Usihofu, tatizo la mdomo sungura linatibika

Muktasari:

  • Ni hali inayotokea kutokana na sehemu husika za uso kutofunga sawasawa wakati wa utengenezaji wake mtoto akiwa tumboni.

Mdomo sungura ni ile hali ya kuwa na uwazi ama nafasi katika mdomo wa juu jirani na pua.

Ni hali inayotokea kutokana na sehemu husika za uso kutofunga sawasawa wakati wa utengenezaji wake mtoto akiwa tumboni.

Mdomo sungura unaweza kuwa upande mmoja ama pande zote. Mtoto mwenye mdomo sungura pia anaweza akapata tatizo kama hilo kwenye paa la kinywa (kaakaa).

Ukubwa wa tatizo

Mdomo sungura pekee ama ukiunganika na kasoro kwenye kaakaa, huweza kutokea kwa kadiri ya wastani wa mtoto mmoja kati ya watoto hai 700 wanaozaliwa.

Watoto wa kiume wanakuwa na nafasi mara mbili zaidi ya kupata mdomo sungura pekee bila ama pamoja na shida kwenye kaakaa (Cleft palate) kuliko watoto wa kike.

Kwa upande mwingine, watoto wa kike hupata zaidi upungufu kwenye kaakaa bila kuhusisha kuwa na mdomo sungura

Mdomo sungura pekee ukiwa umeungana na mpasuko wa kwenye kaakaa, ni upungufu wa kawaida anaozaliwa nao mtoto. Kuwa na mtoto mwenye mdomo sungura inaweza kukutisha ama kuleta hali ya kujilaumu, lakini ukweli ni kwamba kasoro zote hizi zinarekebishika.

Kwa watoto wengi, upasuaji wa mara kadhaa huweza kurudisha hali ya kawaida ya ufanyaji kazi wa kinywa.

Dalili

Mara zote mdomo sungura ukiwa pekee ama unapohusisha kasoro kwenye kaakaa, hutambulikana mara tu mtoto anapozaliwa. Hali hii inaweza kutambuliwa kwa dalili zifuatazo:

Moja, mpasuko kwenye mdomo wa juu na kaakaa unaoathiri upande mmoja wa uso ama pande zote

Mbili, mpasuko kwenye mdomo wa juu wa mtoto ambao huanzia kwenye mdomo mpaka kwenye ufizi na kufikia kwenye pua.

Tatu, nafasi ama mpasuko kwenye kaakaa la mtoto ambao hauathiri muonekano wa sura ya mtoto

Mdomo sungura huonekana mtoto anapozaliwa na daktari husika hutoa taarifa kwa wazazi husika, ili kuwaelimisha na kuanza kushauri matibabu ya mtoto husika wakati huo huo

Nini husababisha hali hii?

Mdomo sungura hutokea wakati sehemu za uso na kinywa kwa ujumla zinaposhindwa kuunganika kikamilifu na hivyo kuacha uwazi.

Kitafiti inaaminika kwamba kinachosababisha kutokea kwa mdomo sungura, ni muingiliano wa chembechembe za kinasaba na mazingira

Ndio maana mara nyingi hakuna sababu moja maalumu inayotajwa kitaalamu kwamba ndio inayosababisha kutokea kwa hali hii kwa mtoto anapozaliwa

Sababu hatarishi

Kuna sababu kadhaa ambazo huweza kuongeza uwezekano wa kupata mtoto mwenye mdomo sungura; baadhi ni hizi zifuatazo:

Moja, historia ya familia. Wazazi wenye historia ya kuwa na mdomo sungura, wana nafasi kubwa ya kupata mtoto wa aina hiyo.

Mbili, matumizi ya baadhi ya vitu wakati wa ujauzito. Mdomo sungura pekee ama unapohusishwa na mpasuko wa kwenye kaakaa, inawezekana ukawa na nafasi kubwa zaidi ya kutokea miongoni mwa wajawazito ambao huvuta sigara, hunywa pombe ama wanaotumia dawa fulani fulani kipindi cha ujauzito.

Ndio maana inashauriwa unapokuwa mjamzito kabla hujatumia dawa yoyote, uonane na daktari wako na kuongea naye kuhusu madhara ya dawa hiyo na hali ya ujauzito wako.

Tatu, kuwa na kisukari. Kuna ushahidi kidogo wa kisayansi kwamba wanawake wanaopatikana na kisukari kabla ya kuwa wajawazito, wana uwezekano mkubwa wa kuzaa watoto wenye mdomo sungura

Nne, kuwa na unene uliopitiliza wakati wa ujauzito. Unene uliopitiliza umeonekana kisayansi unaweza kuchangia kupata mtoto mwenye mdomo sungura

Madhara zaidi

Watoto wenye midomo sungura pekee ama ambao midomo sungura imeambatana na mpasuko kwenye kaakaa, wana changamoto nyingi, mojawapo ni zifuatazo kulingana na ukubwa wa tatizo.

Moja, shida ya kumlisha. Moja ya changamoto kubwa baada ya kuzaliwa kwa watoto wenye midomo sungura ni ulishwaji wake. Hii ni kwa kuwa uwezo wake wa kunyonya ni mdogo

Mbili, matatizo ya meno. Kama mdomo sungura utasogea mpaka kwenye taya la meno, hali ya kawaida ya utengenezwaji, uotaji na mpangilio wa meno huathirika.

Tatu, kuongea kwa tabu. Kwa kuwa kaakaa hutumika kuumba sauti, hali ya kuzungumza kikawaida miongoni mwa watu wenye mdomo sungura huathirika. Mara nyingi sauti zao huonekana kutokea puani zaidi

Matibabu

Matibabu ya mdomo sungura huwa ni upasuaji ili kurekebisha hali hiyo na kuleta muonekano na ufanyaji kazi wa kawaida. Upasuaji hufanyika kwa namna ambayo itapunguza ukubwa wa kovu na ambalo litaendela kupotea taratibu kadiri mtoto anavyokua

Lengo la upasuaji huu ni kuboresha uwezo wa mtoto kula, kuzungumza na kusikia kikawaida pamoja na kuwa na muonekano wa sura wa kawaida.