Abaya, vazi linalozidi kupata umaarufu

Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani mavazi marefu yenye stara na heshima ndiyo hupewa kipaumbele zaidi.

Uvaaji wa mavazi haya huwa si kwa Waislamu pekee, bali hata kwa watu wa dini nyingine wanaowaunga mkono marafiki zao wa dini hiyo.

Wengine hufanya hivyo kwa kupenda kuvaa mavazi yao kutokana na wakati au tukio lililopo katika muda husika.

Katika kipindi hiki mavazi kama baibui, madera ya aina mbalimbali, magauni marefu na nguo nyingine za stara huvaliwa na wanawake wengi hata wale wasiokuwa Waislamu.

Katika kipindi hiki cha mwisho cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kuelekea maandalizi ya Sikukuu ya Eid el Fitri, moja kati ya vazi lililojizolea umaarufu ni abaya na kusababisha kutengenezewa misemo mbalimbali katika mitandao ya kijamii.

Vazi hilo siyo jipya, limekuwepo katika miaka mingi iliyopita, lakini limekuwa likiboreshwa kila kukicha kwa kuliweka katika mitindo mbalimbali na kuliwekea nakshi, jambo linalofanya watu kuendelea kuvaa vazi hilo, hasa kwa wale wanaopenda stara.

Mwajuma Suleiman anasema anapendelea kuvaa abaya kwa kuwa ni vazi linalomfanya kuwa huru kufanya shughuli zake huku akiwa katika stara.

“Unapovaa vazi hili pia inakupa hadhi fulani kwa kuwa kama inavyojulikana bei yake imechangamka kulivaa inatakiwa ujipange,” alichombeza Sakina.

Akizungumza na Mwananchi, muuzaji wa abaya kutoka Manzese jijini Dar es Salaam, Sakina Ibrahim anasema abaya ni vazi jeusi au rangi yoyote ya kung’aa linalofanana na baibui, linalo valiwa juu ya nguo ambalo asili yake ni nchi za Uarabuni kama vile Dubai, Oman, Saudia na nchi za Uturuki, Indonesia, India, Pakistan na nyinginezo.

“Kutokana na asili ya vazi hilo kuwa nchi za Uarabuni, watu kutoka katika baadhi ya mataifa walilichukulia kama ni kwa ajili ya Waarabu na na Waislamu,” anasema.

Anasema kutokana na ukuaji wa utandawazi ambao umefanya dunia kuwa kama kijiji, imefanya vazi hilo kuenea katika maeneo mbalimbali na kupendwa na wengi, hasa wale wanaopenda mavazi ya stara.

Anasema tofauti kidogo na baibui, abaya gharama yake ni kubwa kidogo huanzia kati ya Sh100, 000 hadi Sh250,000 kutegemea nchi ilipotoka.

Mfanyabiashara mwingine, Fatma Hamidu maarufu kama Fatuma Collection anasema katika kipindi cha Ramadhani na sikukuu ya Eid hupata wateja wengi kulinganisha na miezi mingine.

Anasema changamoto kubwa anayokumbana nayo huwa ni wateja wake kulalamikia kuwa vazi hilo gharama yake ni kubwa.

“Bei za abaya hutegemea nchi ambayo mtu amenunua, hivyo ni moja kati ya vazi ambalo lina gharama kidogo.”

Jackson Kibanda, ambaye ni muuzaji wa mabaibui na abaya za mtumba katika eneo la Kariakoo, anasema kipindi hiki amekuwa akipata wateja wengi ikilinganishwa na awali.

Anasema pengine inasababishwa na mabaibui na abaya hizo za mtumba kuwa gharama nafuu ukilinganisha na zile za dukani.

"Abaya na baibui za mitumba mimi ninaziuza kati ya Sh 25,000 hadi 45,000 kwa zile ambazo zimetokana na mtumba daraja la kwanza," anasema.