Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Ummy: Takribani watu 132, 000 nchini huambukizwa Kifua Kikuu kila mwaka

Waziri wa afya Ummy Mwalimu akizungumza katika mkutano wa makatibu wakuu na waratibu wa mipango ya nchi ya kupambana na ugonjwawa Kifua Kikuu kutoka nchi 11 za Afrika jijini Arusha.

Muktasari:

  • Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kwamba takribani watu 132, 000 hapa nchini, wanaambukizwa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kila mwaka, huku wengine 25, 800 huripotiwa kufa ambao ni wastani wa watu 70 wanaopoteza maisha kila siku.

Arusha. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kwamba takribani watu 132, 000 hapa nchini, wanaambukizwa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kila mwaka, huku wengine 25, 800 huripotiwa kufariki ambao ni wastani wa watu 70 wanaopoteza maisha kila siku.

Ummy ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa makatibu wakuu na waratibu wa mipango ya nchi ya kupambana na ugonjwa huo kutoka nchi 11 za Afrika.

Ummy amesema kuwa, lengo la mkutano huo ni kujadili jinsi gani nchi za Afrika zinaweza kuja na ubunifu na mikakati mipya ya kutokomeza ugonjwa huo Afrika na duniani, kwani takwimu za kidunia zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 10.5 wanaambukizwa TB.

"Tulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa  Uviko 19 na hatukuwahi  kufikia vifo hivi, lakini TB ni kama ugonjwa wa maskini haujapata sauti au mwitikio  kutoka kwa viongozi na jamii namna ya kuutokomeza," amesema.

Amesema, Serikali kwa kushirikiana na mfuko wa dunia wa kupambana na kifua kikuu, Ukimwi na malaria (Global Fund) wameweza kukutana ili kuona jinsi gani ya kufikia malengo ya kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.

"Sisi kama Tanzania tunaona hili  linawezekana mwaka 2015 tulikuwa tunaibua  wagonjwa wa kifua kikuu kwa  asilimia 39 lakini tuliongeza jitihada hadi kufikia asilimia 65 kwa kuwatumia  wahudumu wa afya  ngazi ya jamii," amesema Waziri Ummy.

Amesema wizara yake ina  mkakati wa kuwekeza kwa jamii sanjari na kutoa mafunzo ya miezi mitatu kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 5,000 kila mwaka, na kuyatumia maduka ya dawa baridi na waganga wa tiba asili katika mapambano ya TB hapa nchini.

Awali Mkuu wa kifua kikuu kwenye mpango wa dunia wa TB na Malaria kutoka Global Fund, Dk Eliud Wandwalo amesema kwamba mfuko huo unasaidia zaidi ya nchi 100 ulimwenguni ikiwemo Tanzania.

Amesema ugonjwa wa kifua kikuu unaua watu wengi zaidi duniani hasa nchi maskini ambazo zina watu wengi, hivyo mkutano huu wameuleta hapa nchini kwani imeonyesha Tanzania ni kinara wa maambukizi ya TB

Amesema kwamba shirika lao limekuwa likitoa Takribani Dola 800 milioni kwa mwaka katika mapambano ya kifua kikuu Malaria pamoja na Ukimwi ambapo Takribani dola 4 bilioni kwa Bara la Afrika.

Amesema nchi ya India ndio yenye maambukizi makubwa ya TB duniani, takribani watu milioni 2 kila mwaka wanaugua TB na katika nchi za Afrika nchi ya Nigeria na Afrika kusini ndio zinaongoza, na nchi zenye maambukizi makubwa duniani ni 30  zikiwemo 17 kutoka Afrika.