Waziri Silaa asisitiza umuhimu ulinzi maeneo ya hifadhi Tabora

Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa akizungumza na watumishi wa sekta ya Ardhi Mkoa wa Tabora (hawapo pichani).Picha na Robert Kakwesi.

Muktasari:

Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa amewataka watumishi wa Serikali Mkoa wa Tabora kulinda kwa wivu mkubwa maeneo yote ya hifadhi mkoani humo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Tabora. Watumishi wa Serikali Mkoa wa Tabora wameagizwa kulinda kwa wivu mkubwa maeneo ya hifadhi mkoani humo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa leo Oktoba 9, 2023 wakati akizungumza na watumishi wa Serikali mkoani Tabora.

Amesema zaidi ya asilimia 46 ya eneo la Mkoa wa Tabora wenye ukubwa wa kilometa za mraba 75,000 umetengwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi, hivyo ni muhimu kwa watumishi wote wenye dhamana kuhakikisha maeneo hayo yanahifadhiwa.

‘’Zaidi ya kilometa za mraba 32,000, sawa na asilimia 46 ya eneo lote la kilometa za mraba 75,000 za Mkoa wa Tabora ni hifadhi; hivyo ni wajibu na jukumu la watumishi wote wa Serikali kuhakikisha siyo tu maeneo yote yanahifadhi vema, bali pia inanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo,’’ amesema Waziri Silaa

Ametaja baadhi ya umuhimu wa maeneo ya uhifadhi mkoani Tabora kuwa uhakika wa maji kwa ajili ya matumizi ya kijamii na kiuchumi huku akifichua kuwa baadhi ya mito inayoanzia mkoani humo huchangia maji katika bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere.

‘’Wanaoingia na kufanya shughuli za binadamu ndani ya maeneo ya hifadhi wanahatarisha vyanzo vya maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi,’’ amesema Waziri Silaa

Amewataka viongozi na watendaji katika taasisi za umma kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao, huku akifichua kuwa matumizi ya Tehama itamaliza migogoro inayohusisha mipaka ya maeneo ya uhifadhi na makazi ya watu.

Ameziagiza mamlaka za halmashauri kote nchini kutenga, kupima na kulinda maeneo ya wazi dhidi ya uvamizi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji kwa waziri Silaa, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Louis Bura amesema wilaya hiyo haina migogoro mikubwa ya ardhi isipokuwa malalamiko madogo ambayo yanaendelea kutatuliwa.