bila kufanya biashara kwa sababu bidhaa zetu zimechukuliwa," amesema.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Waziri Mkuu ameamuru bidhaa zote zilizokamatwa zirudishwe kwa wamiliki wake ili waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato.

Aidha, amemwagiza Mkuu wa Wilaya kuwachukulia hatua maofisa waliohusika na ukamataji huo, akisisitiza kuwa vitendo vya namna hiyo haviendani na dhamira ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Amesema bidhaa zinazouzwa na wafanyabiashara wadogo ndizo ofisi zao na chanzo kikuu cha riziki kwa maelfu ya familia za Watanzania, hivyo zinapaswa kulindwa badala ya kuzuiwa.

"Msitie watu umaskini. Hizi ndizo ofisi zao, ndizo mitaji yao. Serikali haiwezi kuwa chanzo cha kuwafilisi wananchi wake," amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amerejea maelekezo yake kuhusu ukamataji wa vyombo vya usafiri, akisisitiza kuwa magari, pikipiki na baiskeli zisikamatwe isipokuwa pale zinapohusika na makosa makubwa yanayoruhusu hatua hizo kisheria.

Amesema baadhi ya watumishi wa umma wanapaswa kutambua ugumu wa maisha unaowakabili wananchi wanaojitegemea kupitia biashara ndogo ndogo na kuacha kutumia mamlaka yao kwa namna inayowaumiza wananchi.

Desemba 8, 2025, Dk Mwigulu akiwa mkoani Dodoma alisema: “Msichukue bidhaa za raia; hizo ndio ofisi za raia wetu, hata kama kuna jambo ambalo anapaswa kuelekezwa kuhusu masuala ya utaratibu basi mshughulikie jambo linalohusu utaratibu, msizuie mitaji ya watu. Utaratibu wa kuchukua bidhaa haukubaliki na hakuna uhalali wa kuchukua bidhaa za raia. Msicheze na mitaji ya watu.”

Agizo hilo la Dk Mwigulu alilitoa wakati akizungumza na wafanyabiashara katika soko la Machinga jijini Dodoma baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Richard Joseph ambaye ni mfanyabiashara sokoni hapo, aliyedai bidhaa zake zimechukuliwa na watumishi wa jiji.

Dk Mwigulu aliwaagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri wahakikishe wanafuatilia suala hilo na wahusika warudishe bidhaa za mfanyabiashara.

“Kama wamepotea nazo, wachukuliwe hatua kama wezi wengine. Mheshimiwa Rais hapendi uonevu, ni mtu wa haki,” alisema.