Yanga walia kuonewa Ligi Kuu Bara

Friday February 19 2021
yangapicc
By Clezencia Tryphone

SARE mbili mfululizo walizozipata Yanga katika michezo yao ya Ligi Kuu Bara zimewaibua viongozi wa timu hiyo na kuzituhumu mamlaka zinazosimamia soka nchini kuchangia juu ya matokeo hayo.

Yanga imetoka sare ya bao 1-1 na Mbeya City mchezo uliopigwa jijini Mbeya na juzi kukubali sare dhidi ya Kagera Sugar ya bao 3-3 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia shutma hizo Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela amesema, kwa sasa timu yao haitendewi haki na mamlaka zote zinazosimamia soka, kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kamati ya Waamuzi pamoja na Kamati ya saa 72.

Mwakalebela amesema, katika mchezo wao na Mbeya City walinyimwa penati mbili za wazi ambazo walistaili kuzipata na zingepelekea wao kushinda mchezo huo na sio kupata pointi moja.

Amesema mbali na mchezo huo hata mchezo na Kagera nao walinyimwa penati ambazo zingewafanya kupata pointi tatu badala ya kupata moja, huku akikiri kuamini mamlaka hizo kuna timu inayoandaliwa kuwa bingwa.

"Tumewakosea nini mpaka mnatufanyia hivi, au hatustahili kucheza Ligi ya Tanzania tujue, hivi vitu vinavyofanyika uwanjani vinawafanya hata mashabiki kukosa uvumulivu na kufanya fujo, Yanga tumechoka kuonewa waziwazi,"

Advertisement

"Kama kuna bingwa kaandaliwa basi apewe kombe tujue moja, tunatarajia kamati husika zitatoa maamuzi katika hizo mechi zetu mbili na hao waamuzi wachukuliwe hatua stahiki tusitolewe kwenye mstari wetu wa kutwaa ubingwa msimu huu," amesisitiza Mwakalebela.

Mwakalebela amesema, Yanga wametumia gharama kubwa kuiandaa timu hiyo hivyo namna matukio yanayotokea na kufumbiwa macho na vyombo husika yanawafanya kutafsiri vibaya juu yao.

Advertisement