Waziri Ummy aonya michango holela shule za msingi, sekondari
Muktasari:
- Waziri Ummy ameonya michango holela kwa wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza na wa shule za msingi, akisema wapo katika mchakato wa kubaini watu wanaofanya vitendo hivyo ili kutoa mfano wa kuwachukulia hatua.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ummy Mwalimu amewataka wakuu shule za sekondari na msingi nchini kujiepusha na michango holela kwa wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza, akisema hatua hiyo inaleta vikwazo kwa watoto kuanza masomo yao.
“Niwaambie ukweli tunataka tuwapate walimu wa mfano ili tuwachukulie hatua. Inatosha sasa kwa shule za sekondari na msingi za sekondari, kama kuna mchango umekubaliwa fuateni utaratibu za kuchangisha wazazi na walezi.
“Tujiepushe kuwachangisha wazazi au walezi, michango holela kinyume cha utaratibu. Nataka niwaambie ukweli, bila kupepesa macho tunatafuta shule mbili za mfano ili tuzichukulie hatua,” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameeleza hayo leo Jumatano Desemba 15, 2021 wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (Tahossa), uliofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 5,000 wa umoja unaojumuisha shule za Serikali na binafsi.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy ameunga mkono maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuwataka wadau wa elimu kufuata utaratibu uliowekwa katika utekelezaji wa majukumu.
Kwenye mkutano huo, Waziri Ummy amewasomea wakuu wa shule hizo maelekezo hayo yaliyotolewa na Kamishna wa Elimu Lyabwene Mtahabwa, ikiwataka wadau hao kuzingatia Waraka wa elimu namba 14 wa mwaka 1997.
Waraka huo wa elimu unazungumzia umuhimu wa walimu kuhudhuria vipindi vya darasani na kufundisha, pia waraka wa elimu namba sita wa mwaka 2011 unaohusu kupiga marufuku utitiri wa mitihani.
Pia amewasomea waraka wa elimu namba nane wa mwaka 2011 kuhusu kukithiri kwa michango shuleni.
Katika maelekezo yake kupitia barua iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, Mtahabwa ameeleza baadhi ya maeneo yanayokiukwa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa ratiba ndefu ya masomo inayoanzia alfajiri na kuendelea, kuzuia likizo kwa wanafunzi hususan walioko kwenye madarasa ya mitihani.
Maeneo mengine ni pamoja na shule kutoza michango kutoka kwa wazazi au walezi bila ridhaa yao kwa ajili majaribio ya mitihani ya mara kwa mara na utoaji wa adhabu ikiwemo ya viboko, bila kuzimngatia taratibu zilizopo.
Akizungumzia jambo hilo, Waziri Ummy amekubaliana na maelekezo hayo akiwataka wakuu wa shule kuyasimiamia na kuyatekeleza kwa ukamilifu.Waziri huyo alikwenda mbali kwa kuwasomea maelekezo hayo wakuu wa shule waliohudhuria mkutano huo.
Mbali na hilo, Waziri Ummy amesema hatawavumilia baadhi ya wakuu wa shule wanaowadhalilisha wanafunzi wa kike, akisema watakaobainika hawatarudi kazini. Pia amewakata wakuu hao kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea wanafunzi walioachwa shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa sekondari ya Enong’o wilayani Simanjiro, Thomas Nno amesema watatekeleza maelekezo hayo kama ambavyo Serikali imeagiza, akisema ni sahihi wakati wa likizo mwanafunzi kumpumzika na kukutana na familia yake.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Teknoloji, Dk Leonard Akwilapo amesema Serikali imeshakamilisha uandishi wa vitabu wa vyote, vitakavyochapishwa Januari mwakani, akisema kilichobaki ni taratibu za uhakiki ili kuondoa makossa.