Zitto awataka Jaji Mkuu, Biswalo waachie ngazi
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akizungumza katika mahojiano na Mhariri wa siasa wa gazeti la Mwananchi, Salehe Mohamed, katika ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George
Muktasari:
- Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kunusa harufu ya ufisadi kwenye fedha zilizolipwa kwa ‘Plea Bargaining’ chama cha ACT Wazalendo kimewataka waliokuwa viongozi wa mahakama wakati huo kuachia ngazi.
Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemtaka Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Jaji wa Mahakama Kuu, Biswalo Mganga wajiuzulu kupisha uchunguzi wa upotevu mabilioni ya fedha ya ‘Plea Bargaining’.Taarifa ya upotevu wa fedha hizo, ilidokezwa juzi na Rais Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake baada ya kuwaapisha wajumbe wa kamati ya kupitia mfumo wa haki jinai nchini.Katika hafla hiyo, Rais Samia alisema: “Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kulikuwa na ngoma kubwa kidogo inachezwa, mpaka kukusanya fedha za wale wa plea bargaining. Pesa zile nyingine zinaonekana na nyingine hazionekani.“Uki-trace (ukifuatilia) utaambiwa kuna akaunti China, sijui zimepelekwa pesa zipi. Tukatizame haya yote, kuna nini hasa kilichoikumba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,” alisema Rais Samia.Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo, Februari 2, 2023 Kabwe amesema wawili hao wanapaswa kujiuzulu kwa kuwa hayo yalifanyika wakiwa wasimamizi wakuu wa eneo hilo.“Kwa maelezo hayo ya Rais, aliyekuwa msimamizi mkuu wa muhimili wa haki ni Jaji Mkuu (Profesa Juma) ambaye hadi sasa yupo na Mganga alikuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).“Na sasa ufisadi unanukia wawili hao hawana sifa tena ya kuendelea kutumikia nyadhifa za kisheria walizonazo sasa,” amesema.Kwa mujibu wa Kabwe aliyezungumza kwa niaba ya ACT Wazalendo, viongozi hao wanapaswa kujiuzulu kupisha uchunguzi, kadhalika kuusitiri muhimili wa mahakama.