VIDEO: Miaka 14 ya hedhi ya mateso

Maisha ni mapambano, si vyema kukata tamaa. Ni ujumbe unaoshabihiana na simulizi ya Sada Jinyevu (35), anayepitia mateso kila anapopata hedhi.

Licha ya hali ya kawaida ya hedhi, amekuwa pia akitokwa damu sehemu ya haja kubwa, kushindwa kula, kunywa maji na hata kutoka nje. Hupitia hali hii siku 20 ndani ya mwezi.

Kutokana na anayopitia, amekuwa akijichoma sindano kupunguza maumivu na kujitundikia dripu ya maji.

“Kila siku nachoma sindano mbili au tatu kulingana na maumivu. Nimeuza kila kitu cha ndani, hadi nguo ili kupata fedha ya kununua dawa,” anasema Sada huku akimalizia kujichoma sindano.

Sada ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga anasema maumivu hayo yanatokana na ugonjwa wa Endometriosis unaomtesa kwa miaka 14 sasa.

Kwa kipindi chote, anaishi akiwa na maumivu makali ya tumbo kabla, baada na wakati wa hedhi.

Endometriosis ni ugonjwa unaohusisha seli zinazofaa kuwa ndani ya mji wa uzazi kuwa nje ya mji huo, hivyo kusababisha maumivu makali wakati wa hedhi na kuathiri mishipa na mji wa uzazi.

“Hedhi kwangu imekuwa mapambano, ni kama vita ambayo sijui mwisho wake," anasema Sada.

Mwaka 2009 anasema ndio alianza kupata tatizo hilo la maumivu wakati wa hedhi, huku ndugu na watu wa karibu naye walimwambia ana tatizo la change.

Sada anasema walimweleza dawa za miti shamba zitamsaidia kumaliza tatizo hilo na itamwezesha kupata ujauzito.

“Kuna siku dada yangu aliambiwa na mtu wa tiba za asili akatafute mfupa wa mnyama yoyote kwenye jalala achanganye na dawa aliyopewa anichemshie ninywe. Nilikunywa bila kujua kama ilichanganywa na mfupa uliookotwa jalalani.

“Lakini hata kwa kufanya hivyo bado maumivu makali hayakuniacha, nilisafishwa kizazi, nimefanya upasuaji lakini bila mafanikio,” anasema.


Maumivu, matibabu

Sada anasema alianza tiba katika hospitali mbalimbali mkoani Tanga bila kupata nafuu, ndipo ndugu zake walimhamishia jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Mwaka 2009 hadi 2015 anasema aliishi kwa kutumia dawa na sindano za kupunguza maumivu kila alipoingia katika mzunguko wa hedhi.

“Nilitibiwa hospitali mbalimbali za Tanga nikiwa na kilio cha maumivu ya tumbo yasiyopungua. Nikiingia katika mzunguko wa hedhi, maumivu huwa makali. Siwezi kulala, kukaa wala kusimama na hapo sikuweza kula chakula chochote kwa siku nne,” anasema Sada.

“Hospitali walitaka nisafishwe wakati sijawahi kutumia uzazi wa mpango wala kutoa mimba, ila kwa kuwa ni mgonjwa ilibidi nijipange kufanya hivyo. Nilivyofanya hali ilibadilika.

“Maumivu yalizidi, sikupata haja kubwa, nilianza kupata maumivu hata siku ambazo sipo kwenye mzunguko wa hedhi.”

Anasema alipofikishwa Dar es Salaam kwa matibabu alipelekwa hospitali (jina linahifadhiwa) ambako baada ya vipimo alielezwa anapaswa kufanyiwa upasuaji wa dharura.

“Walinifanyia upasuaji tumboni lakini matibabu hayo hayakumaliza maumivu yangu ya tumbo," anasema na kuongeza kuwa ilibainika ana tatizo la kidole tumbo (appendex).

“Baada ya kufanyiwa upasuaji nilipoteza fahamu kwa siku nne, ziliponirudia nilikuwa na maumivu makali hadi nikahisi kuchanganyikiwa. Sikuwa namjua anayeingia wala kutoka. Nilikata tamaa, baada ya upasuaji nilihisi tatizo kuzidi kutokana na maumivu makali ya tumbo hata siku ambazo hazikuwa za hedhi, sikupata haja kubwa na sikuweza kula," anasema.

Sada anasema alirudi Tanga kuendelea na maisha yaliyogubikwa na maumivu makali. Baada ya matibabu anasema ndipo alipoanza kutoa damu ya hedhi sehemu ya haja kubwa ikiambatana na maumivu makali.

Anasema alipewa rufaa kwenda hospitali nyingine mkoani Tanga, ambako vipimo vilionyesha ana uvimbe katika mrija wa uzazi upande wa kulia.

Anaeleza alianza kuhudhuria kliniki lakini bado aliendelea kupata maumivu makali na kutetemeka.

“Maumivu huwa makali kwa siku mbili hadi tatu, kisha hedhi huendelea kutoka katika njia ya kawaida na sehemu ya haja kubwa. Ndugu zangu wamenisaidia hadi wamechoka, kwa kuwa matibabu yanahitaji fedha,” anasema Sada.

“Kutokana na ugonjwa unaonisumbua nimeacha biashara niliyokuwa naifanya kama wakala katika kampuni ya simu (anaitaja jina). Si rahisi kuendelea na biashara kwa sababu katika siku 30 naishi na maumivu makali kwa siku 20, hivyo biashara inayumba inakosa usimamizi," anasema.

Anasema kutokana na anayopitia amejifunza kujichoma sindano na kujitundikia dripu ili kujisaidia muda wowote anapopata maumivu bila kwenda hospitali.

