Sababu waishio mijini wanatajwa kuwa hatarini kwa shinikizo la damu
Muktasari:
- Vitu vinavyoongeza hatari ya shinikizo la juu la damu ni kutofanya mazoezi, unene kupita kiasi, kula chumvi nyingi, kuvuta sigara, pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.
Dar es Salaam. Wakati kesho, Mei 17, dunia ikiadhimisha ugonjwa wa shinikizo la juu la damu (World Hypertension Day 2026) kwa ajili ya kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo, imetajwa kuwa waishio mijini wako hatarini zaidi kuliko wanaoishi maeneo ya vijijini, kulingana na mtindo wa maisha.
Kitaalamu, hypertension ni ugonjwa wa shinikizo la damu kuwa juu kuliko kiwango cha kawaida kwa muda mrefu (presha ya juu). Shinikizo la damu ni nguvu ambayo damu hutumia kusukumwa kwenye mishipa ya damu na moyo.
Kwa kawaida, kipimo cha presha huwa: kawaida chini ya 120/80 mmHg, lakini hypertension ni 140/90 mmHg au zaidi (kwa vipimo vinavyorudiwa mara kadhaa).
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu bilioni 1.4 duniani wanaishi na shinikizo la damu, huku karibu asilimia 44 ya wagonjwa hao wakiwa hawajui kama wana tatizo hilo. Aidha, ni asilimia 23 pekee duniani wenye uwezo wa kudhibiti presha yao ipasavyo.
Kitaalamu, shinikizo la juu la damu hutokea pale mwili unapopata hali zinazofanya mishipa ya damu kuwa myembamba au moyo kusukuma damu kwa nguvu zaidi, hivyo presha hupanda.
Sababu kuu ni mishipa ya damu kubana kutokana na mafuta, chumvi nyingi na magonjwa mengine, ambayo yanaweza kufanya mishipa iwe myembamba au migumu. Hali hiyo huifanya damu ipite kwa shida, hivyo presha huongezeka.
Aidha, moyo kufanya kazi kupita kiasi pale mwili unapokuwa na uzito mkubwa, msongo wa mawazo au matumizi mengi ya chumvi, hulazimisha moyo kusukuma damu kwa nguvu zaidi.
Akifanya mahojiano na Mwananchi Digital, leo, Mei 16, 2026 Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk Davis Ngarashi, amesema aina ya maisha wanayoishi watu wa mjini, ikiwemo unywaji wa pombe uliopitiliza, matumizi ya shisha na vyakula vya “fast food”, vinasababisha changamoto hii.
“Unapokula chakula kama chipsi mayai au wanga, unaingiza mafuta mwilini. Na mjini watu hatufanyi kazi za kuchosha, unakuta unatengeneza mafuta kwenye mishipa ya damu.
“Hali hiyo inafanya mshipa wa damu kuwa mwembamba na mgumu kutanuka. Kingine, hapa mjini mawazo ni mengi kulingana na maisha kuhitaji vitu vingi, ikiwemo ada za watoto, michango mbalimbali ya harusi, bado na kumudu maisha ya kila siku.
Kutokana na hali hiyo, kwenye mwili kuna mfumo wa ‘sympathetic’ unapanda na mara nyingi unasababisha mirija ya damu kusinyaa,” amesema.
Dk Ngarashi amesema hata hali ya kupitiliza ya kuongeza chumvi ambayo haijapikwa katika vyakula ni sababu ya presha kupanda.
Hata hivyo, kwa mujibu wa WHO, katika miji mingi watu hutumia muda mwingi wakiwa wamekaa ofisini, kwenye magari au wakitumia simu/kompyuta. Kutofanya mazoezi ya kutosha kunatajwa kuwa sababu kubwa ya kuongezeka kwa uzito wa mwili na hatimaye presha.
Mbali na hilo, ulaji wa vyakula vya haraka vyenye chumvi nyingi, mafuta na sukari umekuwa sehemu ya kawaida ya maisha ya mjini.
Taarifa za WHO zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 55 ya watu duniani wanaishi mijini, na idadi hiyo inatarajiwa kufikia asilimia 68 ifikapo mwaka 2050.
Uchafuzi wa hewa nao umeendelea kuwa sababu nyingine inayochangia magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo shinikizo la damu. Moshi wa magari, viwanda na mazingira yenye msongamano mkubwa huongeza madhara kwa moyo na mishipa ya damu.
Dk Daud Emmanuel naye amesema mtindo wa maisha ya mjini, hasa aina ya vyakula na kutofanya mazoezi, pia husababisha mafuta kujilimbikiza katika mishipa ya damu, tofauti na waishio vijijini ambao hutembea umbali mrefu na kula vyakula vya asili.
Vijijini
Ingawa wananchi wa vijijini nao wanaweza kupata shinikizo la damu, wataalamu wanaona mazingira yao bado yana faida kadhaa za kiafya. Watu wengi vijijini hutembea zaidi, hushiriki shughuli za kilimo au kazi zinazohusisha kutumia nguvu za mwili, jambo linalosaidia mwili kufanya kazi vizuri.
Aidha, ulaji wa vyakula vya asili kama mboga za majani, nafaka zisizokobolewa na matunda huwa mkubwa zaidi ukilinganisha na vyakula vya viwandani vinavyopatikana kwa urahisi mijini.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa tofauti hiyo inaanza kupungua kutokana na kasi ya mabadiliko ya maisha hata katika maeneo ya vijijini, ambapo matumizi ya vyakula vya kusindikwa yanaongezeka kila mwaka.