Zingatia ulaji kiasi wa nyama nyekundu

Tafiti zinaonyesha ulaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kuwa hatari na ni kati ya vyakula vinavyosababisha aina mbalimbali za saratani kama ya kinywa, koo, utumbo mpana, mapafu na kongosho.

Nyama nyekundu ni pamoja na nyama ya ng’ombe, nguruwe, kondoo, mbuzi, sungura na wanyama wote wenye miguu minne.

Nyama hizi zinatajwa kuwa na lehemu kwa wingi ambayo huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, shinikizo kubwa la damu, saratani, kisukari na kiharusi.

Ingawa nyama nyekundu ni chanzo kizuri cha virutubisho vya protini, lakini katika kuepuka hatari hizo ni vema ziliwe angalau mara moja kwa wiki.

Inashauriwa kutumia zaidi nyama nyeupe ambayo ni pamoja na kuku, bata mzinga na samaki au vyakula vingine vyenye protini kama maharage, kunde, mbaazi na aina nyingine za mbegu mbegu.

Mgonjwa wa kisukari anatakiwa kuepuka nyama nyekundu, hasa zilizosindikwa kwa sababu huwa na sodiamu nyingi, nitriti na nitrati, ambazo zote zimekuwa zikihusishwa na matokeo mabaya ya afya. Mfano wa nyama hizo ni soseji na nyama za kopo. Kwa wagonjwa wa kisukari, ni bora zaidi kutumia vyanzo vingine vya vyakula vyenye protini kama maharage, soya, karanga, mbaazi na kunde kwa sababu hazina mafuta au lehemu, yana protini, nyuzinyuzi na vitamini mbalimbali na virutubisho vya amino.

Vyanzo hivi vina virutubisho vya protini ambavyo husaidia kushusha kiwango cha lehemu mbaya mwilini, pia hupunguza ugandaji wa damu, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupata mshituko wa moyo au kiharusi.

Pia husaidia kuboresha msukumo na mishipa ya damu mwilini. Kumbuka kuwa protini mwilini huongeza uwezo wa mwili kuhifadhi na kunyonya madini ya calcium kwenye mifupa.