Saratani ya macho hatari kwa watoto, Serikali yasisitiza uchunguzi wa mapema
Mwakilishi wa mganga mkuu wa serikali, Dk Eliudi Eliakim wa tatu kulia) akizungumza na wazazi wenye watoto wenye changamoto za macho katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma leo Mei 15, 2026
Muktasari:
- Serikali imeeleza kuwa ongezeko la watoto wanaogundulika na saratani ya macho nchini linatokana na uelewa mdogo wa jamii na kuchelewa kwa wazazi kuwapeleka watoto hospitali baada ya kuona dalili za awali.
Dodoma. Serikali imewataka wazazi na walezi kuwahi kuwapeleka watoto hospitalini mara wanapoona dalili zisizo za kawaida kwenye macho yao ili kusaidia kugundua mapema saratani ya macho, maarufu retinoblastoma, ugonjwa ambao wataalamu wanasema unatibika endapo utabainika mapema.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, leo Ijumaa, Mei 15, 2026, jijini Dodoma katika maadhimisho ya wiki ya kuelimisha jamii kuhusu saratani ya macho kwa watoto, Dk Eliudi Eliakimu amesema ingawa ugonjwa huo hauonekani mara nyingi, bado ni miongoni mwa saratani zinazochangia vifo vya watoto barani Afrika kutokana na kuchelewa kugundulika.
Amesema takwimu za dunia zinaonesha kuwa kati ya watoto 16,000 hadi 18,000 wanaozaliwa hai, mmoja hupatikana na saratani ya macho, huku ugonjwa huo ukichangia asilimia tatu ya saratani zote za watoto duniani.
Kwa Afrika, amesema saratani hiyo huchangia kati ya asilimia 10 hadi 15 ya saratani zote za watoto, huku wavulana na wasichana wakiathirika kwa kiwango sawa.
Mwakilishi wa mganga mkuu wa serikali Dk Eliudi Eliakim (mwenye shati jeupe) akizungumza na wazazi wenye watoto wenye changamoto ya macho katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma leo Mei 15, 2026
“Pamoja na kwamba saratani hii haitokei mara nyingi, inaweza kutibika ikiwa mtoto atagundulika mapema, na endapo atacheleweshwa inaweza kuathiri macho yote na kusababisha madhara, ikiwemo kifo,” amesema Dk Eliakimu.
Kwa mujibu wa takwimu za huduma za afya nchini, wagonjwa 902 wa saratani ya macho walionwa katika vituo vya kutolea huduma za afya mwaka 2025, idadi ambayo ni zaidi ya mara tano ya wagonjwa 184 waliobainika mwaka 2024 katika hospitali za rufaa na ngazi za msingi.
Dk Eliakimu amesema tafiti zinaonesha kuwa katika nchi nyingi za Afrika ni asilimia 20 hadi 48 tu ya watoto wanaogundulika na saratani hiyo wanaoweza kuishi kwa zaidi ya miaka mitano baada ya kubainika kuwa na ugonjwa huo.
Amesema sababu kubwa inayochangia vifo hivyo ni kuchelewa kwa wazazi kuwapeleka watoto hospitalini, hali inayosababisha ugonjwa kufikia hatua za juu kabla ya kuanza matibabu.
“Utafiti uliofanyika Tanzania umeonyesha kuwa wazazi wengi huchelewa kuwapeleka watoto kwenye vituo vya afya kwa takribani miezi 10 tangu walipoanza kuona dalili za awali. Chanzo kikubwa ni uelewa mdogo kuhusu saratani hii,” amesema.
Amefafanua kuwa saratani hiyo husababishwa na mabadiliko ya vinasaba yanayoweza kutokea wakati wa ujauzito au kurithiwa kutoka kwa wazazi. Kwa mujibu wa takwimu, asilimia sita ya wagonjwa hurithi tatizo hilo, huku asilimia 94 ikitokana na mabadiliko ya vinasaba wakati mimba inakua.
