Zuio la mikutano latinga 2020 likionyesha taswira halisi ya utendaji wa Jeshi la Polisi

Ibara ya 3 (1) ya Katiba ya mwaka 1977 inasema “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”

Misingi ya mfumo wa siasa wa vyama vingi pia unasisitizwa katika sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 na marejeo yake yote kuanzia mwaka 2002 inayotoa haki na usawa katika shughuli za kisiasa kwa vyama vyote vyenye usajili wa kudumu.

Maandamano ya amani na mikutano ya hadhara yenye lengo la kunadi na kueneza sera ili kutafuta ushawishi na uungwaji mkono wa umma kwa lengo la kushinda uchaguzi, kushika na kuongoza dola kupitia sanduku la kura ni miongoni mwa haki zinazoelezwa na kulindwa na sheria hiyo.

Hata hivyo, haki hiyo ya kisheria imezuiwa tangu mwaka 2016 baada ya Serikali kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara ya kisiasa isipokuwa kwa madiwani na wabunge katika maeneo yao ya uwakilishi.

Tofauti na wenzao wa CCM, viongozi na wawakilishi wa vyama vya upinzani wamekuwa waathirika wakuu wa zuio hilo na mikutano yao imekuwa ikizuiwa na wakati mwingine vikao vyao vya ndani kuingiliwa kutokana na sababu zinazotajwa za “kiusalama na taarifa za kiintelijensia zinazoifikia jeshi la polisi”.

Mifano ni mingi lakini itoshe tu kutaja matukio machache, yakiwamo ya viongozi wakuu wa Chadema katika maeneo mbalimbali na la hivi karibuni la mkutano wa Zitto Kabwe-- mbunge Kigoma Mjini na kiongozi wa ACT-Wazalendo-- uliopangwa kufanyika Januari 17, 2020 lakini ukazuiwa na polisi.

Kupitia barua ya mkuu wa polisi wa Wilaya ya Kigoma yenye kumbukumbu namba KIG/A.24/60/VOL.1/114 ya Januari 16, 2020, Jeshi la Polisi mkoa wa Kigoma ilitaja sababu za kiusalama na taarifa za kiintelijensia kuzuia mkutano huo.

Siku ambayo mkutano huo ulizuiwa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alianza ziara ya siku tatu mkoani humo akitembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Kigoma mjini alikofanya vikao vya ndani na kuhutubia viongozi, wanachama na wananchi.

Katika ziara zake kwenye majimbo ya uchaguzi yanayoongozwa na wawakilishi kutoka vyama vya upinzani, Dk Bashiru alisikika akitamba kufunga na kutesti mitambo ya ushindi katika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Tukio lingine ni lile la Januari 26, 2020 ambapo Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alikamatwa na polisi Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kwa madai ya kufanya mkutano wa hadhara alipokuwa akifungua matawi ya chama hicho.

Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Handeni, William Nyero aliyezungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema Profesa Lipumba alikamatwa kwa tuhuma za kufanya mkutano wa nje kinyume cha maelekezo ya kufanya vikao vya ndani.

Kiongozi huyo wa upinzani aliyekuwa katika siku ya mwisho wa ziara yake ya siku saba mkoani Tanga aliachiwa baada ya kuhojiwa kwa saa mbili.

Wakati vyama viongozi wa upinzani wakikosa fursa ya kufanya siasa, wenzao wa CCM, hasa Dk Bashiru Ally na Humphrey Polepole, katibu wa Itikadi na Uenezi wamekuwa wanazunguka maeneo mengi nchini wakifanya vikao vya ndani na mingine katika viwanja vya michezo huku wakati mwingine wakipokewa kwa maandamano ya pikipiki na magari bila kizuizi.

Kitendo hicho siyo kinaibua tu tuhuma za upendeleo dhidi ya jeshi la polisi, bali pia inaonyesha rangi mbili za jeshi hilo kuhusu jinsi linavyosimamia matukio ya kisiasa.

Wakati wadau wa siasa wakihoji hali hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni imesisitiza kuwa zuio hilo liko palepale hadi muda muafaka utakapowadia.

“Muda wa siasa ukifika watu wataruhusiwa kuendesha mikutano mbalimbali yenye lengo la kueleza kwa wananchi walichokifanya kwa muda waliopewa nafasi baada ya kuchaguliwa na kuteuliwa katika nafasi mbalimbali,” Masauni alikaririwa akisema hayo akiwa ziarani Zanzibar.

