Waziri Ndumbaro aipa maagizo Rita

Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Dk Damas Ndumbaro

Muktasari:

Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Dk Damas Ndumbaro ameongoza wanafunzi wa Shule ya Msingi Gongolamboto, jijini Dar es Salaam katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya tano ya siku ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu Barani Afrika.

Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Dk Damas Ndumbaro ameielekeza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kuimarisha huduma wanazotoa mikoa ya pembezoni kwa kuhakikisha kunakuwa na watumishi na vifaa vya kutosha ili kukabiliana na watu ambao sio waaminifu.

 Maagizo hayo ameyatoa jijini Dar es Salaam leo Jumatano Agosti 10, 2022 katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya tano ya siku ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu Barani Afrika yaliyofanyika Shule ya Msingi Gongolamboto.

"Tanzania imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuongeza kasi ya usajili kupitia mkakati wa kitaifa wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu ambao tayari umeshaanza kutekelezwa kwa program mbalimbali lakini Rita kama chombo cha kutekeleza nilazima mzingatie maagizo ili kuongeza weledi na kupata taarifa sahihi," amesema 

Dk Ndumbaro amesema Serikali bado inaendelea kujipanga kuiboresha mifumo ya Tehama ili kuifanya Rita kuwa ya kidijitali kwa kuongeza matumizi ya teknolojia katika kusajili na kuhifadhi taarifa baada ya kutambua manufaa ya taarifa Kwa Maendeleo ya Taifa.

Naye Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Slaa amesema Serikali inapaswa kuelekeza nguvu kwenye kuweka mifumo ya kutatua changamoto ya mirasi inayojitokeza kwenye jamii pindi wenza wao wanapofariki.

"Tumeona jitihada zimewekwa kwenye kusajili akini kwakuwa taasisi hiyo inashughulika na mirasi tunaomba muweke nguvu eneo hilo kumaliza utata unaojitokeza katika jamii zetu," amesema


Kwa upande wake,  Kabidhi Wasii Mkuu wa Rita,Angela Anatory alisema bado wanaendelea na mpango wa usajili wa watoto wa umri wa miaka 5-17 ambao unatekelezwa kwa kutoa huduma za usajili katika shule wanazosoma.

“Tutaongeza kasi ya usajili kwa watoto wa kundi hili kwani tumedhamiria kwamba ifikapo mwaka 2025 wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari wawe wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa kama Serikali ilivyokusudia,"alisema

Mchambuzi wa Maendeleo na Takwimu (UNFPA), Ramadhan Hangwa alipigia chapuo uboreshaji wa mifumo kwa kufanya hivyo kutasaidia hata watoto wakizaliwa wapewe cheti Cha kuzaliwa kama haki yao ya msingi.

Alisema hata tathimini waliyofanya kwa mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania Sensa zao zinatumia gharama kubwa kwa sababu wanakosa taarifa sahihi kwenye kurekodi idadi ya matukio.

"Kuboresha mifumo kutasaidia michakato ya sensa kuwa mifupi Kwa maana hata madodoso hayatakuwa na maswali mengi lakini taarifa zitapatikana Kwa wakati na serikali kujua mahitaji yake," alisema