Wizara ya Elimu kupandisha bango la Kiswahili mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza safari ya kupandisha bango la kutambua lugha ya Kiswahili kwenye mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania.


Dodoma. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza safari ya kupandisha bango la kutambua lugha ya Kiswahili kwenye mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe ameyasema hayo leo Jumamosi Desemba 03,2022 wakati akikabidhi bango la Kiswahili katika mlima Kilimanjaro.

“Sisi tumedhamiria tunapoadhimisha uhuru wa nchi yetu basi tuone fahari ya kutoa hamasa ya kufundisha kiswahili nchini na nchi majirani. Kuna sababu ya kutambua Kiswahili katika miaka 61 ya uhuru,”amesema.

Amesema wameamua kutambua lugha ya Kiswahili katika maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru kwa kupandisha bango katika mlima Kilimanjaro huku kauli mbiu ikiwa ni Kiswahili kileleni.

Profesa Mdoe amesema lengo ni kueneza Kiswahili kwa mataifa mengi zaidi kuliko hivi sasa duniani na kwa kuanzia wanatangaza Kiswahili kwa kupandisha bango kwenye mlima huo.

Amesema hivi sasa Kiswahili kinawazungumzaji takribani milioni milioni 250 na vyuo visivyopungua 150 vinavyofundisha lugha hiyo ni 150 huku radio zinazorusha vipindi kwa Kiswahili.

Pia Profesa Mdoe amesema katika vyuo nchini vina makubaliano na vyuo vya nje ya nchi katika kufundisha Kiswahili na wizara yake inamikataba na wizara za nje nchi kufundishia lugha hiyo.

Mwandishi wa Vitabu vya Kiswahili kutoka nchini Misri, Menna Yasser, amesema kwa kuzungumza kingereza wala kuvaa mavazi ya kizungu hayawezi kumfanya mtu awe mstaarabu.

“Unapaswa kuhifadhi utambulisho wako mwenyewe. Sasa sisi tunafahamu lugha ni hali ya kuelezea watu, ni ulimi ukitaka kuelezea hali yako utatumia mdomo wako, ulimi wako na lugha,”amesema.