Mnyika asema ni hofu

Akizungumzia zuio la shughuli za siasa, Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema hiyo ni dalili ya hofu na kutojiamini kwa viongozi wa CCM na Serikali yake.

“Wametuzuia kufanya mikutano ya hadhara kwa miaka minne, licha ya kuwa ni haki ya kikatiba na kisheria; hii ni dalili na kuthibitisha hofu na woga kwa vyama vya upinzani,” anasema Mnyika. Hata hivyo, Mnyika anasema zuio hilo limevifanya vyama vya upinzani kubuni mbinu mbadala ya kufanya siasa na hivyo kujiimarisha zaidi.

“Tumekuwa imara zaidi kuliko tulivyokuwa tukifanya maandamano na mikutano ya hadhara. Tuko tayari kwa uchaguzi na ushindi hata uchaguzi ukiitishwa sasa,” ametamba Mnyika ambaye ni mbunge wa Kibamba jijini Dar es Salaam.

Nini kifanyike

Katika mapendekezo yake, Mnyika anasema “Polisi waache kufanya kazi kwa ubaguzi, waanze kutenda haki kwa vyama vyote na makundi yote na watu. Haileti picha nzuri mikutano na shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani kuzuiwa huku CCM wakifanya mikutano ya hadhara nchi nzima kwa uhuru.”

Wakati Mnyika akisema hayo, Zitto alinukuliwa hivi karibuni akisema kwa miaka minne vyama vya upinzani vimelalamikia zuio hilo ikiwemo kufungua mashauri mahakamani bila mafanikio, hivyo sasa vimeamua kufanya siasa kwa mujibu wa sheria.

“Hata Wabunge tunapata wakati mgumu kufanya mikutano kwenye maeneo yetu ya uwakilishi...Sisi tutaanza mikutano yetu bila kujali zuio la Serikali mara baada ya mkutano mkuu wa chama Machi, 2020,” anasisitiza Zitto.Ukiacha msimamo huo wanasiasa, Majid Kangile, Wakili wa kujitegemea jijini Mwanza naye pia analitaka Jeshi la Polisi si tu kutenda haki, bali pia haki hiyo inatakiwa kuonekana ikitendeka bila ubaguzi.

“Polisi wasimamie misingi hiyo kuondoa madai ya vyama vya upinzani kutotendewa haki katika suala la shughuli za siasa,” anasema Kangile.

Wakili huyo anasema haki na usawa kwa wote ndiyo nguzo kuu ya amani na utulivu na kuomba pawepo utashi wa kisiasa, unaofuata na kuheshimu misingi ya sheria na haki kwa wote.

Misingi ya haki

Suala la haki linazungumzia pia na kiongozi wa dini, Mchungaji Godfrey Ongiri wa Kanisa la PEFA jijini Mwanza, ambaye anawataka viongozi wa Serikali na vyama vya siasa kukukumbuka, kusimamia, kuenzi na kutekeleza kwa vitendo misingi ya haki na usawa kwa wote bila kujali tofauti za kidini, kisiasa, kikabila wala maeneo.

Anasema moja ya misingi ya iliyoasisiwa, kulindwa na kusimamiwa kwa nguvu na Serikali zote tangu awamu ya kwanza, ni haki na usawa kwa wote ambayo ilikuwa moja ya ahadi 10 za mwana Tanu, chama ambacho kiliungana na ASP ya Zanzibar kuzaa CCM Februari 5, 1977.

“Ahadi muhimu nyingine inayotakiwa kuzingatiwa na viongozi wote bila kujali itikadi zao ni ile inayosema, “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.” Bila kunyooshea kidole kwa kundi lolote, mchungaji Ongiri anasema viongozi wote nchini wanatakiwa kujua kuwa vyeo vyao ni dhamana na wanapaswa kuvitumia kwa hekima na hofu ya Mungu kwa faida na maslahi ya Taifa.

Anasema matumizi sahihi na ya haki ya madaraka pia inapatikana katika ahadi ya mwana Tanu inayosema; “Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu; na nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko,” hoja ambazo zinaonekana kutozingatiwa ipasavyo katika usimamizi wa zuio la mikutano ya vyama vya siasa.