Zungu akosa mpinzani…

Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
Uchaguzi wa Naibu Spika wa Bunge utafanyika kesho Ijumaa Februari 11, 2022 ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee ndicho kimeteua mgombea wa nafasi hiyo ambaye ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu.
Dodoma. Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu ambaye amepitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Bunge kesho atapigia kura za ndio au hapana.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 10, 2022 na Idara ya Habari ya Bunge ambayo imesainiwa na na Katibu wa Bunge Nenelwa Mwihambi, inaonyesha hakuna chama kingine cha siasa chenye uwakilishi bungeni ambacho kilipeleka jina la mgombea.
Ratiba iliyotolewa na Ofisi hiyo ilionyesha kuwa leo saa 10 jioni ilikuwa mwisho kwa vyama vya siasa kupeleka majina ya wagombea wao.
Kanuni za Bunge zinataka Naibu Spika atokane na mbunge aliyeko bungeni ambapo Bunge la 12 vyama vyenye wabunge ni CCM, Chadema, CUF na ACT Wazalendo.
Uchaguzi huo utakaofanyika kesho unakuja kutokana na aliyekuwa Naibu Spika, Dk Tulia Akson kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge hilo kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Job Ndugai aliyejiuzulu Januari 6 mwaka huu.
Wabunge wengi wanatokana na CCM, ambao ndani ya chama chao walishampitisha Zungu, hivyo kazi ya kesho ni kama kwenda kumthibitisha.
Zungu ambaye alipitishwa na wabunge wote wa CCM kukiwakilisha chama hicho, amekuwa Mwenyekiti wa Bunge tangu Bunge la 10 akimsaidia aliyekuwa Spika wa wakati huo Anne Makinda na ameendelea na nafasi hiyo hadi sasa.