Wanachosema wanawake kuhusu uzazi wa mpango

Muktasari:

  • Jamii bado inahitaji kupewa elimu sahihi kuhusu uzazi wa mpango

Uzazi wa mpango ni miongoni mwa mambo yanayoibua changamoto katika familia nyingi.

Wapo wanaoamini kuwa ni vyema kutumia njia za asili za uzazi wa mpango na wengine wakiamini za kisayansi.

Wanaotumia njia za asili wanaamini kuwa hazina madhara na kinachohitajika ni umakini tu na kujua mabadiliko ya mwili na tarehe za kushika ujauzito.

Baadhi ya njia za uzazi wa mpango za kisayansi ni pamoja na sindano, kijiti, vidonge, mipira ya kiume na kitanzi.

Lakini wanawake kama wahusika wakuu wanazungumziaje njia wanazotumia kuzuia ujauzito?

Neema Rahim Mshumbusi, mkazi wa Mabibo, Dar es Salaam ni mama wa watoto wawili, anasema anatumia kalenda na amekuwa akitumia njia hiyo tangu alipoolewa.

“Ninatumia zaidi kalenda, ingawa ni hatari kidogo endapo utakosea tarehe zako au kama haupo makini kujua tarehe zako za kushika mimba. Ila mimi njia hiyo naiamini zaidi,” anasema Mshumbusi.

Anasema ili kufanikiwa katika kutumia njia hiyo, ni muhimu zaidi kushirikiana na mwenza kwa sababu endapo baba hatashirikishwa na kujua umuhimu wa kuheshimu kalenda basi ni rahisi kupata mimba zisizotarajiwa.

“Kama ni tarehe za hatari halafu baba akawa hajali au hajashirikishwa, basi hilo suala la kalenda ni gumu sana. Kwenye haya mambo baba/ mwenza ni muhimu zaidi,” anasema.

Fidelis Mwambona, mkazi wa Buguruni anasema, ni vigumu kutumia njia ya kalenda kwa sababu ambazo zipo nje ya uwezo wake na hawezi kuzitaja.

“Ninalazimika kutumia njia za kisayansi, mimi natumia kitanzi, hiki hakina vichocheo vinavyoweza kunifanya nikabadilika au nikakosa siku zangu za hedhi,” anasema Mwambona.

Mwambona anasema amewahi kutumia njia nyingine za uzazi wa mpango kama vidonge na sindano na vyote vilimpa madhara.

“Kuna wakati unapata siku za hedhi mfululizo, yaani hata mwezi mzima. Nilipoanza kutumia sindano ndipo nilipokutana na tatizo hilo, nikaacha. Nikahamia kwenye vidonge navyo vikawa vinanipa kichefuchefu yaani najihisi kama mjamzito kabisa,” anasema.

Lakini baadhi ya wanawake wanasema njia za kisayansi zinawasaidia zaidi kwa sababu kalenda ni hatari na inaweza ikasababisha mimba isiyotarajiwa.

“Mimi niliwahi kutumia kalenda, nikahisi nipo sawa kabisa na sijafanya tendo la ndoa siku za hatari, lakini nilishangaa nimeshika mimba, wakati huo mtoto wa kwanza ana miezi tisa, nilipagawa sana,” anasema Mwambona.

Anasema tangu wakati huo ameamua kutumia njia ya uzazi wa mpango ya sindano, ingawa ina madhara yake lakini ina uhakika.

Akizungumzia matumizi ya njia za uzazi wa mpango, Muuguzi Mkuu kutoka Manispaa ya Kinondoni, Nusura Kesi anasema jamii bado inahitaji kupewa elimu sahihi kuhusu uzazi wa mpango.

“Ukifika kituoni utapata elimu wewe kama wewe, Usisikilize elimu aliyopata mtu mwingine ukaitumia wewe, huenda wewe una tatizo la kiafya, hivyo njia fulani inakusumbua kutokana na afya yako, ni vizuri kusikia kutoka kwa mhudumu wa afya. Unaweza ukasema hii njia ni mbaya, lakini kumbe ungeelimishwa, ungepata njia inayokusaidia wewe,” anasema Kesi.

Pia, anasema njia za uzazi wa mpango inahitaji ushirikiano wa watu wote, kuanzia mama, baba na wahudumu wa afya.

“Sisi hatuzuii mtu azae, bali tunashauri njia za uzazi wa mpango, ili kuwe na nafasi kati ya mtoto na mtoto,” anasema Kesi.

Muuguzi huyo anasema bado kuna mwamko mdogo wa kinababa kushiriki katika masuala ya uzazi wa mpango hata kwa njia ile ya asili.

“Sisi kama wahudumu wa afya na wizara, bado tunaona kuna mwamko mdogo wa kinababa kushiriki katika masuala haya, hivyo tunaomba, kinababa waambatane na wake au wenza wao wakapate elimu hii (uzazi wa mpango), ili pindi mama anaposahau baba amkumbushe.”

Mganga Mfawidhi kituo cha afya cha Tandale, Dk Emmanuel Kazimoto anasema mwanamke anapofika kituo cha afya, anaelimishwa na kisha anachagua njia ya kutumia.

“Lakini kuna majadiliano kati ya mhudumu wa afya na mama atashauriwa kuhusu njia za uzazi wa mpango zilizopo kabla ya kuchagua njia ipi ni bora ya uzazi wa mpango,” anasema Dk Kazimoto.

Utafiti wa Tamwa

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kilifanya utafiti na kutoa elimu kwa vikundi vya kuweka na kukopa (Vicoba) katika kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni.

Baada ya elimu hiyo, ilibainika kuwa kuna ongezeko la uelewa wa uzazi wa mpango miongoni mwa wanachama wa Vicoba.

Meneja tathmini na ufuatiliaji wa Tamwa, John Ambrose anasema Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni iliafiki kuwatumia wauguzi na wahudumu wake wa afya kwenda kutoa elimu kwa vikundi vya Vicoba vya wanawake katika kata sita za Kinondoni.

“Hili ni jambo tunalolishukuru sana kwa Wilaya ya Kinondoni kuwatumia wahudumu wake wa afya kutoa elimu. Hata baada ya elimu hiyo tumeona mabadiliko makubwa kwa kinamama kujitokeza kwa wingi kupata elimu na kuanza kutumia njia hizo,” anasema.

Pia, Ambrose anasema halmashauri hiyo imekubali kutoa huduma za elimu ya uzazi wa mpango katika mpango wake wa huduma za nje kwa vikundi vya kinamama katika mwaka wa fedha 2019/20.