Yara Tanzania yajipanga kuongeza tija sekta ya mfugo, uvuvi

Dar es Salaam. Kampuni ya Yara Tanzania imezindua bidhaa za lishe ya mifugo na uvuvi zitakazosaidia kuchochea mageuzi ya sekta hiyo hususani katika kukuza mapato wafugaji na wavuvi.

Kwa mujibu wa Yara Tanzania, bidhaa hizo zinazowezesha unenepeshaji, ukuaji wenye afya, kinga ya magonjwa na virutubisho kwa vipimo tofauti ni pamoja na Maziwa Pro, Kynofos 21, Phospro 17, Phossure 12 na Kimtrafos 12 Grande.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumanne, Septemba 19, 2023 mkoani Iringa, ikiwa ni siku chache baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula la Afrika (AGRF), uliochechemua huduma ya chakula kwa uhakika, ubora na utoshelevu.

Katika wasilisho lake, mtaalam wa lishe ya mifugo kutoka kampuni hiyo, Dk Peter Mukua amesema bidhaa ya ‘Maziwa Pro’ itasaidia ongezeko la lita tatu zaidi kwa ng'ombe kwa siku ikilinganishwa na wastani wa nusu lita hadi lita mbili za maziwa kwa sasa baada ya kuongeza kinga ya mifugo na uboreshaji wa uzazi.

“Maziwa Pro inashughulikia upungufu wa fosforasi unaochangia uzalishaji duni, ina Phosphorous iliyoongezewa nguvu kwa kuchanganywa na molasi (molasses) ya unga na asilimia 15 ya protini,”amesema Dk Mukua.

Kwa mujibu wa Bodi ya Maziwa ya Tanzania (TDB), Tanzania ina upungufu wa uzalishaji wa maziwa wa takriban lita bilioni tisa kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya lita bilioni 12 na Mwaka jana Taifa lilitumia Sh23 bilioni kuagiza maziwa ili kukidhi upungufu huo, hali iliyosababisha kupoteza ajira muhimu na mapato ya kigeni.

“Kwa bidhaa nyingine kama Kynofos 21 zinatatua matatizo ya maganda dhaifu ya mayai, miguu dhaifu ya kuku hali inayofanya washindwe kutembea, tatizo la kudonoana wao kwa wao hususani kwa kuku wa mayai, kasi ndogo ya ukuaji, na ongezeko dogo la uzito kwa kuku wa nyama na nguruwe,” amesema Dk Mukua.

Mkurugenzi Mtendaji wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo amesema kampuni hiyo itaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali, wafugaji na wazalishaji wa chakula cha mifugo ili kuboresha wingi na ubora wa uzalishaji wa maziwa, nyama, mayai na Samaki.

“Yara Tanzania, tunahakikisha kutoa lishe ya mifugo kwa ufanisi sawa na tulivyofanya miaka yote kwa kutoa suluhisho la uzalishaji wa mazao kwa wakulima kupitia mbolea bora na huduma za ugani," amesema.

Tanzania ambayo ni nchi ya tatu barani Afrika kuanzisha lishe ya mifugo kutoka Yara International ASA ya Norway baada ya Afrika Kusini na Kenya inashika nafasi ya pili kwa mifugo Afrika na namba tisa kidunia.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo kati ya 2006/07 na 2020/21, ng’ombe waliongezeka kutoka milioni 18.5 hadi milioni 33.9, mbuzi milioni 13.1 hadi milioni 24.5 ,kondoo milioni 3.5 hadi milioni 8.5 na kuku milioni 30 hadi milioni 87.7 lakini Serikali imekuwa ikikiri tija yake kuwa ndogo. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga amesema sekta ya mifugo imekuwa na mchango wa asilimia saba katika pato la taifa, kiwango ambacho ni kidogo kulingana na utajiri wa mifugo nchini.

“Hivyo basi juhudi za pamoja kati ya sekta ya umma na binafsi zinahitajika kukuza uzalishaji na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni ambazo hutumika kila mwaka kuagiza maziwa, nyama na mayai kutoka nje ya nchi, na hivyo basi kuua ajira kwa vijana wetu huku Serikali ikipoteza mapato,” amesema RC Sendiga akifafanua:

“Kuja kwa hii lishe bora itasaidia wafugaji wetu na wajasiriamali wanaotengeneza vyakula vya mifugo kuondokana na ukosefu wa lishe sahihi na raslimali yake inayochangia kuzorota kwa sekta ya ufugaji.”

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Iringa amesema pamoja na matokeo mazuri ya kunufaika na bidhaa hizo katika lishe bora pia itasaidia kunusuru kiwango cha uharibifu wa mazingira pamoja na changamoto ya utapiamlo unaoendelea kwa sasa mkoani hapo.

Yara International ASA ya Norway ni mtengenezaji wa kimataifa wa vyakula vya mifugo kutoa bidhaa za lishe ya mifugo kwa wateja katika nchi zaidi ya 70 ulimwenguni. Viwanda vya uzalishaji wa chakula cha mifugo viko Helsingborg ( Sweden), Kokkola (Finland), Durban (Afrika Kusini), Le Havre (Ufaransa), na Brunsbüttel (Ujerumani).