Miaka 14 ya hedhi ya mateso

Kusaka matibabu

“Nimehangaika kutafuta tiba, nimechoshwa na maumivu ya tumbo na ya kukosa mtoto,” anasema Sada huku akinyanyuka kwenda kuchoma sindano ya pili kuzuia maumivu yaliyokuwa yanaanza.

“Sindano moja ni Sh2,000 kwa siku, ninaweza kuchoma mbili hadi tatu. Ili nishinde vizuri natakiwa nichome sindano, bora nisipate hela ya kula lakini nipate ya sindano.

“Nilirudi hospitali ile ile ya kwanza Tanga, katika kupimwa walitaka niwapelekee damu inayotoka katika sehemu ya haja kubwa ili wajue inatokea wapi, ilikuwa ngumu kuwapelekea niliwaomba kama wataruhusu niihifadhi niwapelekee siku nyingine maana kwa siku ile ingekuwa ngumu,” anasema Sada.

Anasema alipewa vidonge vya kuzuia asiingie katika hedhi hali inayomfanya aondoke katika maumivu hayo, lakini vidonge vikiisha nguvu maumivu hurejea.

“Nikimeza dawa nilikuwa napata choo kama kawaida, naweza kula chakula, damu hazitoki kwa kifupi naishi vizuri bila maumivu yoyote," anasema.


Kutoa kizazi

Anasema aliwekwa katika uangalizi maalumu katika hospitali hiyo aliyotakiwa kuhudhuria kliniki kila mwezi ambako daktari alimweleza tiba ya kudumu ya tatizo lake ni kuondoa kizazi.

Anasema alikubali, lakini changamoto ni wazazi wake, hasa baba yake mzazi, Omary Jinyevu.

Hata hivyo, baba mzazi anasema, “sijaona mtu akiuza mtoto, matatizo ya mwanangu ni ya kwangu, siwezi kumtenga mimi ni msaidizi wake, kiu yangu ni kuona anapata matibabu sahihi. Najiuliza je, akitolewa kizazi tatizo hilo litaisha? Nawaomba Watanzania wenye uwezo wa kumsaidia kwa hali na mali wamsaidie ili tumuokoe mtoto huyo.”


Hali ilivyo sasa

Sada hajakata tamaa ya kusaka matibabu sahihi yatakayomtoa katika maumivu ya tumbo na kukata kiu yake ya kupata mtoto.

Anasema ameshindwa kubeba mimba kwa sababu ya ugonjwa huo.

Sada anasema akiwa katika maumivu hawezi kushiriki tendo la ndoa na kwamba, mume wake amebeba tatizo lake na wakati mwingine humsaidia kumchoma sindano na kumwekea dripu.

“Namshukuru Mungu amenipa mume sahihi, ni dereva wa magari ya mizigo lakini kwa kazi yake hii amenikubali na matatizo yangu na amejifunza kuchoma sindano ili aweze kunisaidia,” anasema.

Anamtaja Dk Joseph Mberesero wa Hospitali ya Safi Medics mkoani Tanga kuwa ndiye aliyetambua tatizo lake la endometrioses baada ya kumfanyia vipimo.

“Daktari amesema nifanye kipimo kinachogharimu Sh350,000 ili kuangalia kama nina tatizo gani linalosababisha nishindwe kula. Ingawa ameshajua tatizo la endometriosis. Nawaomba Watanzania wanisaidie kwa namna yoyote ili niweze kufanya matibabu haya,” anasema.

Dk Mberesero bingwa wa magonjwa ya wanawake, uzazi na utasa anasema Sada ana tatizo la endometrioses likiwa katika hatua ya nne ambayo ni mbaya.

Anasema amekutana na wanawake wenye matatizo kama hayo wakiwa katika hatua mbaya, akitoa mfano wa Sada na kubainisha wengi wenye tatizo hilo wanapata matibabu yasiyo sahihi.

“Kwa hatua ya nne ya ugonjwa wa endometriosis, huwa imesambaa kwenye njia zote za uzazi na wakati mwingine inaweza kuwa imeanzia kwa njia za uzazi kutoka nje. Inaweza kuwa imeshahama kwenda maeneo ya mbali, inaweza kwenda kwenye kichwa, kifua na hata katika mkono, ukipata hedhi na yenyewe pale ilipo ina breed (toa damu) kama kizazi kinapotoa damu ya hedhi,” anasema Dk Mberesero.

“Wanapata matibabu mbalimbali kwa uelewa wa madaktari ambao wanawaona, kwa bahati mbaya si wote wanaotibu wana elimu ya endrometrisis. Nitoe wito kwa madaktari wenzangu kutoa elimu kwa wazazi, anapoona mtoto wa kike anapata maumivu makali wakati wa hedhi amfikishe katika kituo cha afya. Kitu hiki kinapokuwa cha muda mrefu ndiyo athari kubwa inavyokuwa kwa sababu endometriosis inaua kizazi."


Hali ya tatizo la Sada

Kuhusu hali ya Sada ilipofikia, Dk Mberesero anasema ni mbaya kwa sababu imeenda sehemu ya haja kubwa na ndiyo husababisha kutoka damu ya hedhi sehemu hiyo.

“Ugonjwa umeenda hadi katika sehemu ya haja kubwa, hivyo upasuaji utahitaji daktari wa tumbo aweze kuondoa kipande kilichoota katika utumbo. Mimi kama daktari wa uzazi niangalie ninaweza kukilinda kizazi cha Sada ili aweze kuzaa au tunaangalia kuokoa maisha ya mtu aliye hai, tukiona hakuna namna tutatoa kizazi kwa kumshauri mgonjwa,” anasema Dk Mberesero.


Imeandikwa kwa kushirikiana na Bill & Melinda Gates