Zimamoto wauzima moto jengo la Tamisemi Dodoma

Muktasari:
- Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma limeuzima moto uliodumu kwa saa kadhaa na kuteketeza baadhi ya sehemu ya jengo la ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Dodoma. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma limeuzima moto uliodumu kwa saa kadhaa na kuteketeza baadhi ya sehemu ya jengo la ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mto huo ulianza saa 11 jioni na ilipofika saa 1 usiku jeshi hilo lilikuwa limefanikiwa kuuzima.
Wakizungumza na Mwananchi Digital mashuhuda wa tukio hilo wamesema moto huo ulianza kwa kasi huku Rashid Mazrui akieleza kuwa alikuwa akiingia msikiti wa Nunge kwa ajili ya kufanya ibada lakini alipoangalia upande wa pili aliona moshi ukitoka katika jengo la Tamisemi.
“Nikaacha kwenda kuswali na kuanza kuangalia kuna nini nikaona wafanyakazi wakikimbia kuomba msaada, tukaanza kuwasaidia kuwatoa nje,” amesema.
Maimuna Shaaban mfanyakazi wa Tamisemi amesema moto huo ulianza kama mzaha na walifanya juhudi za kuuzima lakini walipoona unazidi walilazimika kupiga simu Zimamoto.
“Tunashukuru wamefika kwa wakati na wanaendelea kuuzima kama unavyoona,” amesema.