Vifahamu vipimo muhimu vya afya vinavyosahaulika na wengi
Muktasari:
Takwimu za Shirika la Afya Duniani
(WHO) zinaonyesha ni asilimia 39 tu ya
wanaume watu wazima wanaopata vipimo
vya afya wakilinganishwa na asilimia 71 ya
wanawake wanaofanya hivyo kabla hawajaugua
chochote.
Vipimo ni muhimu kwa maendeleo
ya afya ya mwanadamu bila kujali
umri wala jinsia. Kupitia vipimo
tunaweza kutambua mustakabali wa afya
zetu hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri
ya kupambana na maradhi mbalimbali.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani
(WHO) zinaonyesha ni asilimia 39 tu ya
wanaume watu wazima wanaopata vipimo
vya afya wakilinganishwa na asilimia 71 ya
wanawake wanaofanya hivyo kabla hawajaugua
chochote.
Kupata vipimo sahihi na kwa wakati
ni kitu muhimu ambacho mtu anapaswa
kukifanya kwa kujali afya yake. Kufanya
vipimo kunasaidia kuyagundua magonjwa
mapema kabla hayajaanza kuonyesha dalili
wakati ambao ni rahisi zaidi kutibika.
Magonjwa mfano saratani, kisukari, na
mengine hasa yasiyoambukiza yakigundulika
mapema, husaidia kumuepusha
mgonjwa na madhara makubwa anayoweza
kuyapata katika matibabu yake mfano
kupoteza nguvu za kiume au uwezo wa
kuona hata vifo cha mapema zaidi.
Kupitia makala hii tutaviona baadhi ya
vipimo muhimu ambavyo wengi hawavitilii
maanani ila vikiendelea kusahaulika,
madhara yake ni makubwa.
Tezi dume
Kuna wanaume wachache wanaofikiria
kufanya vipimo vya tezi dume. Mwanaume
anakuwa hatarini zaidi kupata tezi dume
kadri umri unavyozidi kusogea kuanzia
umri wa miaka 50 hivi.
WHO limethibitisha kuwa tezi dume ni
ugonjwa unaoua zaidi sababu kubwa ikiwa
kutopata vipimo mapema hivyo kuwahi
matibabu yake.
Habari njema ni kwamba, tezi dume ni
moja ya aina chache za saratani ambayo
uwezekano wa kupona upo kwa zaidi ya
asilimia 90 iwapo itagundulika katika hatua
za awali.
Hivyo, ni vyema kufanya vipimo vya saratani
mara kwa mara hasa kwa wenye umri
wa zaidi ya miaka 55.
Saratani ya utumbo mpana
Saratani ya utumbo mpana ni moja ya
saratani zinazoua kwa kasi. Japo takwimu
zinaonyesha wanaume wana nafasi ndogo
zaidi ya kupata ugonjwa huu kuliko
wanawake, hii haimaanishi wajisahau hasa
tukizingatia inaweza kumpata mtu yeyote.
Mara zote saratani ya utumbo mpana
inaanza kwa kuota uvimbe mdogo ndani
ya ukuta wa utumbo na kadri uvimbe
unavyoongezeka ndivyo saratani inavyoongezeka.
Njia ya kuzuia saratani hii ni kuondoa uvimbe huu unaoota mapema kabla ya kutokea kwa saratani husika. Njia pekee ya kuugundua uvimbe huu ni kufanya vipimo.
Inashauriwa kufanya vipimo vya saratani ya utumbo mpana mara kwa mara kwa wenye umri zaidi ya miaka 50 kwa sababu katika umri huu mtu anakuwa hatarini zaidi kupata ugonjwa huu.
Saratani ya ngozi
Aina hii ya saratani kwa kitaalamu inajulikana kama melonoma. Inasababishwa na uzalishwaji mwingi wa seli kuliko zinazohitajika mwilini. Seli hizi zinaitwa melanocytes ambazo huathiri ngozi kwa kubadili rangi na muonekano wa ngozi.
Saratani hii huwashambulia zaidi wanaume kuliko wanawake. Takwimu zinaonyesha hali hiyo hutokea mara tatu zaidi kwa wanaume kutokana na sababu za kibailojia. Lakini sababu hatarishi za ugonjwa huu kwa ujumla wake ni kupigwa na jua kwa muda mrefu zaidi.
