Usile vyakula hivi kwa wakati mmoja
Matumizi ya aina mbalimbali za vyakula hapa nchini limekuwa ni jambo la kawaida bila kujali madhara yanayoweza kujitokeza.
Hapa nchini, hasa katika migahawa hupikwa vyakula vya aina tofauti tofauti, huku vikichanganywa pamoja bila kujua mchanganyiko wa baadhi ya vyakula huweza kuleta changamoto katika mwili wa binadamu.
Mwandishi wa makala hii ameangalia vyakula ambavyo huwa vikichanganywa pamoja huweza kuleta madhara katika mwili wa mwanadamu.
Tovuti ya india.com, inabainisha kuna vyakula vikichanganywa huleta madhara katika mwili wa binadamu na haishauriwi kutumiwa kwa wakati mmoja.
Mayai na nyama ya nguruwe kitaalamu hivi haviruhusiwi kutumika kwa wakati mmoja, kwa kuwa atakayetumia kwa kula basi anaweza kupata changamoto ya kiafya.
Vyakula hivi viwili vina protini nyingi na huwa vizito katika tumbo, hivyo itachukua muda mrefu kusaga vyakula vyote viwili.
Hata hivyo, matumizi ya sharubati itokanayo na machungwa pamoja na matumizi ya maziwa havitakiwi kutumika kwa pamoja kwa kuwa huchukua muda kumeng’enywa mwilini.
Unapotumia maziwa na machungwa, maziwa huganda na kusababisha gesi tumboni.
Chakula cha jibini na kinywaji baridi, muunganiko huu huleta madhara katika mwili wa binadamu kwa kuwa mchanganyiko unaweza kusababisha maumivu ya tumbo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Health, vyakula kama ndizi na maziwa, nyama na viazi vinaweza kuleta changamoto endapo vikitumiwa kwa wakati mmoja.
Mfano matumizi ya viazi na nyama kwa wakati mmoja huweza kusababisha matatizo ya umeng’enyaji chakula au matatizo ya tumbo.
Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa Lishe, Sweetbert Njuu anasema nyama na maziwa havitakiwi kutumiwa pamoja kwa kuwa mtu hataweza kupata faida vyote vikitumika pamoja.
“Vyakula hivi vinashauriwa angalau vipishane saa moja endapo mtu atatumia, kwa sababu madini ya chuma na madini ya kalsiamu yanakinzana,” anasema Njuu
Anasema matumizi ya pombe husababisha ufanisi mbaya wa ufyonzaji wa chakula mwilini, hivyo pombe haishauriwi kutumiwa endapo mtu anakula chakula.
“Ikiwa mtu amekunywa pombe nyingi sana na wakati huohuo amekula chakula chenye sifa ya mlo kamili, basi uwezekano wa ufyonzaji chakula unaweza kufika asilimia 50,” anasema Njuu.
Hata hivyo, matumizi ya matunda na nafaka zisizokobolewa kwa wakati mmoja kitaalamu huweza kusababisha baadhi ya changamoto katika tumbo, mfano tumbo kujaa gesi.
Sweetbert Njuu anasema watu wanatakiwa kuzingatia matumizi ya lishe bora ambayo, huwa na mbogamboga, matunda, nafaka zisizokobolewa, vyakula vitokanayo na mizizi, matumizi ya protini nzuri yaani nyama zisizo na mafuta na bila kusahau kunywa maji ya kutosha.