Kukithiri udumavu Afrika kwawaibua wadau

Muktasari:
- Lengo la makubaliano hayo ni kusaidia kupunguza hali ya udumavu katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Arusha. Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA), na Mtandao wa Asasi za Kiraia zinazohusika na masuala ya lishe ( ESA SUN CSN), wamesaini mkataba wa miaka mitano wenye lengo la kupunguza changamoto zinazosababishwa na ukosefu wa lishe.
Mkataba huo umesainiwa leo Jumanne Julai Mosi, 2025 katika makao makuu ya ESCA, jijini Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa ECSA, Dk Ntuli Kapologwe amesema wameingia makubaliano hayo kutokana na nchi nyingi za ukanda huo kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu.
"Ni muhimu tushirikiane kuondoa ukosefu wa lishe sababu kama katika nchi zote 15 zina tatizo la lishe kati ya asilimia 30 hadi 40, ukondefu ukiwa asilimia 30 na upungufu mkubwa wa damu miongoni mwa watoto wa kike ukiwa zaidi ya asilimia 30," amesema.
Mkurugenzi huyo ametolea mfano Tanzania ambayo ilianzisha mkataba wa lishe ambao ni moja ya afua itakayoenezwa katika nchi zingine za ukanda huo ili afua za lishe zitekelezwe.
Amesema baada ya kusaini mkataba huo wa makubaliano watashirikiana kupambana na changamoto za lishe.
"Ukiangalia Tanzania mwaka 2018 walianzisha mkataba wa lishe na ulikuwa ukisimamiwa na Rais kushirikisha wakuu wa mikoa, tunaamini utatusaidia kujifunza wote kama nchi wanachama."
"Ukosefu wa lishe unasababisha madhara makubwa kiafya ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza kama sukari, shinikizo la damu na mengine hivyo tutaweka mkazo kukabiliana na tatizo hilo," amesema.
Mwenyekiti wa Mtandao wa asasi hizo, Edgar Onyango amesema mkataba huo utasaidia kuungana kukabiliana na tatizo la lishe na kuwa mbali na mkataba huo wataanzisha chuo kwa ajili ya masuala ya lishe ambapo pia watashirikiana na jamii, ili kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na ukosefu wa lishe.
Amesema utekelezaji wa mkataba huo unaanza mara moja baada ya kusaini na kila baada ya miezi sita watakuwa wanatoa taarifa za utekelezaji wake.
"Tumekubaliana na tumezungumza mengi na miongoni mwa afua za mkataba huo ni kutolewa taarifa ya maendeleo ya utekelezaji kila baada ya miezi sita pamoja na kuboresha lishe kwa kuweka virutubisho shuleni, pamoja na kumtathmini mtoto kwa siku 1,000 za awali tangu kuzaliwa.”
" Tunaamini kupitia mkataba huu tutamaliza utapiamlo wote ifikapo mwaka 2030 na takwimu zimetuonyesha kuwa bado utapiamlo ndani ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini upo," amesema.