Hivyo inashauriwa kufanya vipimo vya ngozi mara kwa mara hasa zinapojitokeza kwenye ngozi kama vile kubadilika kwa maumbile ya ngozi, kubadilika kwa rangi ya ngozi au kujitokeza kwa chunusi sugu mara kwa mara kwa kuwa hizi ndizo dalili zake. Tiba ya magonjwa ya ngozi inaleta tija zaidi wakati ambapo vipimo vikifanywa kwa wakati na kugundua tatizo.
Shinikizo la juu la damu
Hatari ya kupata shinikizo la juu la damu huongezeka kadri umri unavyosogea licha ya ukweli kwamba lina uhusiano mkubwa na uzito uliopitiliza. Mtindo wa maisha pia ni kichocheo kingine hasa ulaji wa vyakula vyenye mafuta kwa wingi na kutofanya mazoezi mara kwa mara hata sababu za kisaikolojia.
Shinikizo la juu la damu humpata mtu bila dalili zozote na linaweza kuleta madhara makubwa kama vile magonjwa ya moyo, kiharusi au kusababisha figo kushindwa kufanya kazi.
Hivyo ni muhimu kujua vipimo vya shinikizo la damu mara kwa mara kwa na kama vinaashiria kupanda ni vyema kupata msaada wa daktari mapema.
Lehemu
Lehemu ni muhimu mwilini lakini inahitajika kwa kiasi kidogo sana. Lehemu ni malighafi ambayo mwili inayatumia kutengeneza vitu vingine mwilini vikiwamo baadhi ya vichocheo au homoni.
Hata hivyo, kiwango kikubwa cha lehemu mwilini kinaweza kudumu kwa miaka kadhaa bila dalili zozote na kusababisha kuziba kwa mirija ya damu mbalimbali hivyo kuongeza hatari ya kupata magonjwa mbalimbali kama ya moyo na kiharusi.
Ni vyema kuzitambua sababu zinazochangia uwapo wa lehemu nyingi mwilini ambazo zinajumuisha ulaji wa mafuta kwa wingi na kutofanya mazoezi mara kwa mara.
Ni vyema kufanya vipimo ili kujua kama una lehemu mbaya au nzuri kwa afya yako. Kwa kufanya hivyo utakua umejiepusha na magonjwa sugu kama vile shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na kiharusi.
Kwa walio hatarini kupata magonjwa ya moyo wanashauriwa kuanza vipimo kuanzia wakiwa na miaka 20 na ni vyema kufanya vipimo vya lehemu mara kwa mara kuanzia miaka 35 hata kama haupo kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Kisukari
Takwimu zinaonesha wanaume wapo hatarini zaidi kupata kisukari kuliko wanawake. Ni ugonjwa unaotokana na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu.
Huenda ikasababishwa na aina fulani ya maisha kama vile ulaji wa vyakula vinavyosababisha kisukari, kutofanya mazoezi hata kurithi.
Japo kisukari kinaweza kuwapata watu wa rika zote, inashauriwa kupata vipimo mara kwa mara kwa kuwa hasa kwa wenye umri wa zaidi ya miaka 45.
Glaukoma
Huenda likawa neno ngeni kwa wengi, glaucoma au glaucoma ni ugonjwa ya macho unaoshambulia kuharibika kwa neva zilizopo ndani ya macho na kusababissha upofu wa kudumu.
Glaukoma inaweza kutokea bila dalili yeyote hadi mgonjwa anapopoteza uwezo wa kuona. Ni muhimu kupata vipimo vya macho mara kwa mara kubaini madhara yeyote yanayojitokeza kwenye macho.
Ni ukweli usipongika kuwa watu wengi hawana utamaduni wa kupima macho hadi wanapobaini dalili kama vile matatizo ya kuona, macho kuuma na kuwasha au kutoa machozi.
Ni vyema ikafahamika kuwa glaukoma inashambulia jicho bila kuwa na dalili zozote hivyo ni vyema kufanya vipimo mara kwa mara hata kama hauna tatizo lolote.
Vipimo hivi vinashauriwa kufanywa kwa kuzingatia umri na mazingira hatarishi. Aidha, wenye chini ya miaka 40 wanashauriwa wafanye vipimo kila baada ya miaka miwili mpaka minne wakati wenye kati ya miaka 40 na 54 wafanye kila baada ya mwaka mmoja mpaka mitatu na zaidi ya miaka 55 iwe mara mbili kwa mwaka mmoja.