Amesema saratani hiyo inaweza kuathiri jicho moja au yote na asilimia 25 hadi 35 ya wagonjwa huathirika macho yote mawili.
“Wale wanaopata saratani ya kurithi mara nyingi huathirika macho yote mawili na asilimia 50 ya watu hao wanaweza kurithisha tatizo hilo kwa watoto wao,” amesema.
Akitaja dalili za ugonjwa huo, Dk Eliakimu amesema wazazi wanapaswa kuwa makini wanapoona sehemu nyeusi ya jicho la mtoto kuwa nyeupe, jicho kuwa jekundu kupita kawaida, mtoto kuwa na kengeza, jicho kutokeza nje, kuvimba, kutoa usaha au damu pamoja na maumivu ya macho.
“Napenda kuwakumbusha wananchi kuwa wanapoona dalili hizi, wamuwahishe mtoto kwenye kituo cha kutolea huduma ili wataalamu waweze kubaini kama ni saratani au tatizo lingine la macho,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Hamad Nyembea, amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) linaelekeza kila watu milioni 10 kuwepo na hospitali ya rufaa inayotoa huduma za kibingwa bobezi za macho kwa watoto.
Amesema huduma hizo zinahitaji uwekezaji mkubwa kutokana na mahitaji ya wataalamu maalumu, vifaa tiba na mazingira rafiki kwa watoto.
“Serikali imeendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha huduma za kibingwa bobezi za macho kwa watoto zinapatikana katika hospitali mbalimbali nchini,” amesema Nyembea.
Ameeleza kuwa huduma hizo zilianza rasmi mwaka 2005 katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro, kabla ya kuanzishwa katika Hospitali ya CCBRT Dar es Salaam mwaka 2006 na Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2008.
Kwa mujibu wa Nyembea, kuanzia mwaka 2024 huduma hizo zimeanza pia kutolewa katika Hospitali za Rufaa za Mbeya na Benjamin Mkapa, na kufanya hospitali zinazotoa huduma hizo kufikia tano kati ya saba zilizopangwa nchini.
“Hadi sasa Tanzania ina madaktari bingwa bobezi wa macho 12 waliopo Muhimbili, KCMC, Bugando, Benjamin Mkapa, Mbeya na CCBRT,” amesema.
Takwimu za wizara zinaonesha kuwa mwaka 2025 watoto 205,026 walihudumiwa katika kliniki za macho kwenye hospitali za rufaa za mikoa na ngazi za msingi, ambapo asilimia 22 walikuwa chini ya miaka mitano.
Magonjwa yaliyoongoza ni mzio wa macho, uoni hafifu unaorekebishika kwa miwani, maambukizi ya macho pamoja na majeraha ya macho.
Katika kliniki za kawaida za msingi, watoto milioni 2.5 walio chini ya miaka mitano walihudumiwa, huku watoto 290,960 wakibainika kuwa na matatizo ya macho.
Baadhi ya wadau wa macho wakiwa kwenye maadhimisho ya wiki ya elimu kuhusu saratani ya macho kwa watoto Jijini Dodoma leo Mei 15, 2026.
Naye Judith Mollel, mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake amewahi kuugua saratani ya macho, amesema uelewa mdogo wa jamii kuhusu dalili za ugonjwa huo bado ni changamoto kubwa.
Amesema mtoto wake aligundulika akiwa na miezi tisa na kulazimika kuondolewa jicho moja ili kuzuia saratani isisambae kwenye jicho la pili.
“Nilikuwa naona jicho la mwanangu lina mng’ao usio wa kawaida. Nilipompeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili ndipo nikaambiwa ana saratani ya jicho na ilibidi afanyiwe upasuaji haraka. Kama mzazi nilihuzunika sana lakini ilikuwa lazima ili kuokoa maisha yake,” amesema Judith.
Ameiomba Serikali kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu dalili za saratani ya macho kwa watoto pamoja na kuingiza huduma za uchunguzi wa macho kwenye kadi za kliniki za watoto ili wagonjwa waweze kubainika mapema na kupata matibabu kabla hali haijawa mbaya.