Wizara yarejesha mafunzo
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akizungumza na Maofisa wa uhamiaji nchini waliokutana mkoani Kilimanjaro katika chuo cha Uhamiaji cha Kikanda(TRITA).Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema imerejesha mafunzo ya askari, wakaguzi na maofisa wa uhamiaji nchini yaliyokuwa yamesitishwa kwa muda mrefu.
Moshi. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema imerejesha mafunzo ya askari, wakaguzi na maofisa wa uhamiaji nchini yaliyokuwa yamesitishwa kwa muda mrefu.
Hayo yamesemwa leo Novemba 29, 2022 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini, wakati wa kikao kazi cha Maofisa waandamizi, Wakuu wa vitengo, maofisa utumishi na Maofisa sheria wa mikoa wa uhamiaji nchini katika kikao kilichofanyika katika chuo cha uhamiaji cha kikanda (TRITA).
"Tayari zimetengwa Sh900 milioni kwa ajili ya mafunzo ya askari, Wakaguzi na maofisa wa uhamiaji, haya mafunzo yalikuwa yamesismamishwa kwa muda mrefu kidogo lakini sasa yamerejeshwa na serikali inayagharamikia,"amesema Sagini
Pamoja na fedha hizo za mafunzo, amesema Serikali imetenga Sh1.3 bilioni kwa ajili ya sare za uhamiaji, kuendeleza ofisi za mikoa na wilaya pamoja na nyumba za watumishi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Geita, Manyara, Butiama na Mlele.
"Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Sukuhu Hassan kwa mambo mengi mema anayoyafanya pamoja na serikali yake, sisi tunamuahidi kuendelea kutekeleza kazi na majukumu tuliyopewa kwa uamanifu, weledi, uaminifu, bidii na kutenda kulingana na viapo vyetu katika kulitumikia Taifa kizalendo,"
Amesema kwa wale wanaoenda kinyume na kukiuka maadili ya kazi zao kwa makusudi hatua kali za kinidhamu na za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Akizungumza na maofisa hao, aliwataka kuzingatia misingi ya sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyopo katika wizara hiyo wakati wote wanapotekeleza majukumu yao na kwamba wizara hiyo kwa kushirikiana na Idara ya uhamiaji haitawalinda wala kusita kuchukua hatua kwa watumishi wanaokwenda kinyume na maadili kwa maslahi yao binafsi.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini, Dk Anna Makakala amesema kikao kazi hicho kilichokutanishwa Maofisa katika idara mbalimbali kitasaidia kubadilishana uzoefu na kuelimishana mambo mbalimbali ya kiutendaji na namna ya kushughulikia mashauri ya nidhamu katika ofisi za uhamiaji.