Usafi wa kinywa utakuepusha kutoboka kwa meno

Muktasari:
Kutoboka kwa jino ni hali ya kuwa na tundu linaloweza kuwa kubwa au dogo. Wakati mwingine meno kadhaa huwa na matundu ambayo ni matokeo ya sababu mbalimbali ikiwamo bakteria wa kinywa, ulaji wa vyakula vyenye sukari na kutosafisha kinywa vizuri.
Bila shaka umewahi kumuona mtu mwenye matundu kwenye meno.
Kutoboka kwa jino ni hali ya kuwa na tundu linaloweza kuwa kubwa au dogo. Wakati mwingine meno kadhaa huwa na matundu ambayo ni matokeo ya sababu mbalimbali ikiwamo bakteria wa kinywa, ulaji wa vyakula vyenye sukari na kutosafisha kinywa vizuri.
Kutoboka kwa meno ni moja ya matatizo yanayoenea zaidi duniani yakiathiri karibu kila mtu, watoto wadogo wakiwamo. Hii ni kwa kuwa kila mtu mwenye meno yumo kwenye uwezekano wa kupata matundu kutokana na sababu tofauti.
Matundu haya yasipotibiwa mapema huweza kuathiri matabaka ya jino na kusababisha maumivu makali ambayo yakizidi mgonjwa huweza kuling’oa endapo jitihada za kulitibu zitashindwa kufanikiwa.
Pamoja na hayo kumuona daktari wa kinywa mara kwa mara, usafishaji mzuri wa meno na mazoea ya kufanya flosi ni njia za kuzuia meno kutoboka na kuoza.
Dalili
Ukweli ni kwamba dalili za meno yaliyotoboka hutofautiana kulingana na kiwango cha utobokaji wa jino husika. Wakati tundu linapoanza, inawezekana kabisa usiwe na dalili yeyote ile.
Lakini kadri tundu linavyoongezeka na kwenda ndani zaidi mgonjwa anaweza kuona tundu kwenye jino husika kwa kujiangalia. Uwapo wa rangi ya kahawia, nyeusi au doa jeupe zaidi kwenye jino nayo ni dalili nyingine.
Wakati mwingine jino linaweza likawa linauma upepo ukiingia kinywani au baada ya kula ama kunywa kitu kitamu, cha moto au baridi. Maumivu unapotafuna kitu pia.
Unaweza ukawa hujui kama una matundu kinywani mwako hivyo ni muhimu kuwa na ratiba ya kumtembelea daktari wa kinywa na meno mara kwa mara kwa uchunguzi na ushauri hata kama afya ya kinywa chako iko sawa.
Unapokua na dalili tajwa hapo juu ni vizuri kumuona daktari haraka zaidi kwa msaada kabla madhara yake hayajawa makubwa zaidi.
Jinsi jino linavyotoboka
Matundu kwenye meno ni matokeo ya kuoza kwa jino na huchukua muda kwa kuwa si lazima likaendelea kila linapoanza. Linaweza likaanza kisha likasimama na kuendelea tena baadae.
Jino hutoboka baada ya tabaka laini kushambuliwa na bakteria waliomo kinywani. Kiasili kinywa chako kina aina mbalimbali za bakteria ambapo baadhi yao huishi kwa kutegemea aina fulani ya sukari unazotumia kwenye mahitaji yako ya kila siku.
Inapotokea sukari hii haisafishwi kutoka kwenye meno, bakteria hawa huitumia kama chakula chao na kisha kuzalisha tindikali na kujikusanya pamoja kufanya tabaka laini jeupe ambalo hujishika kwenye meno karibu na ufizi.
Kama tabaka hili halitaondolewa mapema, hukomaa na haiwezekani kuondoa kwa mswaki mpaka uende hospitali, hili huwa ni eneo zuri kwa bakteria kujificha huku wakiendelea kuliozesha jino kabla ya kulitoboa.
Kuna hatua kadhaa za kutoboka kwa tabaka laini. Katika hatua ya kwanza, tindikali izalishwayo na tabaka laini taratibu huondoa madini kwenye tabaka la nje la meno. Kuondoka kwa madini hayo husababisha kutokea kwa vitundu vidogo kwenye tabaka hili.
Mara tabaka hili la nje linapotoboka, bakteria pamoja na tindikali huweza kufika kwa urahisi kwenye tabaka la kati ambalo kiasili ni laini kuliko la nje na halina uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi ya tindikali
Kadri jino linavyoendelea kutoboka, ndivyo tindikali na bakteria wanakwenda ndani zaidi na kufikia tabaka la ndani linalobeba mishipa ya fahamu na ya damu ya jino husika.
Kutoboka na kuoza kwa meno kunapofika kwenye tabaka hili, mgonjwa huhisi dalili mara moja. Inaweza kuwa maumivu makali ya mishipa ya jino au wakati wa kutafuna kitu au dalili nyingine.
Madhara
Kuoza kisha kutoboka kwa meno ni jambo la kawaida kiasi kwamba wengi hawalipi uzito unaostahili. Wengine hupuuza hata mtoto mdogo anapopata matundu kwenye meno hasa yale ya utotoni.
Hata hivyo, yapo madhara makubwa yanayoweza kuleta uharibifu wa kudumu hata kwa watoto ambao hawana meno ya ukubwani.
Mgonjwa anaweza kupata maumivu makali yanayotokana na kupata jipu kwenye fizi na kutunga usaha.
Usaha katika kinywa au jirani na jino unaweza kuonekana baada ya kuminya ufizi au jino husika kuvunjika.
Endapo meno yataendelea kutoboka bila hatua za haraka kuchukuliwa, maumivu makali yanayoweza kujitokeza huenda yakaingilia kazi za kila siku za mgonjwa hivyo kumzuia kwenda shambani, shuleni au kwenye biashara zake.
Inaweza ikasababisha kung’olewa kwa jino husika hali inayoweza kuathiri kujiamini kwenye shughuli za kila siku na pengine kutengeneza majipu makubwa ambayo hutishia uhai wa mhusika.
Hii ni kwa sababu majipu na maambukizi husika huweza kusambaa na kwenda sehemu mbalimbali za mwili.