Sababu 10 za kukosa mayai kwa kuku wanaotaga-2
Muktasari:
Hii ni baada ya kuangalia sababu nne kwenye makala yaliyopita na sasa tuangalie sababu sita zilizobaki.
Makala haya ni mwendelezo wa kuangalia sababu 10 zinazosababisha kukosa mayai kutoka kwa kuku wanaotaga.
Hii ni baada ya kuangalia sababu nne kwenye makala yaliyopita na sasa tuangalie sababu sita zilizobaki.
Tukumbushane sababu nne zilizopita ambazo ni mabadiliko ya hali ya hewa kama vile baridi, giza, mvua na joto kali; umri wa kuku na mabadiliko ya mwili kutokana na hatua za ukuaji.
Sababu ya tatu ni chakula kinachotolewa kwa kuku kuwa duni au hakitoshi mahitaji ya mwili na kuzalisha. Sababu ya nne ni kukosa maji kwa muda mrefu na kusababisha mwili kuwa na mshituko mkubwa.
Makala hii ya leo itaendelea na sababu sita zilizobaki tukianza na sababu ya tano ambayo ni kubanana kwa kuku bandani. Kwa kawaida kuku wanahitaji nafasi ya kutosha kutembea kupata chakula na maji.
Kuku wakibanana bandani hushindwa kula na kunywa maji vizuri na matokeo yake hushindwa kushiba.
Kwa kawaida kuku mwenye umri wa kutaga, anatakiwa kula chakula gramu 120 hadi 140 kwa siku na eneo la kuishi linatakiwa kuwa mita moja ya mraba kukaa wastani wa kuku watano hadi sita kwa kuku wa mayai na kuku nane wa nyama.
Idadi kubwa ikiwekwa zaidi ya kiasi kinachotakiwa, kuku watachafua banda, kumwaga maji na kushindwa kukua vizuri na kushindwa kuzalisha.
Sababu ya sita ni uchafu. Banda la kuku linatakiwa kuwa safi bila harufu mbaya ya uozo au madawa yoyote. Kuku wanaokaa kwenye banda chafu hushambuliwa na magonjwa kutokana na kula uchafu ulioko kwenye sakafu au kunywa maji machafu.
Hali ya banda inatakiwa kuwa kavu na mbolea isigande au kuwa na unyevunyevu kama zizi la ng’ombe. Hali kama hiyo husababisha magonjwa mengi kwa kuku na kushindwa kutaga vizuri kama ni kuku wa mayai, kuhalisha na kudumaa kwa kuku wa nyama.
Sababu ya saba ni wadudu wanaoishi ndani au nje ya ngozi ya kuku kama vile minyoo, chawa, viroboto, kupe na utitiri. Wadudu hawa hufyonza damu kwenye ngozi ya kuku na kusababisha kuku wasitulie kwa kuwashwa. Muda mwingi kuku hutumia kuhangaika, matokeo yake uzalishaji hushuka kwa kushindwa kula vizuri, kutulia na kutaga.
Minyoo wa tumboni hutumia chakula kilekile ambacho kuku anahitaji kwa ajili ya mwili na kuzalisha mayai. Kuku wenye matatizo haya hudhoofika hata kama wanapewa chakula na dawa za kutibu.
Mfugaji anatakiwa kufuatilia na kujua tatizo kabla ya kuanza matibabu ili atumie dawa sahihi. Dawa za minyoo ni tofauti na dawa za wadudu wa nje kama vile utitiri, chawa kupe na viroboto. Minyoo huonekana kwenye kinyesi cha kuku. Kuku wenye utitiri, chawa, kupe na viroboto, wadudu hao huonekana kwenye ngozi.
Sababu ya nane ni vimelea. Mabanda mengi yanayofungwa kwa muda mrefu hutengeneza ngome ya vimelea vya magonjwa kuzaliana. Mara nyingi mfugaji utakuta anatibu ugonjwa huu, lakini punde ugonjwa mwingine tena unatokea.
Hii ni kutokana na sehemu hiyo kuwa na hifadhi kubwa ya vimelea. Mfugaji anatakiwa kufanya usafi wa kina kukusanya uchafu wote na kuchoma moto mabaki yote ya kuku waliopita.
Aoshe kuta na sakafu za banda baada ya kutoa mbolea na kupeleka shambani. Usihifadhi mbolea ya kuku jirani na banda la kuku unakofugia, kwani vimelea kutoka kwenye mbolea wataingia tena kwenye banda la kuku. Kinga bora dhidi ya magonjwa ni usafi wala sio chanjo au tiba. Chanjo na tiba zipo baada ya usafi kuzidiwa nguvu.
Sababu ya tisa ni wezi. Wezi sio ugonjwa wa hali ya hewa lakini ni sehemu ya kupunguza uzalishaji. Kama unamfanya kazi anayeiba mayai au kuku, madhara yake ni sawa na vifo vya kuku.
Mfugaji unashauriwa kuwa na mbinu thabiti kudhibiti wizi kwenye mabanda yako. Tengeneza mfumo wa kutunza kumbukumbu kila siku ujue idadi ya kuku au mayai kwa maandishi. Kuwa rafiki wa mhudumu wa banda kupanga na kutatua changamoto zote kwa pamoja.
Sababu ya tisa ni wanyama waharibifu. Kuna wanyama wanaopenda kula kuku au chakula cha kuku. Wanyama kama vile kenge, vichehe, nyoka, panya, paka na wengineo ni hatari kwa kuku na mayai. Tengeneza banda lenye uwezo wa kuwadhibiti.
Wanyama hawa pia husambaza magonjwa kwa kuku. Ni rahisi kuona unaokota mayai machache, lakini kila ukichunguza huoni sababu yoyote ya kupata mayai kidogo kumbe kuna panya, kenge, nyoka au paka wanaokula mayai kabla hujayaokota bandani.
Fanya uchunguzi kila mahali na tumia mitego safi kuwaua ili upunguze gharama za kupoteza kukua au mayai.
Sababu ya 10 ni kutojali na haraka ya kutaka kuona mambo makubwa kwa wakati mfupi kuliko uhalisia. Wafugaji wengi hukimbilia kutaka faida bila kuitafuta; matokeo yake huona wanachelewa na hata kutelekeza mradi.
Katika biashara zote ikiwamo ufugaji, faida ni matokeo ya kazi na hatua fulani. Wafugaji wengi huanza vizuri kwa huduma nzuri kwa kuku wao, ikifika sehemu wakaona kuku wanachelewa kutaga huamua kuwauza ghafla.
Maamuzi ya haraka bila kupata ushauri wa kitaalamu kwenye biashara yoyote ni kununua hasara kwa gharama yako mwenyewe.
Kabla hujaanza ufugaji, chukua hatua kujifunza kila kitu ili upate upeo wa kutosha na kuzingatia mambo yote muhimu.